Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Dar es Salaam
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi amewataka viongozi wanaofanya kaguzi katika Mahakama za chini zilizopo katika Kanda hiyo kuwa wabunifu katika ukaguzi wa Mahakama hizo.
Mhe. Maghimbi alieleza hayo katika kikao cha Kamati ya Uongozi wa Kanda ya Dar es Salaam kilichofanyika tarehe 18 Julai, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Kinondoni.
Mhe. Maghimbi alisema katika kaguzi alizofanya amebaini baadhi ya mapungufu katika kaguzi zinazofanywa na wafawidhi, ambapo ameeleza kuwa, kuna mazoea katika kazi ya ukaguzi hivyo amewataka kufanya ukaguzi kwa ubunifu kila mkaguzi awe na mbinu mpya kila aendapo kukagua, “(there is no business as usual every day is a new day) hakuna kufanya biashara kimazoea wakati wote, kila siku ni siku mpya),” alisisitiza Jaji Maghimbi.
Katika kukabiliana na hilo, Jaji Mfawidhi alitaka kupatiwa siku moja kwa Maafisa Ukaguzi na Mahakimu wote ili waweze kupata mafunzo ili kuweza kufanya kaguzi zenye ufanisi.
Alisema, hawezi kumlaumu mtu kabla ya kumfundisha hivyo baada ya mafunzo
hayo kama kuna mtu atashindwa itakuwa yeye lakini yeye kama kiongozi atakuwa
hana lawama.
Kadhalika, Jaji Maghimbi ameomba walau mara mbili kwa mwaka upatikane muda wa kukutana na kufanya vikao maalum vya kitaaluma na kubadilishana uzoefu katika kazi maana kuna changamoto nyingi wanazokutana nazo kila siku hivyo ni vema kuwa na vikao hivyo ili kushirikishana.
“Tukiwa na utaratibu wa kufanya vikao hivi tunaweza kutatua changamoto zetu huenda Mahakama fulani walikutana nayo na waliishughulikiaje hivyo na wewe ukikutana nayo utaweza kujifunza kupitia Mahakama hiyo,” alisema Mhe. Maghimbi.
Naye, Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Mary Moyo akitoa taarifa ya mashauri kuanzia Januari mpaka tarehe 30, Juni mwaka huu, alisema kasi ya umalizaji wa mashauri imeongezeka kutoka asilimia 99 mpaka asilimia 102.
Katika taarifa yake, Mhe. Moyo alizipongeza Mahakama ya Wilaya Ubungo, Mahakama za Mwanzo Kwembe, Kigamboni na Kimara kwa kufanyia kazi mfumo wa utoaji nakala za hukumu ipasavyo na hakuna mashauri ya mlundikano.
Wakati huohuo, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam,
Mhe. Aziza Mbadjo aliwataka Mahakimu Wafawidhi wa Kanda hiyo kufikika kwa wananchi
ili kuepuka malalamiko yanayofika katika dawati lake la malalamiko kwani amebaini
malalamiko mengi yanatokana tu na ugumu wa wafawidhi kufikika kwa urahisi kwakuwa
kama wangefikika wangeweza kusuluhisha changamoto hizo.
Kikao hicho cha robo ya mwisho ya mwaka 2024/2025 kimekuwa na maazimio ya muda mfupi na ya muda mrefu ikiwemo kutekeleza mwongozo wa Jaji Mkuu unaohusu mahabusu wa Mahakama za Mwanzo lakini pia kuwepo ukaguzi wa awali kupitia mfumo kabla ya kutembelea vituo husika.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Wasajili, Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama za Wilaya, Maafisa Utumishi na Maafisa Tawala, Wahasibu, Maafisa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na Maafisa Ugavi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Mghimbi (katikati) akiwa katika kikao cha Kamati ya Uongozi wa Kanda ya Dar es Salaam kilichofanyika tarehe 18 Julai, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Kinondoni. Kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Mary Moyo na kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Bw. Moses Mashaka.
Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Mary Moyo akiwasilisha taarifa ya mashauri ya mwezi Januari mpaka Juni 30, 2025 wakati wa kikao cha Kamati ya Uongozi Kanda ya Dar es Salaam.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Mghimbi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Naibu Msajili Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Mary Moyo, kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam. Waliosimama ni Naibu Wasajili kutoka kushoto ni Mhe. Livin Lyakinana, Mhe. Franco Kiswaga na Mhe. Aziza Mbadjo.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni