· Asisitiza pia kuhusu ulinzi wa taarifa binafsi ‘Data Protection’
Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Mambi ametoa rai kwa Majaji, Mahakimu na Wadau wa Sheria kutumia fursa ya teknolojia ya kisasa na Akili Unde katika kazi ya utoaji haki nchini.
Akitoa mada hivi karibuni kuhusu Uzoefu wake wa Matumizi ya Akili Unde (AI) katika Utawala wa Sheria kwenye Mafunzo kwa Majaji, Naibu Wasajili, Watendaji wa Mahakama Kanda ya Ziwa yaliyofanyika jijini Mwanza, Mhe. Dkt. Mambi alisema matumizi ya Akili Unde (AI) hayakwepeki kwakuwa ni teknolojia ambayo imekuja kwa kasi duniani.
“Akili Unde ina matumizi mengi sana mahakamani, mfano programu kama ‘Quillbot’ husaidia kufanya utafiti wa kisheria, kutafuta kesi na sheria mbalimbali ambazo zinahusu kitu ambacho unashughulika nacho, lakini ukitaka kufupisha sheria, unataka labda uinukuu lakini pia inaweza kukusaidia pia uamuzi wako uliouandaa ikaupitia kama kuna makosa madogomadogo kama makosa ya kisarufi,” alisema Mhe. Dkt. Mambi.
Alitaja programu nyingine za Akili Unde (AI) ambazo zinaweza kusaidia kufanyia tafiti, uandishi wa hukumu na kadhalika nazo ni pamoja ChatGPT, CoPilot, Todoist na nyingine ambapo aliwafundisha kwa vitendo washiriki wa mafunzo hayo jinsi ya kuzitumia.
Jaji Mambi alisema Akili Unde ina faida kubwa katika utekelezaji wa majukumu ya kimahakama au katika utoaji wa uamuzi lakini pia katika Taasisi nyingine zinazotoa uamuzi mfano Mabaraza ya Ardhi, Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) na maeneo mengine.
Akitoa mfano kuhusu suala la mlundikano wa mashauri mahakamani, Jaji Mambi alisema kuwa, Akili Unde inaweza kusaidia kujua kwamba kuna mashauri yanakaribia kuwa mlundikano ‘backlog’ au yamebakiza muda fulani kuwa mlundikano kwahiyo inaweza kusaidia kufanya uamuzi kwa haraka kwa sababu shauri likichukua muda mrefu maana yake haki inachelewa kutendeka.
Aliongeza kuwa, Akili Unde inaweza kutumika pia katika kuangalia Mkataba kwa kuangalia maeneo ambayo yana mapungufu kwenye Mkataba husika, vilevile hutumika kufanya utabiri wa shauri juu ya uamuzi wake utakuwaje, hivyo inaisaidia Mahakama lakini pia inawasaidia wadaawa na wadau wengine kama Mawakili wa Serikali, Mawakili Binafsi kujua au kutabiri shauri fulani linaweza kuamriwaje.
Mhe. Dkt. Mambi alieleza kuwa, kwa sasa Mahakama ya Tanzania imepiga hatua katika matumizi hayo huku akitoa mfano wa Mfumo wa Unukuzi na Tafsiri (TTS) ambao hutumika kurekodi taarifa mfano shahidi anapotoa ushahidi au Wakili anapotoa hoja zake.
Jaji Mambi alisema kuwa, ni muhimu Mahakama na Wadau wa Sheria kuweka bajeti kwa ajili ya programu ‘Software’ za Akili Unde (AI) ambazo nyingine zina gharama ili kusaidia kurahisisha upatikanaji wa haki.
Hata hivyo, Jaji Mfawidhi huyo, alitoa angalizo kuwa, Akili Unde ina changamoto zake ambapo alisema, “siku zote hata kama unatumia Akili Unde (AI) wewe kama Jaji au Hakimu au Muamuzi ndio uwe wa mwisho kufanya uamuzi hutakiwi kuitegemea akili unde kwa asilimia 100 inaweza ikawa ‘biased’ kwa sababu haijapata taarifa za kutosha, kwa sababu akili unde inategemea taarifa kwa hiyo lazima wewe uwe wa mwisho kujiridhisha.”
Aidha, Mhe. Dkt. Mambi aliwakumbusha Majaji, Mahakimu na Wadau wa Sheria kuhusu Ulinzi wa Taarifa binafsi na kueleza kwamba ulinzi wa taarifa (data protection) ambayo Sheria yake ilipitishwa mwaka 2022 ni muhimu kuzingatiwa.“Sisi kama Mahakama na wadau wengine tunao wajibu wa kutunza taarifa za siri za wadaawa na taarifa nyingi kwa mfano taarifa za wanandoa, taarifa za watoto, taarifa za mirathi, kwa hiyo taarifa hizi zinapaswa kulindwa,” alisisitiza Jaji Mambi.
Vilevile, Mhe. Dkt. Mambi katika mada yake alisema licha ya teknolojia ya akili unde kusaidia kubaini na kuzuia uhalifu ikiwemo kutumika katika Ushahidi wa kielektroniki, teknolojia hiyo inaweza pia kutumika kutenda uhalifu wa makosa ya kimtandao.
Mafunzo hayo yaliandaliwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kwa kushirikiana na Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi ambapo moja ya malengo ya kufanyika kwake ni pamoja na kuandaa washiriki kuwa na ujuzi wa kisasa unaoendana na mabadiliko ya dunia ya kazi ili waweze kuchangia katika mazingira ya kazi yenye amani, usalama na tija kwa manufaa ya pande zote na kwa maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni