· Amuelezea Hayati Ndugai kuwa mpenda haki
Na MARY GWERA,
Mahakama - Dodoma
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. George Mcheche Masaju leo tarehe 10 Agosti, 2025 ameungana na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson na Watanzania kwa
ujumla katika ibada ya kumuaga Spika Mstaafu wa Bunge, Hayati Mhe. Job Yustino
Ndugai aliyefariki dunia tarehe 06 Agosti mwaka huu.
Ibada ya kumuaga Hayati
Ndugai imefanyika katika Viwanja vya Bunge la Jamhuri la Muungano wa Tanzania
jijini Dodoma huku ikihudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Serikali na wananchi.
Kabla ya kuanza kwa ibada
ya kuaga mwili wa Hayati Job Yustino Ndugai ilitanguliwa na ratiba ya kuwasili
kwa Waombolezaji, Viongozi katika viwanja hivyo na baadaye kufuatiwa na nyimbo
za maombolezo kutoka Wasanii na Vikundi mbalimbali wakiwemo Vijana wa Kigogo,
Mrisho Mpoto, Peter Msechu, Starah Thomas, Linah Sanga, Kwaya ya Bunge na Kwaya
ya Kanisa la Anglikana.
Mara baada ya Rais Samia
kuwasili katika Viwanja vya Bunge, mwili wa Hayati Job Ndugai uliingizwa katika
eneo ambalo lilikuwa limeandaliwa kwa ajili ya ibada ya kumuaga.
Mara baada ya kumalizika
kwa ibada kumalizika Viongozi mbalimbali walitoa salamu za rambirambi akiwemo Jaji
Mkuu, Mhe. Masaju ambapo amesema kuwa, kwa upande wa Mahakama Hayati Ndugai
atakumbukwa kwa sifa yake ya kuwa mpenda haki.
“Nimepata fursa ya
kumtambua Spika Ndugai nilipokuwa Katibu Binafsi wa Waziri wa Katiba na Sheria
wa wakati huo Hayati Mhe. Bakari Mwapachu na sababu ya kumfahamu alihitaji sana
kujengwa kwa Mahakama pale Kongwa, kwahiyo akawa anakuja na Waziri kuomba
Mahakama ya Wilaya ijengwe katika Kongwa badala ya wananchi kwenda Mpwapwa na
baadaye Mahakama hiyo ilijengwa,” amesema Mhe. Masaju.
Jaji Mkuu amesema kuwa,
alishirikiana pia na Hayati Ndugai katika uzinduzi wa Mahakama ya Mwanzo
Kibaigwa na baadaye katika tukio la kuzinduliwa kwa Mahakama ya Wilaya Kondoa
wakati huo Jaji Mkuu akiwa Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma.
“Kwetu sisi Mahakama,
tutaendelea kumuenzi Hayati Ndugai kwa sababu ya mchango wake wa kupenda sana
haki, vilevile nitamkumbuka Mhe. Ndugai pamoja Mhe. Anne Makinda kwa
ushirikiano walionipatia nilipokuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali,” ameeleza
Mhe. Masaju.
Jaji Mkuu ameongeza kuwa,
wakati wa uzinduzi wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050, moja ya vitu
ambavyo Rais Samia alisema kuhusu Mahakama ya Tanzania ni kwamba Mhimili huo
uendelee kutenda haki kwa kuzingatia viapo bila hofu, upendeleo, huba wala chuki.
“Kama mtakavyokumbuka moja
ya vipaumbele vya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Tanzania 2050 ni haki,
nawashukuru watumishi wa Mungu kwa kutuombea na kutambua mchango wetu sisi Mahakimu
na Waamuzi kwamba tuendelee kutekeleza majukumu yetu kwa kuzingatia viapo vyetu,”
amesema Mhe. Masaju.
Aidha, Jaji Mkuu amewapa
neno la faraja familia ya Hayati Ndugai na waombolezaji kwa ujumla kuwa, kila
binadamu anapoondoka anaacha pengo na pigo ambalo halizibiki kwa kuwa kila mtu
ni wa kipekee na ana utambulisho wake, hivyo ni vyema kuendelea kuishi kwa
kutokuumia zaidi kwakuwa kuna maisha baada ya kifo kama wasemavyo viongozi wa dini.
Viongozi wengine walioambatana na Jaji Mkuu ni pamoja na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Amour Said Khamis, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Manyara, Mhe. Nenelwa Mwihambi na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel.
Mbali na Jaji Mkuu,
Viongozi wengine waliohudhuria katika ibada hiyo ni pamoja na Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, Waziri Mkuu wa
Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mhe.
Hemed Suleiman Abdulla, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Doto
Mashaka Biteko, Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Bunge, Mhe. William Lukuvi,
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule na viongozi wengine.
Hayati Job Yustino Ndugai
anatarajiwa kupumzishwa kwenye makazi yake ya milele kesho tarehe 11 Agosti,
2025 wilayani Kongwa.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akisaini Kitabu cha Maombolezo alipowasili katika Viwanja vya Bunge jijini Dodoma leo tarehe 10 Agosti, 2025 kwa ajili ya kushiriki kwenye ibada ya kumuaga Spika Mstaafu wa Bunge la Tanzania, Hayati Job Yustino Ndugai.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni