- Awataka kubaini maeneo yenye jiografia ngumu
- JMAT watumie fursa uwekezaji kwenye teknolojia
- Awataka kujiandaa na uchaguzi mkuu
Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma
Viongozi wapya wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania-JMAT jana tarehe 7 Mei, 2025 walimtembelea Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na kufanya mazungumzo naye kwenye mambo mbalimbali yanayolenga kuimarisha utendaji kazi katika muktadha mzima wa utoaji haki kwa Wananchi.
Wakiongozwa na Rais wa JMAT, ambaye pia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Elimo Massawe, Viongozi hao walifika katika ofisini ya Jaji Mkuu iliyopo kwenye Jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma majira ya saa 3.00 asubuhi.
Viongozi wengine walioambatana na Mhe. Massawe, ni Katibu wa JMAT, Mhe. James Mniko, Katibu Msaidizi, Mhe. Teddy Mlimba, Mtunza Hazina, Mhe. Devotha Kasebele na Katibu Mwenezi wa Chama hicho, Mhe. Fratern Temba.
Akijibu baadhi ya maombi yaliyowasilishwa kwake na Viongozi hao, Jaji Mkuu aliahidi kufanyia kazi changamoto zinazowakabili Wanachama wa JMAT, ikiwemo kuziainisha vizuri na kuziwasilisha kwa wenzake ndani ya Mahakama ya Tanzania ili kuona njia bora ya kuzitatua kwa pamoja.
Aliwaelekeza Viongozi hao kubaini maeneo yenye jiografia ngumu ambayo Wanachama wa JMAT wanahudumu katika maeneo mbalimbali nchini na kuzungumza na uongozi namna ya kukabiliana na changamoto hiyo.
‘Hili eneo la mazingira magumu ya kazi lina changamoto, tuanze kubaini maeneo gani ambayo yenye jeografia ngumu. Vile vile tusome ile ripoti ya Repoa, nadhani wamejalibu kuelezea mazingira ambayo Watumishi wanakabiliana nayo,’ alisema.
Mhe. Prof. Juma aliitaka JMAT kutumia fursa ya teknolojia na jukwa la masomo ya masafa-e-learning platform ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto-IJA na kuomba kusanifu masomo mengine ambayo wanaweza kupata shahada kupitia njia hiyo, hasa kwenye maeneo mapya.
‘Tusisome sana maeneo ambayo hayaingiliani na teknolojia kwa sababu huko ndiko Dunia inakokwenda. Hili ni eneo ambalo lina potential kubwa sana,’ Jaji Mkuu alisema.
Mhe. Prof. Juma pia aliwataka Wanachama wa JMAT kushiriki kikamilifu katika Mpango Mkakati wa Tatu wa Miaka Mitano wa Mahakama ya Tanzania na kutoa mchango wao kwa kuzingatia kuwa wapo katika kila sehemu kama kupanga bajeti na uongozi.
‘Sijui mtafanyaje ili wanapopanga watilie maanani masuala ya JMAT. Mfano, sasa hivi tunazungumzia Mpango Mkakati wa Tatu wa Miaka Mitano wa Maboresho ya Mahakama. Nyinyi mnamchango wa aina gani katika mpango huo…
‘Mipango ndiyo inayozaa bajeti, mkisubiri mpango uliotayarishwa bila kuweka maslahi ya JMAT mtakuwa nje ya bajeti wakati wa utekelezaji. Sasa hivi nadhani wapo Arusha, bila shaka mna taarifa, masuala yenu yataingizwaje. Unaweza kukuta mambo mengi ambayo mmeyaibua yanaweza kuwa ni sehemu ya mpango,’ alisema.
Jaji Mkuu aliwahimiza pia kutengeneza hoja bila kutumia nguvu na mvutano zitakazosaidia uongozi kuzungumza na Mihimili mingine ili kutafuta namna ya kutatua changamoto zinazowakabili.
Kadhalika, Mhe. Prof. Juma aliitaka JMAT kujiandaa na Uchaguzi Mkuu kwa kuanza mafunzo kwa Mahakimu namna ya kushughulikia migogoro ya uchaguzi itakayoletwa mahakamani.
‘Jengeni hoja kwa Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania ili awatengee maeneo ya kufanya mafunzo. Mkifanya hivyo nyinyi wenyewe kama maofisa wa Mahakama inakuwa na manufaa na uhuru zaidi,’ alisema.
Awali, akizungumza kwa niaba ya Viongozi wenzake, Rais wa JMAT alimpongeza Jaji Mkuu kwa kazi nzuri anazozifanya za kuwahudumia Watanzania na kwa ushirikiano ambao anawapa wakati wa kutekeleza majukumu yao.
Mhe. Massawe alimwomba Jaji Mkuu kuwasaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili Wanachama wa JMAT katika maeneo mbalimbali nchini.
Rais wa JMAT pia alimuomba Jaji Mkuu kuwa ili kuwezesha ufanisi, sheria zilizofanyiwa mapitio mwaka 2023 zipatikane kwenye maktaba ya Mahakama Mtandao ili Majaji na Mahakimu wapate urahisi wa rejea.
Kadhalika, aliomba maboresho ya bima ya afya ili waweze kupata huduma kwa upana zaidi kuliko ilivyo hivi sasa.
Ombi jingine lilihusu JMAT kuendelea kupewa fursa ya kuratibu mafunzo kwa Wanachama wake, kwani ni jukwaa zuri zaidi kwa Majaji na Mahakimu kuzungumza kitaaluma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni