Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma
Wasimamizi wa mirathi wanao wajibu mkubwa wanapoaminiwa na familia na kuteuliwa na Mahakama ili kukusanya na kugawa mirathi hiyo kwa warithi halali wa marehemu kwakuwa wasipofanya wajibu huo huleta migogoro isiyoisha katika familia.
Hayo yamebainishwa hivi karibuni na Msaidizi wa Sheria wa Jaji wa Mahakama Kuu Kigoma Mhe. Hassan Galiatano alipokuwa akitoa elimu kuhusu mirathi kwa wananchi waliofika Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma kupata huduma za kimahakama.
Aliwaasa, wananchi hao kuchagua msimamizi mwaminifu na ambaye atafanya majukumu yake sahihi na endapo atakwenda kinyume na utaratibu wa sheria ya kugawa mirathi basi warithi wanayo haki ya kumpinga mahakamani kwa kukosa imani nae kwa jinsi atakavyoenenda katika kusimamia usawa wa mirathi hiyo.
Aliwakumbusha pia, kuwa kikao cha ukoo au familia ndicho halali kinachompendekeza msimamizi wa mirathi na anaweza kuwa mtu yeyote aliyeaminiwa na wanafamilia hao kuwa msimamizi, ndipo Mahakama itaweza kufuata taratibu zake za kumthibitisha kuwa ni kweli wanafamilia wote wameridhia kwa kauli moja kuwa anafaa kuwa msimamizi, hapo ndio Mahakama itajiridhisha na kumthibitisha na kumpatia nguvu ya kisheria kusimamia mirathi ya marehem husika.
Aidha, aliwaeleza kuwa, mali za marehemu zinagawiwa kwa warithi halali wanaotambulika na sheria na sio kila ndugu wa marehemu anayo haki ya kurithi mali za marehemu husika.
Kwa upande wake Bi. Fitina Charles, mwananchi kutoka Wilaya ya Kasulu, aliishukuru Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma kwa elimu ambayo amepata ambayo ni muhimu katika jamii ya leo ambayo imekumbwa na wimbi la migogoro ya namna hiyo, ambapo ndugu wanagombania mali bila kupata suluhisho la migogoro hiyo, ambayo wakati mwingine husababisha vifo katika jamii.
Bi. Fitina aliendelea kusema kuwa, jamii imejeruhika kwa migogoro ya mirathi, tatizo likiwa ni uelewa mdogo wa taratibu za mirathi kwa warithi na wasimamizi wao. Hivyo, aliiomba Mahakama kuendelea na utamaduni huo wa kutoa elimu kwa jamii kupitia njia mbalimbali ikiwemo kwa wanaofika Mahakamani hapo kupata huduma za mashauri.
Msaidizi wa Sheria wa Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Hassan Galiatano akifafanua jambo hivi karibuni alipokuwa akitao elimu kwa wananchi juu ya mirathi.
Mwananchi kutoka kata ya Ujiji-Kigoma, Bw. Swalehe Hamis akiuliza swali la hatua za wanafamilia watakazochukua kama msimamizi wa mirathi akishindwa kufanya majukumu yake.
Mwananchi kutoka Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, Bi. Fitina charles akitoa shukrani kwa Mahakama kupitia Msaidizi wa Sheria wa Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma Mhe. Hussan Galiatano aliyetoa elimu ya wajibu wa msimamizi wa mirathi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni