Jumamosi, 19 Julai 2025

KILA MMOJA ANA WAJIBU WA KUTUNZA HIFADHI ZETU; JAJI KIONGOZI

 Na MARY GWERA, Mahakama-Serengeti

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani amesema kuwa, suala la uhifadhi wa rasilimali ya wanyamapori ni jukumu la kila mmoja lengo likiwa ni kuhakikisha Wanyamapori hao wanaendelea kusalia.

Mhe. Dkt. Siyani aliyasema hayo jana tarehe 18 Julai, 2025 wakati ujumbe wa sehemu ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Watendaji, Naibu Wasajili na Wadau wa Mahakama walipotembelea Hifadhi ya Taifa Serengeti kufanya utalii.

“Kila mmoja wetu ni Mhifadhi, sisi kama Watanzania bila kujali fani zetu kwa kuwa tu ni Watanzania na kwa kuwa hifadhi ipo Tanzania tuna wajibu wa kutunza rasilimali hii,” alisema Mhe. Dkt. Siyani.

Jaji Kiongozi ameongeza kwa kutoa rai kwa Wadau wa Haki Jinai juu ya wajibu wao kama wasimamia haki kuhakikisha kuwa, hifadhi zinaendelea kuwepo kwa kusimamia ipasavyo eneo la haki hususani usimamizi wa mashauri ya uhalifu wa wanyamapori.

“Ni lazima mnyororo wa uhifadhi ufanye kazi yake, waliopangwa kuangalia mipaka waangalie, waliopewa wajibu wa kuzuia wahalifu wasiingie hifadhini watekeleze wajibu wao, waliopewa jukumu la kukusanya taarifa za kiintelejensia wafanye wajibu wao, waliopewa jukumu la kukamata wafanye jukumu hilo sawasawa, wanaopewa jukumu la kuandaa mashtaka wafanye jukumu hilo sawasawa, walio na jukumu la kuendesha mashauri mahakamani wafanye jukumu hilo sawasawa, wanaosikiliza mashauri mahakamani nao wafanye sawasawa bila kumuonea mtu yoyote,” amesema Mhe. Dkt. Siyani.

Amesema kwamba, anaamini kwamba, hizo ndio njia pekee kubwa na namba moja ambazo anayoona zitawezesha hifadhi hiyo kuendelea kuwepo.

Jaji Kiongozi ameeleza kuwa, “kumekuwa na changamoto ya mashauri mengi yanatokea hifadhini kushindwa hasa yanapofika Mahakama Kuu, wanaoendesha wanaweza kushinda kwenye Mahakama za chini lakini wakifika Mahakama Kuu na wakifanikiwa kupenya hapo yataishia Mahakama ya Rufani, yapo mafundisho kwa kila hukumu yanayoonyesha changamoto kuanzia kwenye ukamataji, uandaaji na uendeshaji wa mashauri hayo.”

Amesisitiza juu ya umuhimu wa Hifadhi hiyo na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kufanya kazi kwa karibu kuziba mianya ambayo inajitokeza kila wakati na kusababisha mashauri mengi kushindwa mahakamani.

“Jukumu la Mahakama siku zote sio kupendelea ni kuhakikisha haki inatendeka na haki haiwezi kutendeka kama kuna mianya ya kiupelelezi ambayo haipo sawa, hivyo ni muhimu kuendeleza kushirikiana,” ameeleza Mhe. Dkt. Siyani.

Aidha, Jaji Kiongozi amesema ni muhimu kuendelea kutoa mafunzo kuhusu ushughulikiaji wa mashauri yanayoanzia hifadhini ili kuhakikisha kwamba haki inatendeka bila kuwakatisha tamaa wale ambao wamepewa wajibu wa kuhakikisha kuwa hifadhi zetu zinaendelea kudumu na kukua.

Akiwasilisha mada ya hali ya Usalama wa Hifadhi ya Taifa Serengeti kwa ujumbe huo, Mhifadhi Mwandamizi kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Bw. Joachim Tesha alisema kuwa, hifadhi hiyo imeendelea kushika namba moja kwa kuwa hifadhi bora.

“Ndugu Viongozi Hifadhi ya Taifa Serengeti imeendelea kushika namba moja kwa mara ya saba mfululiza kwa kuwa hifadhi bora barani Afrika,” alisema Mhifadhi huyo Mwandamizi.

Akizungumzia kuhusu kukabiliana majangili, Bw. Tesha alieleza kuwa, wameendelea kutumia njia mbalimbali ikiwemo teknolojia ili kukabiliana na vitendo vya ujangili.

Ujumbe huo wa Mahakama na Wadau wake ulioongozwa na Jaji Kiongozi, Mhe. Dkt. Siyani ulipata fursa ya kujionea Wanyama mbalimbali ikiwa ni pamoja na Simba, Tembo, fisi, pundamilia, twiga na kadhalika.


Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (kushoto) akizungumza jambo wakati alipokuwa akizungumza na ujumbe wa Hifadhi ya Taifa Serengeti pamoja na Majaji, Wasajili, Watendaji wa Mahakama na Wadau waliotembelea Hifadhi hiyo jana tarehe 18 Julai, 2025. Katikati ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina na kulia ni Mwakilishi wa Mtendaji wa Wakala wa Usalamana Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Bw. Joshua Matiko.

Sehemu ya Wadau wa Mahakama.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (kushoto) akiwa pamoja na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina walipowasili  pamoja na wadau wengine wa Mahakama katika Hifadhi ya Taifa Serengeti jana tarehe 18 Julai, 2025.
Watalii kutoka Mahakama pamoja na Wadau wakipata maelezo kuhusu Hifadhi ya Taifa Serengeti kutoka kwa Afisa Wanyamapori wakati walipotembelea Hifadhi hiyo jana tarehe 18 Julai, 2025.


Simba wakionekana katika Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Swala.

Sehemu ya Watalii wa Mahakama na wengine waliotembelea Hifadhi ya Taifa Serengeti jana tarehe 18 Julai, 2025.

Utalii ukiendelea ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti.



Sehemu ya wanyama pori mbalimbali walioonekana jana katika Hifadhi ya Taifa Serengeti. Wanyama hao ni pamoja na Tembo, Twiga, Swala, Pundamilia na kadhalika.

(Picha na MARY GWERA, Mahakama)




 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni