- Miradi ya ujenzi Mahakama za kisasa yasambaa nchi nzima
- Jengo la Makao Makuu utalii wa majengo ya Mahakama kimataifa
Na FAUSTINE
KAPAMA, INNOCENT KANSHA-Mahakama, Geita
Mahakama ya Tanzania inaendelea na
utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi na ukarabati wa majengo, kupitia Mpango
Mkakati wake wa Miaka Mitano unaotekelezwa sambamba na Mpango wa Miaka Mitano wa
Maendeleo ya Miundombinu (2020/21-2024/25).
Hayo yamebainishwa na Mtendaji Mkuu wa
Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel leo tarehe 21 Mei, 2025
alipokuwa anazungumza na Waandishi wa Habari kupitia Vyombo mbalimbali mkoani
hapa kuhusu maboresho ya miundombinu ya Mahakama katika kipindi maalum cha
kila mwezi.
‘Miradi hii inatekelezwa kwa ngazi
zote za Mahakama kuanzia Mahakama ya Rufani hadi Mahakama za Mwanzo, kupitia
fedha za maendeleo kutoka Serikali Kuu pamoja na ufadhili wa Benki ya Dunia,’
amesema.
Mtendaji Mkuu amewaeleza Waandishi wa
Habari kuwa utekelezaji wa miradi hiyo unapitia katika hatua mbalimbali ambapo
usanifu wake umejikita katika kuzingatia vipaumbele vitano.
Amevitaja vipaumbele hivyo kama mazingira
bora ya kufanyia kazi katika ofisi mbalimbali na urahisi wa kufikika miundombinu wezeshi kwa makundi maalum,’ amesema.
Mtendaji Mkuu amebainisha vipaumbele
vingine kama matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma na uendeshaji wa
shughuli za Mahakama, ulinzi na usalama kwa watumiaji wa jengo na muonekano na taswira
pekee ya Mahakama.
Prof. Ole Gabriel ametaja miradi ya
ujenzi kwa mwaka wa fedha 2024/25 kama ujenzi wa jengo la Makao
Makuu ya Mahakama-Dodoma na ujenzi wa nyumba za Majaji-Dodoma, ambao umeshakamilika.
Majengo hayo yalizinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 5 Aprili, 2025.
‘Jengo hili la Makao Makuu ni jengo la kifahari,
jengo ambalo ni la kihistoria, jengo ambalo ukubwa wake wa sakafu ni mita za
mraba 63,424. Ni jengo la sita kwa ukubwa duniani na la kwanza barani Afrika,
ni jengo la heshima na tayari sasa tumeshaanza utalii wa majengo ya kimahakama,’
amesema.
Miradi mingine ni ujenzi wa nyumba ya Jaji
Mkuu-Dodoma, ujenzi wa Vituo Jumuishi Tisa vya Utoaji Haki (IJCs) katika maeneo
mbalimbali, ikiwemo Visiwani Pemba, ujenzi wa Mahakama 15 za Wilaya na ujenzi
wa Mahakama za Mwanzo katika Wilaya mbalimbali nchini.
‘Tunaishukuru sana Serikali ya Awamu
ya Sita kwa jinsi ambavyo imekuwa ikijitoa na kuhakikisha kwamba rasilimali
fedha inapatikana. Miundombinu hii ya majengo haiwezi kufanikiwa bila fedha.
Serikali ndiyo inayowezesha haya yote kuweza kufanyika,’ amesema.
Mtendaji Mkuu pia ameishukuru Benki ya
Dunia kwa kushirikiana na Serikali kutoa mkopo wa gharama nafuu ili kufanikisha
baadhi ya ujenzi wa miundombinu. Amebainisha kuwa awamu ya kwanza walipata Dola
za Kimarekani million 65 na awamu ya pili Dola za Kimarekani milioni 90.
Kwa mujibu wa Prof. Ole Gabriel,
katika awamu ya kwanza walifanikiwa kujenga Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki sita
katika Mikoa ya Dar es Salaam (Temeke na Kinondoni), Morogoro, Dodoma, Mwanza
na Arusha ambavyo vilizinduliwa kwa pamoja na Mhe. Dkt. Samia terehe 6 Octoba,
2021 jijini Dodoma.
Aliwaeleza Waandishi wa Habari kuwa
baada ya kukamilika kwa miradi hiyo, Mahakama ya Tanzania ilifanya upimaji wa
kile kilichofanyika na kufanikiwa kuokoa kiasi cha Shilingi za Kitanzania
bilioni 3.6 ambazo zilitumika kufanya kazi zingine.
Mtendaji Mkuu ametaja miradi ya ukarabati
inayoendelea na utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2024/25 ni jengo la Mahakama Kuu
– Musoma, jengo la Mahakama Kuu – Dodoma, jengo la Mahakama Kuu Iringa, nyumba
ya Jaji Kiongozi – Dodoma na nyumba ya Jaji Iringa.
Prof. Ole Gabriel ametaja miradi
iliyopo katika hatua za usanifu kama nyumba za Majaji Mikoa ya Geita, Tabora na
Sumbawanga, majengo ya Mahakama za Wilaya Handeni, Kiteto, Igunga, Mlele,
Lushoto na Rufiji na jengo la Mahakama ya Mwanzo Mkomazi.
Ametaja pia ukarabati wa nyumba za Majaji
Mkoa wa Mbeya, majengo ya Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi-Dar
es Salaam, Mahakama Kuu Mbeya na Mwanza na jengo la Mahakama Kuu Divisheni ya
Kazi – Dar es Salaam.
‘Kukamilika kwa miradi hii ya ujenzi
wa Mahakama kwa ngazi mbalimbali kutarahisisha uendeshaji na upatikanaji wa
huduma za kimahakama katika miundombinu bora na ya kisasa kwa Wananchi, ambao
hapo awali walilazimika kutembea umbali mrefu na kutumia gharama kubwa kufikia
huduma za Mahakama,’amesema.
Mtendaji Mkuu amebainisha kuwa juhudi
za kusogeza huduma hizo za Mahakama kwa Wananchi ni katika kutekeleza Dira ya
Mahakama, yaani ‘Upatinakanaji wa Haki kwa Wakati na kwa Wote.’
Kabla ya kuzungumza na Waandishi wa Habari, Prof. Ole Gabriel alimtembelea Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita, Mhe. Kevin Mhina na kufanya naye mazungumzo mafupi. Kadhalika, Mtendaji Mkuu alisalimiana na Watumishi wanaohudumu katika Mahakama hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni