- Wananchi wavutiwa na elimu ya Mahakama waliyopata ndani ya Mahakama Inayotemebea
Na AMANI MTINANGI, Mahakama - Tabora
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora imeendelea kutoa elimu kwa umma kupitia Mahakama Inayotembea katika viwanja vya Maonesho ya Nanenane vilivyopo Manispaa ya Tabora, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha uelewa wa wananchi kuhusu huduma zinazotolewa na Mahakama pamoja na mchakato mzima wa upatikanaji wa haki nchini.
Akizungumza na wananchi
waliotembelea banda hilo jana tarehe 08 Agosti, 2025, Naibu Msajili wa Mahakama
Kuu Kanda ya Tabora, Mhe. Pamela Mazengo alisisitiza dhamira ya Mahakama ya
Tanzania ya kuhakikisha huduma za utoaji haki zinawafikia wananchi wote kwa
uwazi, uwajibikaji na kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
"Mahakama ya Tanzania imejipanga kuhakikisha kuwa huduma za utoaji haki zinawafikia wananchi wote kwa uwazi, uwajibikaji na kwa kutumia teknolojia ya kisasa. Kupitia Mahakama Inayotembea, tunalenga kuwafikia wananchi walioko maeneo ya mbali ambao mara nyingi hukosa huduma hizi muhimu kwa ukaribu, uwazi, uwajibikaji na kwa kutumia teknolojia ya kisasa,” alisema Mhe. Mazengo.
Naibu Msajili huyo
alieleza kuwa, Mahakama Inayotembea ni mojawapo ya njia ya kuwafikia wananchi
walioko mbali na huduma hizo muhimu na kwamba maonesho kama hayo ni jukwaa bora
la kutoa elimu ya kisheria kwa umma ili kuimarisha uelewa wa wananchi kuhusu
mfumo wa utoaji haki na kujenga imani kwa Taasisi ya Mahakama.
Kwa upande wake, Hakimu
Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Tabora, Mhe. Shaibu Mzandah aliwahimiza
wananchi kutumia fursa ya Mahakama Inayotembea kupata elimu na usaidizi wa
kisheria, huku akiweka bayana kuwa, huduma zinazotolewa hazitozwi malipo yoyote
na ni sehemu ya jitihada za Mahakama kuondoa changamoto za upatikanaji wa haki
hasa kwa wananchi wa kawaida.
"Naendelea kuhimiza
wananchi wote kutumia kikamilifu fursa ya Mahakama Inayotembea kupata elimu na
usaidizi wa kisheria, kwani huduma hizi zinatolewa bure bila malipo yoyote. Hii
ni sehemu ya jitihada za Mahakama ya Tanzania katika kuhakikisha kuwa haki
inapatikana kwa urahisi na kwa usawa, hasa kwa wananchi wa kawaida ambao mara
nyingi hukumbana na changamoto mbalimbali za upatikanaji wa huduma za kisheria,"
alisema Mhe. Mzandah.
Mgeni rasmi katika hafla
hiyo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Mhe. Saimon Sirro ambaye alikagua
mabanda mbalimbali ya maonesho na kusisitiza wataalam wa Taasisi mbalimbali
kuwawezesha wananchi na wadau kuandaa bidhaa za kilimo katika vifungashio
vinavyokidhi vigezo ya kimataifa.
"Mimi nasisitiza
kuwa ni muhimu kwa wataalam kutoka Taasisi mbalimbali kuwasaidia wananchi na
wadau wa kilimo kuandaa bidhaa zao katika vifungashio vinavyokidhi viwango vya
kimataifa. Hii itasaidia kuongeza thamani ya mazao na kuhakikisha bidhaa zetu
zinashindana vyema sokoni, ndani na nje ya nchi," alisema Mkuu wa Mkoa huyo.
Wananchi waliohudhuria kwenye
maonesho hayo walionesha kufurahishwa na huduma zinazotolewa na Mahakama
kupitia Mahakama Inayotembea, huku wakieleza kuwa wamepata maarifa mapya kuhusu
haki zao, utaratibu wa kufungua mashauri mahakamani, na namna wanavyoweza
kupata msaada wa kisheria bila gharama.
Huduma ya utoaji elimu ya Mahakama kwa wananchi imekuwa kivutio kikubwa katika maonesho hayo, ambapo wananchi mbalimbali wamejitokeza kwa wingi kutembelea banda la Mahakama, kusikiliza mada mbalimbali kuhusu haki, wajibu wa raia, taratibu za uendeshaji wa mashauri, njia mbadala za utatuzi wa migogoro na masuala ya upatikanaji wa haki kwa wote.
Miongoni mwa Viongozi wa
Mahakama waliohudhuria na kushiriki kikamilifu kutoa elimu kwa wananchi ni Naibu
Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Mhe. Pamela Mazengo, Hakimu Mkazi
Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Tabora, Mhe. Shaibu Mzandah, Hakimu Mkazi
Mwandamizi, Mhe. Paulina Mkaubya pamoja na Maafisa Waandamizi wa Mahakama
wakiwemo Afisa Utumishi Mwandamizi, Bw. Amani Mtinangi na Msaidizi wa
Kumbukumbu, Bi. Miriam Ntenya.
Huduma ya Mahakama Inayotembea katika maonesho ya Nanenane ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania unaolenga kuboresha huduma, kuongeza uwazi, na kujenga imani kwa wananchi.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Mhe. Pamela Mazengo (kulia) akitoa elimu ya kisheria kwa wananchi waliotembelea banda la Mahakama katika viwanja vya Nanenane jana tarehe 08 Agosti, 2025- Manispaa ya Tabora.
Mgeni Rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma,Balozi Mhe. Saimon Sirro (wa pili kushoto) akipokea maelezo kutoka kwa viongozi wa mojawapo ya mabanda ya wadau walioshiriki maonesho ya Nanenane mkoani Tabora.
Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mhe. Paulina Mkaubya (kushoto) akitoa ufafanuzi kwa mwananchi kuhusu umuhimu wa kuzingatia taratibu za kisheria katika kudai haki zao.
Mzazi (wa pili kushoto) aliyefika na Watoto wake kwenye Maonesho ya Wakulima Nanenane Tabora kwa ajili ya kujifunza kuhusu huduma na taratibu mbalimbali za Mahakama.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni