Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ameungana na Viongozi wa kitaifa na Watanzania kwa
ujumla kumuaga aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu Mastaafu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Marehemu Cleopa David Msuya.
Jaji Mkuu aliungana na
Viongozi wengine, akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan kwenye maombolezo hayo yaliyofanyika kitaifa kwenye Viwanja vya
Karimjee jijini Dar-es-Salaam.
Miongoni mwa Viongozi
wengine wa kitaifa waliomuaga Marehemu Msuya ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Phillip Isdor Mpango, Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi na Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.
Jaji Mkuu wa Tanzania anatarajia
kuungana na Viongozi mbalimbali wa kitaifa kwenye maziko ya Marehemu Msuya
yatakayofanyika kesho tarehe 13 Mei, 2025 Usangi, Wilaya ya Mwanga, Mkoa wa
Kilimanjaro.
Mhe. Msuya alifariki tarehe
7 Mei, 2025 katika Hospitali ya Mzena Jijini Dar es Salaam alipokuwa amelazwa
akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa moyo.
Kufuatia kifo hicho, Rais
Samia alitangaza siku saba za maombolezo hadi tarehe 13 Mei, 2025 na kuwapa
pole ndugu, jamaa na Watanzania wote kwa msiba huo mzito kwa Taifa.
Msuya aliwahi kushika
wadhifa wa Waziri Mkuu mara mbili. Mara ya kwanza ni kuanzia tarehe 7 Novemba,
1980 hadi tarehe 24 Februari, 1983. Mara ya pili ilikuwa ni tarehe 5 Desemba,
1994 hadi tarehe 28 Novemba, 1995, huku akishika pia wadhifa wa Makamu wa
Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Baada ya kustaafu siasa
aliendelea kushika nyadhifa kadhaa za uongozi katika Taasisi mbalimbali za
Jamii.
Mhe. Cleopa David Msuya
alizaliwa tarehe 4 Januari 1931 katika kijiji cha Chomvu, Usangi, wilayani
Mwanga, mkoani Kilimanjaro. Alisoma katika Chuo Kikuu cha Makerere kuanzia
mwaka 1952 hadi 1955. Baada ya hapo, alijihusisha na kazi za maendeleo ya jamii
na huduma kwa Wananchi vijijini kuanzia mwaka 1956 hadi 1964.
Kuanzia mwaka 1964, Msuya
alihudumu kama Katibu Mkuu katika Wizara mbalimbali: Wizara ya Maendeleo ya
Jamii na Utamaduni (1964–1965), Wizara ya Ardhi, Makazi na Maendeleo ya Maji
(1965–1967), Wizara ya Mambo ya Uchumi na Mipango (1967–1970) na Wizara ya
Fedha (1970–1972).
Mnamo tarehe 18 Februari
1972, Mhe. Msuya aliteuliwa kuwa Waziri wa Fedha na alihudumu hadi
alipohamishiwa kuwa Waziri wa Viwanda mnamo tarehe 3 Novemba 1975.
Baada ya kuhudumu kwa
miaka mitano kama Waziri wa Viwanda, aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu mnamo Novemba
1980, nafasi aliyoshikilia hadi Februari 1983. Baadaye, alirudi tena kuwa
Waziri wa Fedha kutoka Februari 1983 hadi Novemba 1985.
Tarehe 6 Novemba 1985, Mhe.
Msuya alipewa jukumu jipya akiwa Waziri wa Fedha, Mambo ya Uchumi na Mipango
hadi Machi 1989, kisha alirudi kuwa Waziri wa Fedha tena kuanzia Machi 1989
hadi Desemba 1990, na baadaye kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara kutoka Machi
1990 hadi Desemba 1994.
Mwaka 1994, aliteuliwa
tena kuwa Waziri Mkuu kwa mara ya pili, na pia kuhudumu kama Makamu wa Kwanza
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hadi Novemba 1995.
Katika uchaguzi wa Bunge
wa mwaka 1995, Mhe. Msuya alichaguliwa tena kuwa Mbunge na alihudumu hadi alipostaafu
rasmi tarehe 29 Oktoba 2000.
Baada ya kustaafu, Msuya
aliendelea kuwa mwanachama hai wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na kufikia mwaka
2006 alikuwa bado ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM.
Pia alikuwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Maendeleo la Kilimanjaro.
Mnamo Oktoba 23, 2019, akiwa na umri wa miaka 88, Mhe. Msuya aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Awamu ya Tano, Hayati John Pombe Magufuli kuwa Mkuu wa Chuo cha Ardhi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni