Ijumaa, 16 Mei 2025

MKURUGENZI 'ILO' AFRIKA MASHARIKI AAHIDI KUENDELEZA USHIRIKIANO NA MAHAKAMA YA TANZANIA

  • Afurahishwa na ushiriki wa dhati na mijadala yenye tija ya Majaji Wafawidhi na Wadau wa haki madai

Na MARY GWERA, Mahakama-Arusha

Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Ukanda wa Afrika Mashariki, Bi. Caroline Mugala amekiri kufurahishwa na Ushirikiano uliopo kati ya Shirika la Kazi Duniani na Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Tanzania huku akionesha furaha yake kufuatia mafanikio yaliyopatikana katika Kikao cha Haki Kazi baina ya Shirika hilo na Majaji Wafawidhi na wadau wa haki kazi.


Bi. Mugala amebainisha hayo leo tarehe 16 Mei, 2025 alipokuwa akifunga kikao kazi cha siku mbili kilichohusisha Majaji Wafawidhi pamoja na Wadau wa haki kazi kilichofanyika katika Hoteli ya ‘Corrridor Springs’ jijini Arusha.

 

“Mafunzo haya ni hatua nyingine muhimu katika ushirikiano wa Shirika la Kazi Duniani na Mahakama ya Tanzania katika kuimarisha haki za kazi na kuendeleza kazi zenye staha kwa maadili ya uongozi hadi mageuzi ya kidijitali kutoka viwango vya kimataifa vya kazi hadi mijadala ya kijamii,” amesema Mkurugenzi huyo.

Bi. Mugala amesema kuwa, amefurahishwa hasa na wingi wa mitazamo na madhumuni madhubuti iliyowasilishwa na kujadiliwa  wakati wote wa kikao kazi hicho na kwamba ana imani elimu hiyo ya pamoja itaendelea kuunda Mahakama ya Kazi yenye ufanisi zaidi na yenye kuzingatia haki.

Ameongeza kwa kuahidi kuwa, Shirika la Kazi Duniani litaendelea kutoa ushirikiano kwa Mahakama ya Tanzania hususani Divisheni ya Kazi ili kuendelea kuboresha haki kazi.

Kadhalika, ametoa shukrani zake kwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani kwa kufungua kikao kazi hicho pamoja na uongozi wa Mahakama ya Kuu Divisheni ya Kazi chini ya Jaji Mfawidhi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina kwa kufanikisha uratibu wa kikao hicho.

Awali akizungumza wakati akitoa majumuisho ya Kikao Kazi hicho, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina amelishukuru kwa dhati Shirika la Kazi Duniani (ILO) kwa ushirikiano wanaoendelea kuutoa kwa Mahakama hiyo unaolenga kuboresha haki kazi.  


Mhe. Mlyambina amewakumbusha washiriki wa kikao kazi hicho kuwa ni  muhimu kuzingatia kaulimbiu ya kikao hicho isemayo; ‘Uboreshaji wa Uongozi kwa Ufanisi na Tija katika Utoaji wa Haki Kazi’.

Kadhalika, amewakumbusha pia yaliyosisitizwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani wakati wa ufunguzi wa kikao hicho ambapo alisisitiza juu ya kuhakikisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yanaimarishwa ili kuboresha huduma, kuongeza uwazi na uwajibikaji katika kushughulikia mashauri yote, yakiwemo yanayohusu migogoro ya kazi mahakamani.

Aidha, Mhe. Dkt. Mlyambina aliwadokeza washiriki wa kikao hicho kuhusu mada zilizowasilishwa na Wawezeshaji na kuzielezea kwa ufupi kila moja. Miongoni mwa mada zilizotolewa ni pamoja na Uongozi (Leadership); Motisha kwa watumishi na kujenga ujasiri (motivating employees and building confidence); Kanuni za Maadili za uongozi na Uadilifu (Leadership Code of ethics and Integrity); Utatuzi Mbadala wa Migogoro ADR, kupitia Upatanishi, na Usuluhishi (ADR, through Mediation, and Arbitration) na kadhalika.

Aidha, Majaji Wafawidhi pamoja na wadau wa haki kazi walioshiriki katika kikao hicho walipatiwa vyeti ikiwa ni ishara ya kushiriki ipasavyo katika kikao kazi hicho.

Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Ukanda wa Afrika Mashariki, Bi. Caroline Mugala (kulia) akifurahia zawadi anayopatiwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi wakati wa hafla ya kufunga kikao kazi cha haki kazi kilichoshirikisha Majaji Wafawidhi na Wadau kilichofanyika jijini Arusha tarehe 15 na 16 Mei, 2025.  



Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina akiwasilisha majumuisho ya kikao kazi cha Majaji Wafawidhi pamoja na wadau wa haki kazi leo tarehe 16 Mei, 2025 jijini Arusha.
   

Sehemu ya Washiriki wa kikao kazi hicho wakifuatilia kinachojiri katika hafla ya kufunga.

(Picha na MARY GWERA, Mahakama-Arusha)








 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni