Jumatatu, 11 Agosti 2025

WANACHAMA WA TMJA KIGOMA WAKUMBUSHWA UENDESHAJI WA MASHAURI YA MIRATHI

Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, ambaye ni  Mlezi wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) wa Kanda hiyo, Mhe. Augustine Rwizile amewakumbusha Mahakimu kuhusu kanuni za uendeshaji na usimamizi wa mashauri ya mirathi katika Kanda hiyo.

Mhe. Rwizile alitoa rai hiyo wakati akiwasilisha mada tarehe 08 Agosti, 2025 katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, ambapo kiliwajumuisha waheshimiwa Majaji na Mahakimu wote wa Kanda hiyo.

“Nasisitiza kuwa kanuni za uendeshaji wa mirathi kupitia sheria mbalimbali za nchi pamoja na zile za kimataifa zizingatiwe ili kuweza kupata uelewa mzuri wa kusimamia mashauri ya mirathi katika Mahakama zetu, hii itapunguza mirathi nyingi ambazo hazifungwi kwa utaratibu wa sheria na kusababisha fedha nyingi kubaki katika akaunti ya Mahakama bila kutambulika ili zigawiwe kwa warithi husika,” alisema Mhe. Rwizile.

Aidha, Jaji Mfawidhi huyo aliwasisitiza Mahakimu hao kujiunga na Chama cha Ukarimu ambapo Majaji na Mahakimu wote Tanzania hujiunga na hufanya ukarimu wa kijamii, mwanachama  anapopatwa na jambo katika familia yake na kwamba chama husaidia kumuondolea unyonge mhanga pale anapofarijiwa na wanachama wote tena kwa haraka na kwa kujali tatizo lililomfika mhusika huyo. 

Naye, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa akiwasilisha mada katika kikao hicho alisema kuwa, “upokeaji, usimamizi na utunzaji wa vielelezo katika mashauri imekuwa ni changamoto hasa tunapoendelea na uboreshaji mkubwa wa uendeshaji wa mashauri kwa njia ya mtandao na usahihi wa vielelezo hivyo katika shauri husika ili visaidie katika kutoa uamuzi (hukumu), hili ni eneo muhimu sana katika kuiweka Mahakama katika utendaji mzuri usioacha shaka katika maamuzi yake mbalimbali.”

Mhe. Mbelwa alisema kuwa, sheria mbalimbali zimeelekeza kuhusu upokeaji na utunzaji wa vielelezo husika ambapo, zinataka kuzifuata ili kuhakikisha heshima ya Mahakama katika maamuzi yake ubaki salama na bila kuacha shaka katika kumsaidia Hakimu kufanya uamuzi wa shauri husika.

Kwa upande wake Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Buhigwe na Mwenyekiti wa Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Kanda ya Kigoma, Mhe. Venance Mwakitalu alitoa ripoti ya mwaka ya utendaji wa chama hicho sambamba na kuwatambulisha wanachama wapya waliojiunga utumishi mwaka huu na kuwasisitiza juu ya umuhimu wa kujiunga na chama hicho.

Aliwashukuru Majaji pamoja na wanachama wote wa Kanda ya Kigoma waliosafiri kutoka Mahakama za Wilaza zote sita ambazo ni Kigoma, Kibondo, Kasulu, Uvinza, Buhigwe na Kakonko kwa kuhudhuria na kushiriki vema katika mijadala ambayo iliendeshwa na mlezi wao Jaji Mfawidhi, Mhe. Rwizile pamoja na Majaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. John Nkwabi, Mhe. Projestus Kahyoza na Kamati Tendaji ya chama hicho.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile (katikati) akiwa katika picha ya pamoja ya na Mahakimu Wanachama wa Chama cha Mahakimu  na Majaji  Tanzania (TMJA) (waliosimama). Walioketi, wa pili kulia Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma,  Mhe. John Nkwabi, wa pili kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Projestus Kahyoza, wa kwanza kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa,  wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Buhigwe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mahakimu  na Majaji  Tanzania (TMJA),  Mhe. Venance  Mwakitalu.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile (katikati) akiwa katika picha ya pamoja ya na Mahakimu wapya na wanachama wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA). Walioketi, wa pili kulia Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma,  Mhe. John Nkwabi, wa pili kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Projestus Kahyoza, wa kwanza kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa,  wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Buhigwe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mahakimu  na Majaji  Tanzania (TMJA),  Mhe. Venance  Mwakitalu.


Sehemu ya wajumbe wa kikao cha Wanachama wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Kanda ya Kigoma wakifuatilia mada iliyokuwa ikitolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile (hayupo katika picha).

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahkama ya Wilaya Buhigwe na Mwenyekiti wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Kanda ya Kigoma,  Mhe. Venance Mwakitalu akitoa neno la ukaribisho kwa Majaji na Mahakimu wajumbe wa kikao hicho kilichofanyika tarehe 08 Agosti, 2025 kwenye ukumbi wa Mahakama Kuu Kigoma.


Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa akifafanua jambo wakati alipokuwa akiwasilisha mada kwa wajumbe wa kikao cha Wanachama wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Kanda ya Kigoma.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, ambaye ni  Mlezi wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile akisisitiza jambo wakati alipokuwa akiwasilisha mada kwa wajumbe wa kikao cha wanachama wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) Kanda ya Kigoma.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni