Jumanne, 3 Juni 2025

MTENDAJI MKUU ATETA NA BARAZA LA UONGOZI IJA

Na INNOCENT KANSHA - Mahakama

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel amelihakikishia Baraza la Uongozi la Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto (IJA) kuwa Mahakama ya Tanzania, itaendelea kutoa ushirikiano katika kuhakikisha Chuo hicho kinaendelea kuwa kisima cha maarifa ili kizidi kuisaidia jamii.

Akizungumza na Baraza hilo la Uongozi mapema leo tarehe 03 Juni, 2025 Ofisini kwake Makao Makuu ya Mahakama Jijini Dodoma, Prof. Ole Gabriel amesisitiza kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya Tasisi zote mbili yaani Mahakama na Chuo kwa kuwa kwa kufanya hivyo kutatoa msukumo mkubwa katika utendaji kazi.

“Nitoe rai kwamba kama Chuo lazima kitekeleze majukumu yake kimkakati kwa kuwa na maono na malengo ya muda mrefu na kutafuta ufumbuzi wa kutatua kero na changamoto zilizopo zinazoweza kutatuliwa na pia wataalam wa Taasisi zote kushirikiana inapobidi ili kuja na mikakati ya maboresho mbalimbali ya kimifumo,” amesema Mtendaji Mkuu.

Aidha, Prof. Ole Gabriel ameshauri Uongozi kupanua wigo na kufiria kuongeza matawi ya Chuo kwenye majiji kama vile Dar es salaam, Mbeya na Dodoma ili kuwezesha Chuo kuongeza mapato ya ndani. Vilevile kuanzisha mkakati wa kuanza kufundisha kwa njia ya masafa (e-Classes) ili watu wengi zaidi wapate nafasi ya kupata maarifa kwa kujifunza kwa njia ya mtandao.

Matumizi ya TEHAMA yana mchango mkubwa katika kuboresha utendaji kazi,  Mathalani Mahakama ya Tanzania kwa sasa ni kinara wa Matumizi ya TEHAMA nchini. Hivyo basi Chuo ili kiweze kufundisha kwa njia ya masafa kinatakiwa kuboresha mifumo na matumizi ya TEHAMA ili kuimarisha utoaji wa elimu kwa njia hiyo.  

Mtendaji Mkuu ameongeza kwa kusema kuwa, Mahakama inamtandao nchi nzima na Majengo ya kisasa hivyo Chuo kikishapanua wigo wa kufundisha masomo kwa njia ya masafa kila inapofika mwisho wa muhula wa kimasomo wanafunzi wanaotakiwa kufanya mitihani wanaweza kutumia majengo ya Mahakama na kufanya mitihani huko huko waliko, mitihani kama ile ile inayofanywa na Wanafunzi kwenye kampasi Kuu na pia wanaweza kuwatumia Maafisa Mahakama kusimamia na kuwapa motisha na maisha yakazidi kutamalaki.

Vilevile, Prof. Ole Gabriel akaushauri Baraza la Uongozi kuanza kufikiria kutoa huduma kimataifa kwani Chuo kinafanya mambo mazuri wako watanzania wengi wanaishi nje ya nchi wangepeda kusoma IJA wawekewe utaratibu mzuri wa kujiunga na Chuo ili waweze kujiunga na kupata elimu inayotolewa na Chuo. Kupitia Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anaweza kusaidia hilo likawezekana.

“Chuo kinatakiwa kuendelea kulinda na kuheshimu itifaki za kiserikali na IJA hususani Waheshima Majaji kuna mahali pengine hawawezi kwenda kutekeleza kazi za Chuo basi watumike wawakilishi. Aidha kwa wale watumishi wa Chuo ambao siyo Maafisa Mahakama wafikiriwe kwa karibu ili kuongeza tija katika utendaji kazi,” amesema Prof. Ole Gabriel.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto (IJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mary Caroline Levira ameushurukuru Uongozi wa Mahakama kwa niaba ya Baraza la Uongozi wa Chuo kwa ushirikiano wanaopatiwa na Mahakama katika kutekeleza majukumu yao kama washauri wa Chuo.

“Mjadala wetu umekuwa wa manufaa makubwa kuna mambo mengi tumejifunza na tumepata uelewa wa pamoja ambao utatusaidia kwenda kutekeleza mipango kabambe ambayo tumejiwekea ya kukiendeleza na kuhakikisha IJA inafanya vizuri na tunasonga mbele,” amesisitiza Mwenyekiti huyo.

Aidha, Mhe. Dkt. Levira ameongeza kuwa, ni ari ya kila mwana IJA kuona kwamba anatimiza wajibu wake ili kuleta matokeo chanya na yakupigiwa mfano. Vilevile hoja nyingi zimefafanuliwa vizuri na kutoa muelekeo mpya tofauti na mtazamo wa Uongozi wa Baraza tuliokuwa nao awali kabla hatujafika hapa, hivyo basi Baraza la Uongozi litatoka hapa na taswira chanya juu ya hoja zilizojadiliwa kwa kina na kwa ufasaha mkubwa ili kuleta matokeo yaliyokusudiwa.

Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto (IJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mary Caroline Levira akiongoza kikao baina ya Viongozi Waandamizi wa Mahakama na Baraza la Uongozi la Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto (IJA) leo tarehe 3 Juni, 2025 ofisini kwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel jijini Dodoma.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel akifafanua jambo wakati wa mazungunzo baina ya Viongozi Waandamizi wa Mahakama na Baraza la Uongozi la Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto (IJA)


Sehemu ya wajumbe Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto (IJA) akifuatilia kwa makini mjadala kwenye kikao hicho, Kushoto ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama - Lushoto (IJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Dkt. Paul Faustine Kihwello na kulia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Gerson J. Mdemu.


Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto (IJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mary Caroline Levira akiongoza kikao baina ya Viongozi Waandamizi wa Mahakama na Baraza la Uongozi la Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto (IJA) leo tarehe 3 Juni, 2025 ofisini kwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel jijini Dodoma.


Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto (IJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mary Caroline Levira akifafanua jambo wakati wa kikao baina ya Viongozi Waandamizi wa Mahakama na Baraza la Uongozi la Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto (IJA) leo tarehe 3 Juni, 2025 ofisini kwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel jijini Dodoma.


Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto (IJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mary Caroline Levira akifurahia jambo wakati wa kikao baina ya Viongozi Waandamizi wa Mahakama na Baraza la Uongozi la Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto (IJA) leo tarehe 3 Juni, 2025 ofisini kwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel jijini Dodoma.

PICHA na INNOCENT KANSHA - Mahakama


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni