Jumatatu, 12 Mei 2025

JMAT MANYARA WAKUMBUSHANA JUU YA KANUNI ZA UANDISHI BORA WA HUKUMU

Na Christopher Msagati- Mahakama, Manyara

Wajumbe wa Chama cha Majaji na Mahakimu Nchini (JMAT) tawi la Manyara wamekumbushana juu ya taratibu na kanuni za uandishi bora wa Hukumu.

Akifungua mkutano huo, Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara Mhe. Devotha Kamuzora ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama hicho kwa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara katika mafunzo yaliyoambatana na Mkutano wa Chama hicho uliofanyika tarehe 9 Mai, 2025 katika Ukumbi wa Wazi wa Mahakama ya Wilaya ya Babati.

Mhe. Kamuzora aliwasisitiza Majaji na Mahakimu kuzingatia miongozo mbalimbali inayotolewa katika kufanikisha kazi zao za kila siku kuanzia usikilizaji wa mashauri mpaka utoaji wa maamuzi.

“Hii miongozo na kanuni zinazotolewa, zimeandaliwa ili zituwezeshe kuzingatia taratibu zinazostahili ili kuwa na hukumu bora ambazo zitaleta tija kwa wadaawa wetu. Hivyo ni muhimu kuzingatia na kufuata kanuni hizi,” alisema Mhe. Kamuzora.

Naye, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara Mhe. John Kahyoza wakati wa kutoa Mada aliwaeleza wajumbe kuwa miongozo ya uandishi bora wa Hukumu husaidia katika kuleta uwazi ambao huonekana kwa wadaawa na uwazi huo husaidia kupunguza malalamiko au kutokuridhika katika maamuzi yanayotolewa.

“Kanuni hizi zikifuatwa vizuri, zitawasaidia nyinyi waheshimiwa Majaji na Mahakimu kuwa na uwazi miongoni mwa wadaawa wenu. Vile vile matumizi ya kanuni hizi huongeza usawa na kuwa na mfanano wa utaratibu katika uandishi wa hukumu zetu,” alisema Mhe. Kahyoza.

Akichangia mada katika mafunzo na Mkutano huo, Hakimu Mkazi Mahakama ya Mwanzo Haydom Mhe. Zena Mgalula aliushukuru uongozi wa JMAT Tawi la Manyara kwa kuandaa Mkutano na Mafunzo hayo ambayo yatawapa weledi zaidi katika kuandika hukumu zenye kuzingatia kanuni na miongozo.

“kwa kweli tunashukuru uongozi wa JMAT kwa kuamua kuleta mafunzo haya Katikati ya mkutano huu kwani yatatufaa sana katika uboreshaji wa uandishi wa hukumu zetu,” alisema Mhe. Mgalula.

Katika upande mwingine wajumbe wa JMAT Tawi la Manyara walitumia mkutano huo kujadili masuala yao ambayo yatawasaidia katika kazi zao za kila siku lakini pia masuala mbalimbali ambayo yanapaswa kufanywa na JMAT katika jamii inayowazunguka.

Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara Mhe. Devotha Kamuzora ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha JMAT Mahakama Kuu Kanda ya Manyara akifungua mkutano huo ulioambatana na mafunzo kwa Maafisa Mahakama hao wa Kanda hiyo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara Mhe. John Kahyoza (katikati) akiwa pamoja na Majaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara katika mkutano huo

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara Mhe. John Kahyoza (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja Maafisa Mahakama walioshiriki mafunzo ya JMAT mkoani Manyara


Sehemu ya Maafisa Mahakama walioshiriki mafunzo ya JMAT mkoani Manyara wakifuatilia mawasilisho ya mafunzo hayo.







Hakuna maoni:

Chapisha Maoni