Jumanne, 6 Mei 2025

MAHAKIMU WAFAWIDHI KIGOMA WAKUMBUSHWA KUONGEZA USIMAMIZI WA MASHAURI YA WATOTO KUEPUKA VIFUNGO

Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma

Naibu Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa ametoa rai kwa Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Kanda hiyo kusimamia mashauri yanayohusu watoto wadogo adhabu mbadala zitumike kuepusha vifungo kwao kwakuwa ni kinyume na sheria.

Mhe. Mbelwa aliyasema hayo hivi karibuni wakati akizungumza na Wafawidhi hao katika kikao kilichofanyika kwa njia ya Mtandao wakati akitoa mrejesho wa Ukaguzi wa robo ya kwanza ya mwaka 2025.

Aidha, Naibu Msajili huyo aliwakumbusha wafawidhi hao kutumia fursa ya ukaguzi kuhakikisha, Mahabusu wa Mahakama za Mwanzo hawapo gerezani kwa kuwa hakuna kosa lisilodhaminika katika Mahakama hizo.

Katika kikao hicho, Mhe. Mbelwa aliwakumbusha pia Mahakimu hao kuhusu matumizi ya adhabu yanayoendana na mamlaka za Mahakama zao, huku akiwataka Wafawidhi hao kuwasaidia kwa karibu Mahakimu wapya wa Mahakama za Mwanzo katika miongozo bora ya uandishi wa hukumu na usimamizi wa Mahakama zao. 

Kadhalika Naibu Msajili huyo, alitoa rai kwa Mahakimu Wafawidhi hao kukaa na Mahakimu walio chini yao  kuwakumbusha mara  kwa  mara kuhusu utoaji haki kwa wakati. 

“Hii ndio njia pekee ya kuonesha weledi mkubwa ili huduma za Mahakama Kanda ya Kigoma ziendelee kuwa juu na zenye tija na hatimaye Mahakama ya Tanzania kwa ujumla,” alisisitiza Mhe. Mbelwa.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa akiwa ofisini kwake hivi karibuni wakati akiendesha kikao kwa njia ya mtandao cha kuwakumbusha Mahakimu Wafawidhi kuhusu usimamizi na ukaguzi wa shughuli za Mahakama katika Wilaya zao ili kuendelea kuongeza kasi ya usikilizwaji wa mashauri mahakamani.
                                                                                                              Jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma ambapo Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma Mhe. Fadhili Mbelwa, alipoendesha kikao chake kwa njia ya mtandao kabla kuanza shughuli za kimahakama. 

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)


 
 
 
 
 
 
 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni