Jumatatu, 19 Mei 2025

MAHAKAMA KUU KANDA YA TABORA YAZINDUA SHUGHULI ZA MAHAKAMA KIPILI

Na AMANI MTINANGI – Mahakama-Tabora

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora imeanza rasmi kutoa huduma za kimahakama katika Kata ya Kipili iliyopo katika Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora kuanzia tarehe 17 Mei, 2025 ikiwa ni hatua muhimu katika kusogeza huduma za kimahakama karibu zaidi na wananchi.

Uzinduzi huo umefanyika rasmi kwa ushirikiano na viongozi wa kisiasa na watendaji wa Serikali za Mitaa. Katika tukio hilo la kihistoria Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Sikonge, Mhe. John Mdoe alihutubia wananchi wa Kipili na kueleza kuwa huduma hizo ni sehemu ya mkakati wa Mahakama ya Tanzania wa kuhakikisha upatikanaji wa haki unatolewa kwa wananchi wote kwa haraka na kwa gharama nafuu.

Mhe. Mdoe alisisitiza kuwa, kuwepo kwa huduma hizo katika Kata ya Kipili kutapunguza safari ndefu za kutafuta haki huku akihimiza wananchi kujitokeza pale wanapohitaji msaada wa kisheria.

“Huduma hizi ni sehemu ya mkakati wa Mahakama ya Tanzania kuhakikisha kuwa haki inapatikana kwa haraka, kwa gharama nafuu, na kwa kila mwananchi popote alipo. Kupitia hatua hii ya kuanza kutoa huduma Kipili, tunapunguza safari ndefu za wananchi kusaka haki, hivyo nawahimiza wote mjitokeze pale mnapohitaji msaada wa kisheria Mahakama ipo kwa ajili yenu,” alisema Mhe. Mdoe.

Kabla ya kuzungumza na wananchi, Mhe. Mdoe alifanya kikao cha ndani na baadhi ya watendaji na maafisa kutoka taasisi mbalimbali za umma wanaofanya kazi katika Kata ya Kipili. Kikao hicho kililenga kuweka mikakati ya ushirikiano wa karibu baina ya Mahakama na taasisi hizo ili kuhakikisha huduma za haki zinatolewa kwa ufanisi.

Wakati wa hafla hiyo, Diwani wa Viti Maalum katika Kata ya Kipili, Mhe. Christina Singiwa alitoa pongezi kwa Mahakama kwa hatua hiyo muhimu huku akisisitiza kuwa huduma za haki ni hitaji la msingi kwa jamii na kwamba upatikanaji wake utasaidia kupunguza migogoro isiyo ya lazima.

"Tunaishukuru Mahakama kwa kuona umuhimu wa Kipili kupata huduma hii, wananchi wetu sasa wataweza kupata haki bila kusafiri kilometa nyingi. Kama viongozi wa eneo hili, tutaendelea kushirikiana na Mahakama katika kuhakikisha amani na utulivu vinatawala," alisema Mhe. Christina..

Katika hatua ya mwanzo, jumla ya mashauri matatu (3) yalisikilizwa siku ya kwanza na Mhe. Winifrida Magai, Hakimu Mkazi aliyeteuliwa kuendesha mashauri hayo. Zoezi hilo lilitekelezwa kwa mafanikio makubwa na kupokelewa kwa shukrani na matumaini kutoka kwa wananchi waliokuwa na mashauri ya muda mrefu yaliyokuwa hayajapatiwa ufumbuzi.

Kuanzishwa kwa huduma hizi si tu kwamba ni suluhisho la muda mrefu kwa changamoto za kisheria, bali pia ni ishara ya mageuzi ya kiutawala katika utoaji wa haki. Wananchi sasa wanaweza kusikilizwa ndani ya kata yao, jambo ambalo ni msingi wa amani, maendeleo na haki za binadamu.


Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Sikonge, Mhe. John Mdoe akihutubia wananchi wa Kata ya Kipili tarehe 17 Mei, 2025 wakati wa uzinduzi rasmi wa huduma za kimahakama katika eneo hilo.

Sehemu ya wananchi wa Kipili wakifuatilia kwa makini hotuba ya uzinduzi wa huduma za Mahakama ya Mwanzo Kipili, tukio lililofanyika kwa mara ya kwanza katika Kata yao.

Diwani wa Viti Maalum, Mhe. Christina Samweli Singiwa akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wananchi wa Kata ya Kipili.


Mwananchi wa Kata ya Kipili akiuliza swali kwa Mhe. John Mdoe wakati wa mkutano wa hadhara uliofuatia uzinduzi wa huduma za Mahakama. Maswali mengi yalilenga namna ya kupata haki kwa urahisi na ushauri wa kisheria.

Mhe. John Mdoe (wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Maofisa wa Taasisi za Umma na viongozi wa Kata ya Kipili baada ya kikao kazi kilichofanyika kabla ya uzinduzi wa Mahakama hiyo.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni