Jumatatu, 12 Mei 2025

WANAFUNZI SHULE YA SEKONDARI MLOLE WATEMBELEA MAHAKAMA KUU KIGOMA

  • Wapata fursa ya kujifunza masuala mbalimbali ya kimahakama ikiwemo taratibu za usikilizwaji mashauri

Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma imeendelea kuwa karibu na umma katika utoaji elimu ambapo hivi karibuni wanafunzi 23 wa kidato cha nne kutoka Shule ya Sekondari Mlole walipata fursa ya kujifunza mambo mbalimbali ya kimahakama ikiwemo changamoto zinazoikabili Mahakama katika usikilizwaji wa mashauri na utoaji hukumu.

Msaidizi wa Sheria wa Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Valerian Msola aliwaeleza wanafunzi hao juu ya jukumu kuu la Mhimili wa Mahakama ambapo alisema, “Mahakama ina kazi ya kuzikiliza kesi, na kutoa maamuzi juu ya masuala mbalimbali ya kisheria yanayofikishwa mbele yake.”

Pamoja na hayo, Mhe. Msola aliwaeleza wanafunzi hao kuwa, changamoto zinazoikabili Mahakama ni pamoja na uelewa mdogo wa sheria kwa wadau wa Mahakama, ushahidi hafifu unaoletwa mahakamani, ukosefu wa uwakilishi wa kisheria kwa wananchi wengi kutokana na kushindwa kumudu gharama za Mawakili wa Kujitegemea.

Aidha, aliwadokeza wanafunzi hao kwamba wao ni taifa la kesho hivyo wamefanya vema kufika mahakamani kufahamu sheria na taratibu mbalimbali ili wakawe wajumbe wazuri katika jamii ya wanafunzi na kupata utambuzi wa masuala mengi waliyojifunza.

Akijibu swali la mwanafunzi, Bw. Boid Noah aliyeuliza kuhusu wajibu wa Mahakama kwa wadaawa, Mhe. Msola alisema kuwa, Mahakama pamoja kazi kubwa ya kusikiliza mashauri na kutoa uamuzi inao pia wajibu wa kuwaongoza wadaawa katika usikilizwaji wa mashauri yao kwa mjibu wa sheria za uendeshaji wa mashauri husika ili kila upande upate haki ya kusikilizwa na baadaye maamuzi yanayozingatia misingi ya sheria kutolewa.

Kwa upande wake, Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo, Mhe. Victor Kagina aliwaasa wanafunzi hao kuendelea kusoma kwa bidii ili baadae baadhi yao au wote wawe wanasheria watakaozisaidia jamii zao katika masuala mbalimbali ya kisheria.

Pamoja na nasaha hizo kwa wanafunzi hao, Mhe. Kagina aliwashauri wawe mifano mizuri kwa jamii zao kwa kuishi kwa kufuata taratibu na sheria pamoja na kuwa na maadili kwa watu wanaowazunguka hususani walimu wao, wanafunzi wenzao, wazazi na walezi wao ili pia waje kuwa wazazi na viongozi wazuri hapo mbeleni. 

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mlole iliyopo mkoani Kigoma wakimsikiliza kwa makini Msaidizi wa Sheria wa Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Valerian Msola (hayupo katika picha) alipokuwa akiwafundisha wanafunzi hao waliotembelea Mahakakama hiyo hivi karibuni. 

Msaidizi wa Sheria Jaji wa Mahakama Kuu Kigoma Mhe. Valerian Msola akisisitiza  jambo kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mlole waliofika Mahakama Kuu Kigoma kwa lengo la kujifunza juu ya shughuli za Mahakama na changamoto zake. 

Msaidizi wa Sheria wa Jaji wa Mahakama Kuu Kigoma, Mhe. Valerian Msola akifafanua jambo wakati wa kutoa elimu kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mlole iliyopo Wilaya ya Kigoma Mjini waliofika Mahakama kuu kujifunza juu ya shughuli za Mahakama na changamoto zake. 

Picha ya pamoja ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mlole mara baada ya kumaliza kupata elimu juu ya shughuli za Mahakama.

 Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Victor Kagina (katikati), Msaidizi wa Sheria Jaji wa Mahakama Kuu Kigoma, Mhe. Valerian Msola (kushoto), na  Msaidizi wa Kumbukumbu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Bi. Christina Mpungu (kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na   wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mlole (waliosimama).

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni