Jumamosi, 9 Agosti 2025

JAJI MKUU ATUMA SALAMU KWA WATUMISHI WA MAHAKAMA KANDA YA DAR ES SALAAM

  • Wahimizwa na kuaswa kutekeleza majukumu yao kwa Uadilifu 

Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Dar es Salaam

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju amewataka  watumishi  wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu.

Agizo hilo lilitolewa tarehe 07 Agosti, 2025 katika ukumbi wa Mahakama Kuu Dar es salaam kupitia Mwenyekiti wa Jopo la Majaji wa Mahakama ya Rufani waliomaliza vikao vya Mahakama hiyo walivyokuwa wakiendesha katika Kanda hiyo.

Akitoa ujumbe huo, Mhe Lila alisema kuwa, Jaji Mkuu, Mhe. Masaju alielekeza Wenyeviti wote wa majopo ya Mahakama ya Rufani kupitia kwa Mhe. Augustino Mwarija (dean JR1), kufanya vikao na Majaji, Maofisa wa Mahakama (Judicial Officers) na watumishi wengine wa Kanda za Moshi, Dar es Salaam, Arusha na Mbeya wa kuwahimiza na kuwaasa kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu kwa mujibu wa Katiba na Sheria ipasavyo na kuzungumza nao kuhusu changamoto zozote za kiutendaji. 

Mhe. Lila alisema, wao kama Majaji wa Mahakama ya Rufani hawana mamlaka ya kuitisha vikao hivyo isipokuwa wamepewa mamlaka hayo na Jaji Mkuu kwa kuwa wao hawafanyi kazi za utawala.

Mhe. lila aliwataka watumishi hao ambao ni wawakilishi wa watumishi wengine kubainisha changamoto zote wanazokabiliana nazo katika utendaji kazi wao ili kuboresha utendaji kazi. 

Lakini pia aliwakumbusha watumishi hao kuwa, wao ni watumishi wa Mahakama na wala sio Taasisi nyingine na namna mtumishi wa Mhimili huo anavyopaswa kuwa.

Akinukuu hotuba ya Baba wa Taifa, Hayati Julius Kambarage Nyerere aliyoitoa katika ufunguzi wa Mkutano wa Majaji Arusha mwaka 1981 alisema kwamba, “zipo kazi zinazoweza kufanywa na watu tunaowatilia mashaka, lakini uhakimu na ujaji sio mojawapo ya kazi hizo. Jaji au Hakimu akitiliwa mashaka hata kama ushahidi hautoshi ni lazima aanze kuchunguzwa mara moja.”

Akifafanua ujumbe huo, Mhe. Lila alisema baada ya kupata ujumbe huo ilibidi afanye utafiti na kujua maana  halisi ya uadilifu na kusema kwamba Uadilifu una sifa ya kuwa mkweli, muaminifu na kuwa na misingi imara ya maadili yanayohusisha ukweli kwa maana kusema ukweli na kuwa wazi katika maneno na matendo.

Aliongeza kuwa, maadili yanahusisha kuzingatia misingi na thamani za maadili na msimamo thabiti ni kutenda kulingana na maadili na kanuni za mtu lakini pia uwajibikaji kwa matendo ya mtu mwenyewe.

Aidha, Mhe. Lila alisema uadilifu ni muhimu sana katika mazingira ya kibinafsi na ya kikazi, kwani hujenga uaminifu, kuaminika na heshima na kwamba watu wenye uadilifu huaminika, huwa waadilifu na wawazi katika shughuli zao.

Alisema, jukumu la Mahakama ni kutenda haki, hivyo, mtu anapofika mahakamani anajua anaenda kutendewa haki, na kwakuwa watumishi wa Mahakama wana dini, Mhe. Lila alisema, “hata vitabu vyetu vitakatifu Biblia na hata Quran zinasema hukumuni kwa haki na maamuzi yenu yatakuwa ya Mungu.”

Alisisitiza zaidi kuwa, vitabu hivyo vinaonya kuwa ole wao wabadilishao haki kuwa batili na batili kua haki. Amesema katika utoaji uamuzi unapaswa kuangalia sheria na ushahidi tu na si vinginevyo kwa kuwa sheria inachoongoza ndio hicho tunafanya hata kama jamii itaongea vinginevyo.

Aliwakumbusha pia kuwa, Mahakama ni chombo huru cha kufanya maamuzi bila kuingiliwa, hivyo, anayefanya kazi kwa uhuru dhidi ya wenye kesi kuwa karibu na wenye kesi  hizo taratibu haziruhusu. “Hakimu au jaji hapaswi kupata maelekezo kutoka kwa mtu mwingine lakini pia kuwa huru kutoka kwa jamii, usiogope jamii kuamua kwamba jamii itakuonaje,” alisisitiza Jaji Lila.

Kikao hicho kililenga pia kwa ajili ya kuangalia mapungufu yaliyopo na kujitathmini ili kuondoa mashaka kwenye jamii inayoizunguka Mahakama na kuondoa malalamiko dhidi ya Mhimili huo.

Naye, Mwenyekiti wa Jopo B la Majaji wa Rufani, Mhe. Dkt. Gerald Ndika alisema, “sote hapa ni kada mbalimbali lakini ni watumishi wa Mahakama tumepewa jukumu la kimungu la kuhukumu.”

Akizungumza kwa mfano, Mhe. Ndika alisema hata kama ni Mhasibu au Mlinzi wote wanaunganishwa na jukumu la kutoa haki na hivyo aliwataka watumishi wa Kada zote kutambua nafasi zao kuwa wana jukumu la kumsaidia Jaji Mkuu kufikia maono.

“Tunafanya kikao hiki pamoja na mambo mengine kutambua nafasi zetu kwamba sisi sote tunamsaidia Mhe. Jaji Mkuu, yeye ndiye anatuongoza lakini tunamsaidia kufikia lengo ndio utume wetu tunaoufanya,” alisema Jaji Ndika.

Katika kikao hicho changamoto mbalimbali zilibainishwa ikiwa ni pamoja na masuala ya maslahi ya watumishi pamoja na upandishwaji wa madaraja, kutokuwepo kwa semina elekezi pindi kunapotokea mabadiliko katika utendaji kazi kama kuhama mfumo mmoja kwenda mfumo mwingine lakini pia katika kazi hizo hizo kukumbushwa kwa mafunzo na changamoto ya upataji nafasi ya udhamini wa masomo.

Changamoto nyingine iliyotajwa ni watumishi ambao ni Wasaidizi wa Kumbukumbu na Waandishi Waendesha Ofisi wamekuwa na vyama vyao ambavyo kila mwaka wanakutana na kufanya kikao pamoja na mafunzo lakini kwa upande wa Mahakama hawapelekwi, hivyo wameomba wapelekwe wote kama Taasisi nyingine zinavyofanya.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Majaji wa Mahakama Kuu, Divisheni zote  na Mahakimu ambao waliwawakilisha watumishi wa Kada zote za Mahakama Kanda ya Dar es Salaam.



 Watumishi wa Mahakama Kanda ya Dar es Salaam wakifuatilia kikao cha pamoja na Majaji wa Mahakama ya Rufani.

Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Shaban Lila (katikati) akimsikiliza Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi akitoa neno la ukaribisho kwa Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt Gerald Ndika  (kushoto).

 Baadhi ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Dar es Salaam wakimsikiliza Mwenyekiti wa Jopo la Majaji wa Rufani, Mhe. Shaban Lila ( hayupo katika picha) alipokuwa akiongoza kikao na watumishi wa Mahakama Dar es Salaam.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 


 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni