Alhamisi, 7 Agosti 2025

KITUO JUMUISHI TEMEKE, TAASISI ZA FEDHA WAJADILI MAREKEBISHO YA KANUNI ZA MIRATHI

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama

Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke jana tarehe 6 Agosti, 2025 kilikutana na Wawakilishi wa Mabenki Mkoa wa Dar es salaam kujadili na kupata uelewa wa pamoja kuhusu marekebisho ya kanuni yaliyofanywa na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania kwa Msimamizi wa Mirathi kufungua akaunti moja maalum ya kuhifadhi fedha za marehemu wakati wa usikilizaji wa mashauri ya mirathi.

Kutokana na marekebisho hayo, fedha za mirathi zitakuwa zinawekwa katika akaunti maalum inayoitwa ‘Special Mirathi Account’ badala ya kuwekwa katika akaunti ya mirathi ya Mahakama kwa utaratibu wa awali.

Msimamizi wa Mirathi atafungua akaunti hiyo itakayopokea fedha za mirathi za kutoka Taasisi mbalimbali za fedha badala ya fedha hizo kuwekwa katika akaunti ya mirathi mahakamani.

Akizungumza wakati anafungua majadiliano hayo, Jaji Mfawidhi, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa aliwaeleza Wadau hao kuwa kabla ya marekebisho ya Kanuni za Mirathi, kupitia Tangazo la serikali Na 429 la 2025, fedha za mirathi kutoka Taasisi za fedha zilikuwa zikiwekwa katika akaunti moja ya Mahakama inayoitwa ‘Judiciary Mirathi Account.’

Alieleza kuwa kufuatia marekebisho hayo wameona ni vema wakakutana na Wadau hao muhimu wa Mahakama hiyo ili kujadiliana na kuwa na uelewa wa pamoja namna ya utekelezaji, kwani kwa sasa takwa la kisheria kwa Msimamizi wa Mirathi ni kufungua akaunti maalum inayoitwa ‘Special Mirathi Account’ katika benki yoyote atakayoona inafaa kwa ajili ya kuhifadhi fedha za marehemu zitakazotoka katika taasisi nyingine za fedha, ikiwemo mabenki.

Jaji Mfawidhi alisema kuwa maoni ya Wadau hao ni muhimu kwa sababu yatasaidia kuweka utaratibu ambao ni sahihi ili mnufaika asiweze kupata changamoto yoyote na pia itasaidia kuondoa tofauti kati ya Taasisi moja na nyingine au benki moja na nyingine wakati wa utekelezaji wa marekebisho ya kanuni hizo.

‘Leo hii Mwenyezi Mungu ametujalia tupo hai, lakini hatuwezi kujua kesho tutakuwa hatupo. Kwa hiyo, tukiweka mifumo thabiti itatusaidia. Tukiondoka lazima tutaacha mali na moja ya mali ni fedha kwenye akaunti zetu ndani ya mabenki mbambali. Jambo la kujiuliza ni kwamba usimamizi wa hizo fedha utakuwaje ili wanufaika wazipate,’ alisema.

Alibainisha kuwa hapo awali mtu akifariki na kuteuliwa Msimamizi wa Mirathi, Msajili wa Mahakama Kuu au Hakimu Mfawidhi katika Mahakama ya Wilaya na Mahakama ya Mwanzo walikuwa wanaandika barua kuomba kufunga akaunti na fedha katika mabenki kuhamishwa kwenda katika akaunti ya Mahakama.

‘Lakini, kutokana na mabadiliko ya Kanuni za Mirathi, kupitia Tangazo la Serikali Na 429 la 2025, kwa sasa fedha hizo zitakuwa hazipelekwi tena katika akaunti hiyo ya Mahakama. Msimamizi wa Mirathi anatakiwa kufungua akaunti moja maalum ya mirathi itakayopokea fedha toka taasisi nyingine kama mabenki mbalimbali, hata kama marehemu atakuwa na akaunti zaidi ya moja kwenye benki tofauti,’ Mhe. Mnyukwa alisema.

Jaji Mfawidhi aliwaeleza Wadau hao kuwa walikuwa wanakutana na changamoto nyingi wakati wa kuendesha akaunti moja ya Judiciary Mirathi Account, ikiwemo kutokujua mapema fedha zilizoingizwa zinatoka kwa marehemu yupi.

‘Ukimwandikia barua Msimamizi wa Mirathi kufunga akaunti ya fedha za marehemu kwenye mabenki, fedha zinaweza kuingia kwenye akaunti yetu, lakini kwa haraka tunaweza tusigundue ni za marehemu yupi...

‘Mkumbuke tunahudumia wakazi wote wa Mkoa wa Dar es Salaam, tuna Mahakama za Mwanzo, Mahakama za Wilaya na Mahakama Kuu na kwa siku moja zinaweza kutoka amri zaidi ya kumi na fedha zinaingia kwenye kapu moja,’ Mhe. Mnyukwa aliwaeleza Wadau hao.

Wakati wa majadiliano hayo, Kituo Jumuishi kilijadiliana na Wadau kwa kina ili kupata uelewa wa pamoja wa namna ya ufunguaji wa akaunti husika kwa kila marehemu anaefunguliwa maombi ya mirathi, usalama wa fedha za mirathi hiyo na namna ya kukabiliana na changamoto zinazoweza jitokeza katika utaratibu huo mpya.

Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa [juu na chini] akizungumza wakati anafungua majadiliano na Wawakilishi wa Mabenki Mkoa wa Dar es Salaam kujadili na kupata uelewa wa pamoja kuhusu marekebisho ya kanuni kwa Msimamizi wa Mirathi kufungua akaunti moja ya kuhifadhi fedha za marehemu wakati wa usikilizaji wa mashauri ya mirathi.


Wawakilishi wa Mabenki Mkoa wa Dar es Salaam [juu na chini] wakimsikiliza Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa wakati wa majadiliano hayo.


Picha na Bakari Mtaullah-Dar es Salaam

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni