Na AMANI MTINANGI, Mahakama-Tabora
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora imeanza kusikiliza shauri la kikatiba lililofunguliwa na Bw. Alex Barunguza kupinga kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani kabla ya kufanyika kwa marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Shauri hilo limeanza kusikilizwa jana tarehe 08 Mei, 2025 na jopo la Majaji watatu likiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Juma Mambi na Majaji wengine katika jopo hilo ambao ni Mhe. Dkt. Zainabu Diwa Mango na Mhe. Dkt. Frank Mirindo.
Katika hatua ya awali, Mahakama imeanza kusikiliza mapingamizi yaliyowasilishwa kabla ya kuingia kwenye hoja za msingi za shauri hilo. Miongoni mwa hoja hizo ni ombi la shauri hilo kurushwa moja kwa moja na vyombo vya habari kwa lengo la kutoa fursa kwa umma kupata taarifa kwa wakati na kulinda dhana ya haki ya wazi (open justice).
Mapingamizi mengine yaliyoibuliwa ni pamoja na hoja ya kwamba Mahakama haina mamlaka ya kisheria ya kusikiliza shauri hilo, suala ambalo limeibua mjadala wa kisheria kati ya pande zinazohusika ambapo katika maamuzi madogo yamebainisha imeamuliwa kuwa Mahakama Kuu ndio iliyofanya maamuzi hivyo haiwezi kujiongoza vingine katika maamuzi iyoyafanya.
Upande wa wajibu maombi umeongozwa na Wanasheria wa Serikali pamoja na Mawakili wa Serikali wakiwemo Bw. Mark Mulwambo, Bi. Jackline Kinyasi na Bw. Samwel Mahuma.
Mahakama imepanga kuendelea na usikilizwaji wa shauri hilo tarehe 19 Mei, 2025 ambapo itaendelea kusikiliza hoja za mapingamizi kabla ya kuingia katika kusikiliza hoja za msingi zilizowasilishwa na mlalamikaji, Bw. Barunguza.
Mawakili wa Serikali waliowawakilisha wajibu maombi wakijadiliana jambo. Wa pili kulia ni Bw. Alex Barunguza Mtoa hoja ya kupinga kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba, 2025.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni