Jumatatu, 12 Mei 2025

MAHAKIMU SAME WAKUTANA KUJINOA MABADILIKO MBALIMBALI YA SHERIA

Na JAMES KAPELE,  Mahakama-Moshi

Mahakimu Wakazi wote wa Mahakama ya Wilaya ya Same wamekutana katika Mahakama ya Wilaya ya Same kwa lengo la kupitia pamoja mabadiliko ya sheria mbalimbali ambazo zimefanyiwa marekebisho hivi karibuni ili kupata uelewa wa pamoja na kubadilishana uzoefu katika changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika kazi zao za kila siku za uendeshaji wa mashauri. 

Kikao hicho kilifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita tarehe 09 Mei, 2025 kikiwa kimeitishiwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Same, Mhe. Chrisanta Chitanda.

Awali akifungua kikao hicho ofisini kwake , Mhe. Chitanda aliwasihi  Mahakimu waliohudhuria kikao hicho kujenga utamaduni wa kuwa tayari wakati wote kuendana na mabadiliko ya kisheria pindi yanapotokea ili wafanye kazi yao ya kuzitafsiri sheria hizo kwa weledi wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku.

“Kazi zetu ni za kusoma kila siku na kuhakikisha tunaendana na mabadiliko ya sheria kila wakati yanapotokea. Hii itatufanya tuifanye kazi yetu kwa weledi na kwa kujiamini zaidi, jengeni pia utamaduni wa kubadilishana uzoefu kila wakati hasa mnapokutana na changamoto miongoni mwenu. Hatua hii itawapa wepesi wa kutimiza majukumu yenu ya kila siku,” alisisitiza Mhe.Chitanda.

Pamoja na mambo mengine, kikao hicho kilipitia na kujadili mabadiliko ya Sheria mbalimbali ambazo ni Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura Na. 329, Sheria ya Mtoto Sura Na. 13 na nyingine zinazohusiana na uendeshaji wa mashauri.

 Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Same, Mhe. Chrisanta Chitanda akisisitiza jambo wakati wa majadiliano ya kujadili mabadiliko ya sheria mbalimbali ambazo zimefanyiwa marekebisho hivi karibuni.

Katika picha ni sehemu ya Mahakimu Wakazi wa Mahakama Wilaya ya Same wakiendelea na majadiliano katika kikao hicho kilichofanyika tarehe 09 Mei, 2025.

 Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Gonja, Mhe.Nassoro Nkumulwa (aliyesimama)  akichangia hoja wakati wa majadiliano hayo.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni