Na EMMANUEL OGUDA, Mahakama-Shinyanga
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga imeshiriki kikamilifu kutoa elimu katika Tamasha la Utamaduni wa Msukuma msimu wa nne maarufu kama ‘Shinyanga Sukuma Festival Season 4’.
Tamasha hilo lilifanyika katika Kata ya Kizumbi Kijiji cha Nhelegani Manispaa ya Shinyanga ambapo kwa mwaka huu, tamasha hilo limefanyika kwa siku tatu (3) mfululizo kuanzia tarehe 18 hadi 20 Julai, 2025.
Mbali na maonesho mbalimbali ya utamaduni wa Msukuma, Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga ni miongoni mwa taasisi za umma zilizopata nafasi ya kushiriki katika zoezi la utoaji elimu katika tamasha hilo.
Miongoni mwa elimu zilizotolewa na Watumishi wa Mahakama Kuu Shinyanga ni pamoja na ufunguaji wa mashauri mbalimbali yakiwemo ya jinai na madai kwa njia ya mtandao, huduma za usikilizaji wa mashauri mahakamani kwa njia ya mtandao yaani ‘Electronic Case Management System(e-CMS)’, huduma za usikilizaji wa mashauri kwa njia ya video ‘Video Conferencing’, Mfumo wa Kielektroniki wa Mawakili (e-Wakili) ili kuepuka vishoka pamoja na kusikiliza wateja mbalimbali waliojitokeza katika banda la Mahakama.
Hali kadhalika, mbali na maonesho mbalimbali kutoka katika taasisi zilizoshiriki katika tamasha hilo, miongoni mwa vivutio vilivyokonga nyoyo za wanachi wa Shinyanga ni burudani ya aina yake kutoka vikundi vya utamaduni huku kikundi cha Sungusungu kutoka Kata ya Mwamalili Manispaa ya Shinyanga kikiwa kivutio kikubwa kwa mamia ya wananchi waliojitokeza katika tamasha hilo.
Tamasha la kuenzi utamaduni wa Msukuma maarufu kama Shinyanga ‘Sukuma Festival Season 4’ liliasisiwa na Bw. Frank Peter (Mr. Black) hufanyika mwezi Julai kila mwaka kuenzi tamaduni mbalimbali za Msukuma huku Taasisi mbalimbali zikishiriki kikamilifu kutoa elimu pamoja na huduma zinazotolewazo na Taasisi hizo.
Tamasha hilo lilizinduliwa tarehe 18 Julai, 2025 na Katibu Tawala wa Wilaya ya Shinyanga, Bw. Said Kitinga na kuhitimihwa jana tarehe 20 Julai, 2025 na mgeni rasmi Chifu wa Wasukuma eneo la Kizumbi Chifu Charles Njange Kidola.
Afisa TEHAMA wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Bi. Nashilaa Mollel akitoa elimu ya namna ya ufunguaji wa mashauri kwa njia ya mtandao wakati wa Tamasha maarufu Shinyanga la 'Sukuma Festival Season Four' lililofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Nhelegani Manispaa ya Shinyanga kuanzia tarehe 18 hadi 20 Julai, 2025.
Sehemu ya wananchi wa Shinyanga na maeneo mbalimbali walioshiriki katika Tamasha kubwa la utamaduni wa msukuma maarufu kama Sukuma Festival Season Four lililofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Nhelegani kuanzia tarehe 18 hadi 20 Julai, 2025.
Picha ya wananchi mbalimbali waliohudhuria katika Tamasha la Shinyanga Sukuma Festival, 2025.
Chifu wa wasukuma Kizumbi Shinyanga, Chifu Charles Njange Kidola (aliyekaa) akiwa katika Tamasha la Shinyanga Sukuma Festival katika viwanja vya Shule ya Msingi Nhelegani Manispaa ya Shinyanga.
Mwanzilishi wa Tamasha la Shinyanga Sukuma Festival, Bw. Frank Peter (Mr. Black) (aliyesimama katikati) akionesha sehemu ya utamaduni wa Msukuma.
Kikundi cha burudani cha Sungusungu kutoka Kata ya Mwamalili Manispaa ya Shinyanga wakitoa burudani kwa mamia ya wananchi waliohudhuria katika Tamasha kubwa la utamaduni wa Msukuma maarufu kama Shinyanga 'Sukuma Festival Season Four'.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni