Jumatatu, 21 Julai 2025

MUENDELEZO WA VIKAO USIKILIZA MASHAURI YA MAHAKAMA YA RUFANI KUENDELEA MBEYA

Na Daniel Sichula – Mahakama, Mbeya

Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania Mhe. Barke Sehel afungua kikao cha awali cha tathmini ya usikilizaji wa mashauri ya rufaa kwa mwaka 2025/2026 katika Mahakama ya Rufani Kanda ya Mbeya.

Akipokea taarifa ya tathimini kutoka kwa Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania Mhe. Charles Magese alisema kuwa mashauri 25 yamepangwa kusikilizwa kuanzia tarehe 21 Julai 2025 hadi 07 Agosti 2025.

Aidha, akisoma taarifa hiyo Mhe. Magese alifafanua kwamba, Mashauri 12 ni mashauri ya jinai na 12 ni mashauri ya madai na mashauri yote ni ya mlundikano na shauri moja ni maombi.

Usikilizaji wa mashauri hayo ya rufaa utaongozwa chini ya jopo la Majaji watatu akiwemo Mwenyekiti wa jopo hilo Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania Mhe. Barke Sehel, Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania Mhe. Zepharine Galeba na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania Mhe. Amour Khamis

Mara baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Mhe. Magese, wajumbe walijadili na kutoa changamoto zinazoweza kujitokeza na namna ya kutatua kabla ya usikilizaji wa mashauri kuanza ikiwemo wafungwa walioko mbali na mkoa wa Mbeya kufika kwa wakati mahakamani.

“Mhe. Jaji, wafungwa wote waliopo mbali na Mkoa Mbeya taratibu zimeshafanyika kabla ya kuanza vikao jumatatu watakua tayari mkoani Mbeya na tutawafikisha kwa wakati mahakamani,” alisema Afisa Magereza.

Vilevile, Afisa Magereza huyo alitoa ombi kwa joto la Majaji wa Rufani kuweza kutoa hukumu kwa wakati kwa wadaawa waliopo magerezani.

Katika kikao hicho shauri moja liliombwa kuondolewa na mmoja wa wajumbe waliohudhuria.

“Ni muhimu kutolea taarifa mapema kwa mashauri ambayo mnataka kuyaondoa kabla hayajapangiwa usikilizaji kwani hili litasaidia kuondoa na kupanga shauri linguine,” alisema Mhe. Sehel.

Mhe. Sehel aliwasisitiza wajumbe wote wakiwemo Mawakili wa Serikali, Maafisa wa Magereza, Polisi, Mawakili wa Kujitegemea, Ofisi ya Waendesha mashtaka (NPS) kuwahi kufika kwenye kesi mapema na kuwaambia usikilizaji wa mashauri utaanza saa 3.30 asubuhi.

Aidha, kikao hicho kilihudhuriwa na uongozi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya uliyowakilishwa na Jaji wa Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Tiganga, Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Aziza Temu, pamoja na Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Bi. Mavis Miti.

Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania Mhe. Barke Sehel afungua kikao cha awali cha tathmini ya usikilizaji wa mashauri ya rufaani Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya.

Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania Mhe. Charles Magese akitoa taarifa ya usikilizaji mashauri ya Mahakama ya Rufani Kanda ya Mbeya.

Afisa kutoka Magereza akitoa mchango wakati wa kikao cha tathmini ya vikao vya Mahakama ya rufaani.

Sehemu Viongozi wa Mahakama Kanda ya Mbeya waliohudhuria kikao cha tathmini ya vikao vya mahakama ya rufaani Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya.

Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania Mhe. Barke Sehel (katikati), Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania Mhe. Zepharine Galeba (kushoto) na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania Mhe. Amour Khamis (kulia) wakiwa kwenye kikao hicho.




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni