Jumanne, 3 Juni 2025

JAJI KIONGOZI ATOA WITO WANANCHI KUACHA KUSAMBAZA TAARIFA BINAFSI MITANDAONI

     Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama, Rukwa

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt, Mustapher Siyani ametoa wito kwa wananchi kujiepusha kusambaza katika mitandao ya kijamii taarifa binafsi za watu ambazo zimelindwa kisheria.

 

Jaji Kiongozi ambaye pia ni Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama ametoa wito huo mwishoni mwa wiki wakati alipokuwa akizungumza kwenye Mkutano kati ya Tume na Wadau wa utoaji haki mkoani Rukwa wakiwemo jeshi la Polisi, Magereza, Uhamiaji, Takukuru, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka pamoja na wadau wengine kwenye mnyororo wa utoaji haki.


Alisema kumekuwa na matumizi makubwa ya mitandao ya kijamii yakihusisha uchapishaji usiofaa wa taarifa zinazokiuka haki ya faragha na usalama wa watu ambapo ni kinyume na Sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi namba 11 ya mwaka 2022 yenye lengo la kulinda faragha za watu binafsi.

 

“Sheria hii imeainisha utaratibu wa namna ya kukusanya, kuchakata na kulinda taarifa binafsi na nyeti kama ilivyo katika kifungu cha 3 cha sheria hiyo”, alisema Jaji Kiongozi.

 

Aidha, alizitaja baadhi ya Sheria nyingine zinazolinda taarifa binafsi kuwa ni Sheria ya Mtoto, Sheria ya Mwenendo wa makosa ya Jinai, Sheria ya ulinzi wa Mashahidi na watoa taarifa, na Sheria ya Mwenendo wa mashauri ya jinai.

 

Alisema ni matarajio ya Tume na Mahakama kuwa wadau wa haki, Mahakama, wadaawa, na Mawakili watatunza na kulinda nyaraka zenye taarifa binafsi za watoto, taarifa za kuasili watoto, waathirika wa makosa ya kingono, hatua za kiusalama, afya, umri, hali ya ndoa ya wahusika, anuani, majina ya shule walikosoma, majina ya wazazi kwa kuwa taarifa hizo na nyingine nyingi zinalindwa na sheria ili kutofikiwa na mtu asiyehusika na kutozitoa au kuchapishwa katika vyombo vya habari au mitandao ya kijamii.


Akizungumzi nafasi ya wananchi kama wadau muhimu wa Mahakama, Jaji Kiongozi alisema Tume na Mahakama inatarajia kuwa wananchi wenye mashauri mahakamani pamoja na mashahidi watatoa ushirikiano kwa kufika mahakamani na kutoa Ushahidi wa kweli wanapotakiwa kufanya hivyo ili kuiwezesha Mahakama kutimiza jukumu lake la msingi la utoaji haki kwa wakati.

 

Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama wamemaliza ziara ya siku nne katika mikoa ya Katavi na Rukwa iliyolenga kuimarisha utoaji haki, kuitangaza Tume pamoja na kukutana na Wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama, Wadau wa utoaji haki pamoja na Watumishi wa Mahakama ya Tanzania.

 Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama  Mhe. Dkt, Mustapher Siyani akizungumza na wadau wa Utoaji Haki mkoani Rukwa.  

Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama  Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na wadau wa Utoaji Haki mkoani Rukwa. Kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Sumbawanga Mhe. Frederick Manyanda na kushoto ni Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Bw. Musalika Makungu.  

Sehemu ya Wadau wa Utoaji Haki Mkoa wa Rukwa wakiwa kwenye Mkutano kati yao na Tume ya Utumishi wa Mahakama mjini Sumbawanga.  

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni