- Aeleza
mafanikio ya ushirikiano kwa kipindi cha miaka sita
Na INNOCENT KANSHA na MAGRETH
KINABO - Mahakama
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya
jana tarehe 8 Mei, 2025 ameungana na Nchi wanachama na Mabalozi takribani 193 kushiriki
mkutano wa Kamati ya Maendeleo ‘Miliki
Binifu’ ya Shirika la Miliki Bunifu Duniani (WIPO) alioshiriki kwa njia ya
mkutano mtandao akiwa Ofisini kwake Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.
Akiuelezea ujumbe huo wa nchi wanachama wa shirika hilo wa
Mabara yote Mhe. Nkya amesema Mahakama ya Tanzania imenufaika kwa kiwango
kikubwa kutokana na kuwa sehemu ya shirika hilo la Miliki Bunifu Duniani (WIPO)
amebainisha kwamba, kupitia mashirikiano hayo,imewezesha kuwaongezea uelewa
mkubwa wa masuala ya Miliki Bunifu kwa Maafisa Mahakama na kuongeza njia za
kutatua migogoro inayotokana na kazi za miliki bunifu.
Aidha, Mhe. Nkya ametaja mafanikio mengine ni kutoa
mafunzo kwa Maafisa Mahakama watapatao takribani 1,200 yaliyotokana programu ya
Shirika hilo ya kubadilishana uzoefu.
“Takribani Maafisa Mahakama 404 walifanikiwa kushiriki
mafunzo kwa njia ya masafa na kufuzu mafunzo ya sheria za haki bunifu na zaidi
ya Maafisa 300 walishiriki makongomano ya Miliki Bunifu kupitia Shirika hilo na kuwajenga uelewa mpana
wa namna ya kuzitekeleza sheria zinazohusu
masuala ya Miliki Bunifu,” amesisitiza Msajili Mkuu.
Mafanikio mengine Mahakama ya Tanzania, iliyoyapata ni
kwamba Majaji na Mahakimu 80 wakiwemo Majaji wa Mahakama ya Rufani,
walipata walishiriki warsha za miliki bunifu kwa nyakati tofauti, ambapo Majaji
hao hutoa maamuzi katika Mahakama ya ngazi ya mwisho ya utoaji wa haki nchini
Tanzania.
Aidha, Mhe. Nkya amesema, kupitia ushiriki wa Tanzania
Mahakama imeendelea kuwa mchangiaji mkubwa duniani katika utoaji wa maamuzi
kuhusu miliki bunifu. Kuanzia mwaka 2019 jumla ya Majaji wapato 76 wamekuwa
wakishiriki kwenye mkutano wa mwaka wa jukwaa la Majaji wa Shirika la Miliki
Bunifu Duniani (WIPO) ili kujiongezea uelewa na uzoefu kutoka kwa mamlaka
zingine zinazotatua migogoro ya miliki bunifu.
Mbali na mafunzo ya mara kwa mara ya miliki bunifu, Mhe. Nkya amesema, ushirikiano umeisaidia Mahakama ya Tanzania kuandaa miongozo ya kufundishia, mfano Mahakama imeandaa machapisho maalum ya kuendeshea mafunzo, kuandaa mkusanyiko wa vitabu vya maamuzi ya mashauri yahusuyo miliki bunifu, Vitabu Miongozo ambavyo vipo kwenye hatua ya mwisho ya maandalizi.
“Nyaraka hizo muhimu zitasaidia kutoa mwongozo na hadidu
rejea kwa Maafisa Mahakama na zitachangia kukuza maendeleo ya taaluma na pia
kusaidia ulinganifu wa tafsiri na kupunguza maamuzi yasiyoendani na kusaidia
kujiamini kwa watoa maamuzi yanayohusu miliki bunifu,” ameongeza Msajili Mkuu.
Vilevile, Mahakama ya Tanzania mnamo mwaka 2022 ilisaini
makubaliano na Shirika la Miliki Bunifu Duniani (WIPO) ya kutoa na kusambaza
maamuzi yatokanayo na mashauri ya miliki bunifu ili kuyachapisha kwenye kanzi
data ya Shiriki ijulikanayo kama (WIPO Lex). Mpaka sasa ni maamuzi 41 ya
mashauri ya miliki bunifu yamekwisha chapishwa ama kupandishwa kwenye mtandao
huo wa Shirika na maamuzi mengine 39 yanafanyiwa mapitio kabla ya kuzichapisha.
Mhe. Nkya amesema, eneo lingine la ushirikianao ni kukuza
matumizi na taratibu za usuluhishi, kupitia utaratibu huo wa WIPO na Mahakama
imewezesha Majaji na Mahakimu wapatao 245 wameshafuzu mafunzo ya usuluhishi na
upatanishi kwa njia masafa na Maafisa Mahakama wengine 159 wanendelea kusoma kozi maalum ya usuluhishi
“Mafanikio hayo ya usuluhishi na upatanishi yamewezesha
Mahakama kusuluhisha mashauri 26 ya miliki
bunifu kwa. Aidha Majaji wa Kitanzania wanane,”
wameteuliwa kuwa wasuluhishi wa WIPO ameongeza Msajili Mkuu.
Aidha, Mhe Nkya amesema kupitia program hizo mbalimbali
za kuwajengea uwezo za shirika la WIPO zimewasidia Majaji na Mahakimu kuongeza
uwezo na ujuzi wa kutosha wa kutoa haki kwa weledi na ufanisi katika eneo la
mashauri ya miliki bunifu.
“Majaji na Mahakimu nchi nzima kwa sasa wanasikiliza
mashauri ya miliki bunifu kwa uelewa, utaalum mkubwa na kwa kujiamini, hivyo
kuchangia ufanisi na mashauri kuamriwa kwa wakati na kuondoa migongano katika
kushughulikia migogoro ya miliki bunifu,” ameongeza Msajili Mkuu.
Vilevile, Mhe. Nkya amesema, ushirikiano huo umechangia
kukuza ajenda ya maendeleo ya Taifa, kwani Mahakama yenye uwezo wa kutatua
migogoro ya miliki bunifu kwa uthabiti na kwa kuzingatia sheria kunakuza ustawi
na kuongeza imani kwa wananchi dhidi ya mfumo wa utoaji haki.
“Kwa kufanya hivyo inachangia uvumbuzi, kulinda ubunifu
na kuhimiza uwekezaji wa ndani na wa nje ya nchi. Kuna nyakati miliki bunifu
ilionekana kama masuala ya kiufundi na kutoyatilia mkazo, lakini kwa sasa
yanatambulika kama nguzo ya kimkakati katika mageuzi ya kiuchumi nchini
Tanzania,” amesema Mhe. Nkya.
Kwa
upande mwingine, kuhusu majadiliano ya nchi wanachama ilielezwa kuwa
kikao hicho kina malengo mbalimbali, ikiwemo kujadiliana masuala ya maendeleo ya
Nchi Wanachama, kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya Miliki Bunifu (IP),
kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya nchi uanachama, kuangalia maamuzi yanayotolewa kuhusu suala hilo na kuendeleza
program ya utoaji elimu kwa ajili ya kujengeana uwezo wa kwenye
elimu na ujuzi juu Milki Bunifu
Katika mkutano huo, wa siku tano mambo mengine
yaliyojadiliwa ni kuendana sambamba na mabadiliko ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (TEHAMA) katika kushughulikia mashauri yanayuhusu Miliki Bunifu kupitia
uzoefu wa nchi mfano; China, Ujerumani,
India na nyinginezo. Pia kuangalia maamuzi ya Mahakama ya Juu nchini China
(Supreme Court) na uzoefu wa Mahakama ya Juu ya Latvia.
Halikadhalika kutoa masaada kwa Majaji wanaoshughulikia
mashauri ya IP, kutoa mwuongozo kwa Mabaraza ya Usuluhishi wa Migogoro ya
Viwanda, Majaji wapya waeleweshe juu ya
masuala ya Milki Bunifu kutoka kwa wazoefu wa jambo hilo, kuangalia
mikataba inayohusu Milki Bunifu ikiwemo
utoaji wa mafunzo kwa njia ya masafa.
Mambo mengine yaliyojadiliwa ni kuangalia masuala ya Haki Miliki ya
Bunifu ya mtu, (Copy Rights), mizozo ya
utumiaji wa chapa za miliki ya mtu
mwingine, mashauri yanayohusu mali za viwanda, utangazaji haramu wa matangazo
ya kibiashara, program (software), alama
ya biashara na filamu(video), ikiwa ni hatua ya kuhakikisha utoaji wa haki za Milki
Bunifu unafanyika kwa viwango vinavyotakiwa.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya(kushoto) jana tarehe 8 Mei, 2025 ameungana na Nchi wanachama na Mabalozi takribani 193 kushiriki mkutano wa Kamati ya Maendeleo ‘Miliki Binifu’ ya Shirika la Miliki Bunifu Duniani (WIPO) uliofanyika kwa njia ya mkutano mtandao akiwa Ofisini kwake Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.Kulia ni Mratibu wa Shughuli za WIPO Mahakama ya Tanzania.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni