Jumatatu, 12 Mei 2025

WATUMISHI KIGOMA WASISITIZWA KUDUMISHA UTAMADUNI WA KUFANYA MAZOEZI

Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma

Jaji Mafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile kwa nyakati tofauti ameendelea kusitiza utamaduni wa watumishi kufanya mazoezi kwani yanasaidia kuimarisha afya za watumishi kuwa bora zaidi wakati wote na kuepuka magonjwa yasiyoambukizwa.

Rai hiyo ilitolewa hivi karibuni katika kikao kilichofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita,  na iliungwa mkono na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Projestus Kahyoza ambaye alipendekeza utamaduni wa mazoezi  uzifikie Mahakama mbalimbali za Wilaya na Mwanzo zilizopo katika Kanda hiyo.  

Mhe. Rwizile ambaye ni muasisi wa mazoezi katika Kanda ya Kigoma, aliongeza kuwa  mazoezi hayo ambayo hufanyika siku Jumatano na Ijumaa licha ya kuimarisha afya za watumishi mazoezi hayo pia ni sehemu ya kuwaweka pamoja watumishi na kuongeza ushirikiano katika majukumu mbalimbali ya kuwahudumia wateja wa Mahakama.

“Niwaombe hata wale wasioweza kufika eneo la mazoezi kwa muda uliopangwa katika makao makuu yetu ya Kanda mjitahidi kutenga muda wenu mdogo majumbani kwenu kwa ajili ya mazoezi ya kuimarisha miili yenu,” alisisitiza Jaji Rwizile.

Kwa upande wake, Mlezi wa mazoezi wa Kanda hiyo, Mhe. Projestus Kahyoza alisema kuwa, mazoezi ni muhimu sana kama ilivyo chakula cha kila siku kwa mwanadamu, hivyo aliwataka watumishi kuona umuhimu wake ili kuiweka miili yao katika hali ya kukabiliana na changamoto za kiafya zinazoweza kujitokeza katika miaka ya uzee. 

Mhe. Kahyoza aliongeza kwa kubainisha kuwa, mazoezi ni tiba kubwa ya magonjwa mbalimbali na kuondoa magonjwa nyemelezi katika mwili wa binadamu.

Pamoja na mazoezi, Mhe. Kahyoza alisisitiza pia juu ya umuhimu kwa watumishi kuzingatia ulaji unaozingatia taratibu za kiafya ili kulinda afya za miili yao kwa ujumla. 

Jaji Mafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Karichuba Rwizile akifanya mazoezi hivi karibuni  katika eneo la juu la jengo la Mahakama hiyo.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa (wa kwanza kulia mstari wa nyuma) akishiriki mazoezi pamoja na watumishi wengine wa Kanda hiyo.

 Watumishi wa Mahakama Kuu Kigoma wakifanya mazoezi kuimarisha afya zao ili kuwa imara wakati wote wa kutoa huduma kwa wananchi.

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Mhe. Aristida Tarimo akijumuika na watumishi wa Mahakama Kuu Kigoma kufanya mazoezi eneo la juu la jengo la Mahakama hiyo.

Jaji Mafawidhi wa Mahakama Kuu Kigoma Mhe. Augustine Karichuba Rwizile (wa kwanza kushoto mstari wa kwanza) akiwaongoza sehemu ya watumishi wengine wa Kanda hiyo kufanya mazoezi katika eneo la juu la jengo la Mahakama hiyo. 

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni