Na. Innocent Kansha, Mahakama
Watumishi
wapatao 59 wakiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Musoma Mhe. Fahamu Mtulya walifanya ziara ya kutembelea Jengo la Makao Makuu ya
Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma ili kujionea uzuri wa jengo hilo ambalo ni
la sita Dunia kwa majengo ya kimahakama.
Katika
ziara hiyo ya kimafunzo iliyofanyika tarehe 10 Agosti, 2025 ilitanguliwa na
ziara ya watumishi hao iliyofanyika Zanzibar mnamo tarehe 8 Agosti, 2025, kisha
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es salaam na kuhitimisha katika jengo la
Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Watumishi
hao walipata wasaa wa kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo historia ya Mahakama
namna ya uendeshaji wa shughuli mbalimbali za Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu Masijala
Kuu na zile za Makao Makuu ya Mahakama.
Aidha,
watumishi walipata wasaa wa kuona na kujifunza shughuli mbalimbali zinazofanyika
katika chumba cha mifumo ya kutolea taarifa muhimu za Mahakama (Judiciary
Situation Room). Taarifa mbalimbali za Mahakama ambazo husaidia moja kwa moja
mipango na mikakati ya namna bora ya kuboresha huduma kwa wananchi katika
mchakato wa upatikanaji haki kwa ujumla.
Chumba
hicho maalumu kinahusika kitaalumu kuzalisha, kuchambua, kuchakata, kusimamia
na kutoa taarifa mbalimbali maalumu kwa ajili ya kuonesha na kutoa taarifa ya
shughuli zinazoendelea moja kwa Mahakama zote nchini.
Vilevile,
chumba hicho kinasimamia kuendesha na kuhakikisha usalama na upatikanaji wa
mtandao wa Mahakama sambamba na ufuatiliaji wa miundombinu ya mawasiliano kwa
ajili ya usimamizi mzuri wa rasilimali za TEHEMA, alisema Afisa TEHAMA Bw.
Razaro Sanga.
Watumishi
hao walihitimisha ziara yao kwa kutembelea Kituo cha Huduma kwa Mteja cha
Mahakama ya Tanzania na kupokea maelezo ya jinsi kituo hicho kinavyotoa huduma
kwa wananchi kwa muda wa masaa 24 kwa siku saba za wiki na kuchakata taarifa
mbalimbali za wateja.
Kituo kinapokea taarifa mbalimbali ikiwemo malalamiko, pongezi, maswali mbalimbali ya huduma zinazotolewa mahakamani na hata nje ya Mahakama na kuzitolea ufafanuzi ili kumpa mwananchi au mdau uelewa mpana wa taratibu mbalimbali na njia sahihi za kufuata kutatua kero kwa wakati.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni