• Mashauri 30 kusikiliwa
Na SETH KAZIMOTO, Mahakama-Arusha
Mahakama ya Rufani ya Tanzania imepiga kambi katika Mahakama ya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha kuendesha Kikao cha Mashauri kuanzia tarehe 21 Julai hadi Agosti 07, 2025 ambapo jumla ya mashauri 30 yamepangwa kusikilizwa.
Akizungumza wakati wa kikao cha awali kilichofanyika tarehe 18 Julai, 2025 kwenye ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha, Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Rashid Chaungu amesema kuwa Kikao hicho, kitakuwa na Rufaa za Jinai 13, Rufaa za Madai 11 na Maombi ya Madai sita, hivyo kufanya jumla ya mashauri 30 yatakayosikilizwa katika kikao hicho.
“Katika kufikia malengo yaliyokusudiwa, maandalizi ya kikao yameshafanyika ikiwa ni pamoja na ratiba na Hati za Kuitwa Shaurini (summons) kwa mashauri yaliyopangwa kutolewa kwa wakati” alisema Mhe. Chaungu.
Kikao hicho kitakuwa na jopo moja lenye jumla ya Majaji wa Mahakama ya Rufani wanne wakiongozwa na Mhe. Rehema Mkuye ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jopo, Majaji wengine watakaohusika katika usikilizaji wa mashauri katika kikao hicho ni Mhe. Lucia Kairo, Mhe. Gerson Mdemu na Mhe. Abdulhakim Issa.
Kufanyika kwa kikao hicho ni utekelezaji wa mpango maalum wa Mahakama ya Rufani wa kumaliza mashauri na kwa mujibu wa kalenda ya Mahakama hiyo, kikao hicho ni cha pili kwa mwaka huu na kitafanyika sanjari na vikao vingine vinavyofanyika katika Kanda za Mwanza, Moshi, Dar es Salaam, Mbeya na Dodoma.
Mwenyekiti wa Jopo, Mhe. Rehema Mkuye akiongoza kikao cha awali cha maandalizi ya Kikao cha Mashauri kilichofanyika tarehe 18 Julai, 2025 kwenye ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.
Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Rashid Chaungu akifafanua jambo wakati wa Kikao cha awali cha Maandalizi kilichofanyika tarehe 18 Julai, 2025 kwenye ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha. Kulia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Rehema Mkuye na kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Frank Mahimbali.
Wadau mbalimbali wa mashauri ya Jinai na Madai walioshiriki katika kikao cha maandalizi kilichofanyika tarehe18 Julai, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni