Jumatatu, 21 Julai 2025

MWILI WA MAREHEMU BI. SOPHIA WAAGWA KWA IBADA MAALUM

 Na INNOCENT KANSHA-Mahakama

Majaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Naibu Wasajili wa Mahakama Kuu na Rufani, Wakurugenzi, wakurugenzi wasaidizi na Wakuu wa Idara na Vitengo kutoka Mahakama ya Tanzania jana tarehe 20 Julai, 2025 waliungana na Watumishi wa Mahakama, ndugu, jamaa na marafiki kuuaga mwili wa marehemu Bi. Sophia Bakari Mohamed aliyekuwa mtumishi wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania nyumbani kwake katika viunga vya mtaa wa Kikuyu jijini Dodoma.

Awali akitoa salamu za pole kwa niaba ya Mahakama na kumuelezea Bi. Sophia, Mtendaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Bw. Victor Kategere alimuelezea Mtumishi huyo kuwa alihudumu Mahakamani kwa takribani miaka 5 na alikuwa muadilifu na mchapa kazi watu wote walimpenda kwa jitihada zake kazini.

“Mtumishi wetu Sophia Bakari Mohamed ambaye tulikuwa naye Mahakama, alikuwa mtumishi ambaye hata sisi wenyewe tulimpenda sana lakini haya masuala mengine yaliyotokea kama hili ni mambo ambayo wote hatuwezi kuyakwepa. Naamini linapotokea tukio kama hili mara nyingi mwenzetu kazi yake ameimaliza na safari yake imefika mwisho,” alisema Mtendaji huyo.

Mtendaji huyo aliongeza kuwa, kinachotakiwa kuangaliwa wakati tunamsindikiza na kusherekeka maisha ya mpwenda wetu ni sisi wenyewe kuendelea kutafakari binafsi na wewe mwenzangu tumejipangaje ili safari yetu iweze kuwa nzuri lakini pia tuwe na historia njema, mtakumbuka pia kwamba kuna mpendwa wetu Rais Msataafu aliwahi kusema kwamba, kifo hakikwepeki lakini ni vizuri uwe umejiandaa ili historia yako itakayo baki iwe historia jema na kuandika kitabu chema….

Wito mkubwa katika tukio hili ni sisi wenyewe kujipanga na kutafakari maisha yatu wenyewe yanavyokwenda tulimpenda sana Sophia wengine tumefanya naye kazi, wengine wamesoma naye wameshirikiana naye kwenye mambo mengi basi hayo yote yaliyofanyika ni kwa mpango wa mwenyezi Mungu. Basi kwa pamoja tuendelee kumuombea ili aweze kupumzika kwa Amani na mwenyezi Mungu aweze kumpokea mahali pema pepeoni,” aliongeza Bw. Kategere.

Kwa upande wake, Mchugaji kutoka Kanisa la Kiinjili la kilutheri Tanzania (KKKT) akitoa mahubiri alisema, matukio ya msiba ya namna kama huo siyo jambo rahisi kuyapokea kuachana na mtu mliyemzoea ambaye hamtakuwa naye tena katika macho ya nyama hasa ninyi watumishi wenzake.

Huu msiba unaumiza kwa sababu ni miaka 29 tu bado mpendwa wetu alikuwa kijana, kijana wa miaka 12 mpaka 35 bado ana nafasi kubwa ya nguvu kazi kabisa. Tena yamkini alikuwa na nafasi ya kujiendeleza kielimu ili kuboresha sifa na utukufu kwenye jamii yetu ya kitanzania na kwenye familia pia, kwa hiyo niendelee kusema Mungu atutie nguvu sana.

Akifafanua Mchungaji alisema, neno liliosomwa linasema mwili wa ufufuo katika kristo, ni kweli misiba inaumiza sana na hata wakati mwingine tunaona kama tumempoteza vile tu hatuna namna lakini niseme ndugu yetu huyu ameondoka ametangulia kwenye pumziko la milele, lakini kuondoka kwake ni vigumu kulipokea na kulikubali na hata watumishi wenzake mnaendelea kuona uwepo wake, ambao sasa haupo pamoja nanyi.

Mchungaji ameongeza kuwa, Sura nzima ya waraka huo inagusa juu ya maisha binadamu yanayotaka kuwe na mahusiano na Mungu ikimaanisha kwamba kifo cha kutengana ndugu na jamaa siyo mwisho wa kutengana na mahusiano na Mungu bali kinatoa nafasi ya kutengana na binadamu wengine na ndiyo maana hakizoeleki siku zote, kinapotokea kinatisha na kinaonekana ni kipya kwenye macho ya nyama.  

Aidha, Mchungaji amesema ni muda wa waamini wote kutafakari kwa kina maisha baada ya yale dunia yaani maisha baada ya kifo je waamini mmejipanga vipi kuhusu maisha yenye makazi mapya ambayo ni fumbo kwa kila mmoja wetu, hivyo tuendelee kuamini kuna uzima na ufufuko wa milele.





































(PICHA NA INNOCENT KANSHA-Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni