- Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora apongeza ushirikiano wa Mahakama na wadau wa sekta ya haki
Na AMANI MTINANGI, Mahakama - Tabora
Mahakama
Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora imeendesha mafunzo maalum kwa wadau wa haki
jinai kuhusu makosa ya kimtandao yanayolenga kuwajengea uwezo wadau hao
kukabiliana na uhalifu unaohusisha teknolojia ya kisasa na namna ya kutumia
teknolojia kuzia uhalifu.
Mafunzo
hayo yalifanyika jana tarehe 14 Agosti, 2025 katika ukumbi wa Chuo cha Utumishi
wa Umma mkoani Tabora chini ya uongozi wa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda
ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Juma Mambi ambaye pia alikuwa Mwezeshaji mkuu wa
mafunzo hayo.
Mgeni
rasmi wa mafunzo hayo ambaye ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dkt. John
Rogath Mboya alitumia fursa hiyo kumpongeza Jaji Mfawidhi wa Kanda ya Tabora
kwa mchango wake mkubwa katika kuimarisha uelewa wa matumizi ya Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na jinsi ya kukabiliana na makosa ya mtandaoni.
“Ninampongeza
sana Mhe. Dkt. Mambi ambaye ni mbobezi mkubwa katika masuala ya Teknoljia na
Sheria za TEHAMA kwa juhudi zake binafsi na kwa kujitolea kutoa elimu hii
muhimu kuhusu akili bandia na teknolojia za kisasa zinazosaidia ukusanyaji wa
ushahidi na kuzuia uhalifu wa kimtandao,” alisema Dkt. Mboya huku akiongeza
kuwa Mhe. Dkt. Mambi amekuwa akionesha ushikiano mkubwa kwa wadau wa haki jinai.
Kwa
mujibu wa Mhe. Jaji Dkt. Mambi, lengo la mafunzo hayo ni kuhamasisha matumizi
ya teknolojia zinazoibuka kwa kasi kama akili unde (AI) na mifumo ya
kiteknolojia katika upelelezi wa makosa ya mtandao, kudhibiti ujangili katika
hifadhi za taifa, ukusanyaji wa ushahidi wa kielektroniki, pamoja na kulinda taarifa
binafsi na haki za binadamu katika mazingira ya kidijitali.
Kwa
mujibu wa Mhe. Dkt. Mambi, lengo la mafunzo hayo ni kuhamasisha matumizi ya teknolojia
zinazoibuka kwa kasi kama Akili Unde (AI) na mifumo ya kiteknolojia katika
upelelezi wa makosa ya mtandao, kudhibiti ujangili katika hifadhi za taifa, ukusanyaji
wa ushahidi wa kielektroniki, pamoja na kulinda taarifa binafsi na haki za
binadamu katika mazingira ya kidijitali.
Washiriki
wa mafunzo hayo walijifunza namna ya kutumia mbinu za teknolojia ya Akili Unde
katika kusimamia uhalifu wa majangili katika hifadhi za Taifa, usimamiaji wa
rushwa, makosa ya mtandao pamoja na mbinu ambazo wahalifu wanatumia teknolojia
ya Akili-Unde katika kutenda uhalifu.
Mafunzo hayo yatafanyika kwa siku ya
pili ambapo wadau wa Haki Jinai watapata
fursa ya kujifunza zaidi kuhusu utaratibu wa kisheria wa kukusanya ushahidi wa
kielektroniki na utaratibu wa kuwasilisha ushahidi wa kilektroniki mahakamani kabla
Mahakama haijatoa uamuzi.
Mafunzo
hayo yaliyoratibiwa na Ofisi ya Mashtaka Kanda ya Tabora yaliwaleta pamoja
wadau kutoka taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Jeshi la Polisi, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Mamlaka
ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na
Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA).
Ushirikiano huo ni mfano wa namna Mihimili ya Dola na Taasisi nyingine za Umma zinavyoweza kushirikiana katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu vinavyokua kwa kasi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Mhe. Jaji Dkt. Adam Juma Mambi akiwasilisha mada kuhusu matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kudhibiti uhalifu wa kimtandao yalifanyika jana tarehe 14 Agosti, 2025 katika ukumbi wa Chuo cha Utumishi wa Umma mkoani Tabora.
Washiriki wa mafunzo ya makosa ya kimtandao wakifuatilia kwa makini mada zilizowasilishwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Juma Mambi (hayupo katika picha).
Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dkt. John Rogath Mboya (kulia) akitoa salamu za pongezi kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Mambi kwa kujitolea kwake kutoa mafunzo yenye tija kwa wadau wa sekta ya haki jinai.
Mmoja kati ya washiriki wa mafunzo akishiriki kikamilifu katika majadiliano wakati wa mafunzo hayo.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni