Na SETH KAZIMOTO, Mahakama-Arusha
Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Robert Makaramba amewaasa Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania juu ya usimamizi Madhubuti wa Mahakama katika vituo wanavyosimamia kwa kuwa mfano bora kwa wtumishi walio chini yao katika kuonesha maadili mazuri na uwajibikaji wa kiwango cha juu.
Mhe. Makaramba aliyasema hayo katika Mafunzo ya Majaji Wafawidhi na Wadau wa Mahakama ambayo yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya “Corridor Springs” jijini Arusha tarehe 15 na 16 Mei, 2025.
Akitoa mada kuhusu “Kanuni za Maadili ya Uongozi na Uadilifu” na “Uwajibikaji, Kukasimu majukumu na Usimamizi na matumizi mazuri ya muda” Jaji Makaramba alisisitiza kuwa, Majaji Wafawidhi wanao wajibu wa kuonesha viwango vya hali ya juu vya maadili kwa watumishi walio chini yao katika jukumu zima la kusimamia utoaji haki.
Mhe. Makaramba alisema kuwa, heshima na utu wa Jaji
havipatikani kwa kutumia nguvu au vitisho kwa walio chini yake, bali hutokana
na vitendo na mwenendo wa kimaadili wa Jaji husika.
Aliongeza kwa kuwaasa majaji Wafawidhi juu ya umuhimu wa kuwa mifano bora ya kuigwa katika suala zima la maadili kwa watumishi wanaowaongoza katika vituo vyao vya kazi ili watumishi waige maadili mazuri kutoka kwa viongozi wao.
Kadhalika alisema kwamba, uwajibikaji, kukasimu majukumu na kusimamia matumizi mazuri ya muda ni jukumu linaloenda mbali zaidi ya wigo wa utoaji Haki, ambapo kiongozi anapokasimu majukumu haimuondoi katika wajibu wake wa moja kwa moja wa kumsimamia mtumishi ambaye amempa majukumu.
“Viongozi lazima wakasimu majukumu yao kila inapolazimu huku wakijua kuwa hiyo ni namna mojawapo ya kuwasimamia hao waliopewa majukumu, na viongozi wanao wajibu wa kuchukua hatua stahiki mara tu wanapogundua kuwa watu waliopewa majukumu hawafanyi wajibu wao kama ilivyotarajiwa,” alisisitiza Jaji Makaramba.
Pia alisisitiza kuwa, Kiongozi mzuri ni msikivu na lazima
awe na dira ikiwa ni pamoja na kuipa motisha timu yake na kufanya uamuzi ambao
yananufaisha timu nzima.
Jaji Makaramba alieleza kuwa, ili kufikia malengo ya taasisi yoyote, ni muhimu kwa uongozi kujua hali halisi waliyonayo watumishi wake katika nyanja mbalimbali ikiwemo kiuchumi, na si kuwataka watumishi kufanya kazi tu bila kujali watumishi hao wanaumia kwa kiasi gani.
Kadhalika, Jaji huyo mstaafu aliesema kwamba, ili
Mahakama na Taasisi zingine ziwe na maadili endelevu, hawana budi kujenga
utamaduni wa uadilifu, kuweka na kuzingatia kanuni za maadili, viongozi
kuongoza kwa kuwa mfano wa kuigwa, kuwajengea uwezo watumishi, kuwatambua na
kuwapongeza watumishi wanaofuata maadili ya kazi ikiwa ni pamoja na kuwaadhibu
watumishi wanaokiuka maadili ya kazi kwa mujibu wa taratibu zilizopo.
Alihitimisha kwa kusema kuwa, Uhuru wa Mahakama ni nguzo muhimu ili kuwa na ufanisi, ikizingatiwa kuwa Mahakama ndio chombo ambacho watu wanategemea kupata haki.
Jaji Msataafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Robert Makaramba akitoa mada wakati wa Mafunzo ya Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu Tanzania na Wadau wa Haki Kazi yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Corridor Springs jijini Arusha tarehe 15-16 Mei, 2025.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Arusha)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni