Na ARAPHA RUSHEKE –Mahakama, Dodoma
Jumla ya Watumishi 100
wa Mahakama Kanda ya Morogoro jana tarehe 10 Agosti, 2025 walitembelea jengo la
Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini
Dodoma ili kujifunza na kubadilishana uzoefu wa utendaji kazi na uboreshaji wa
huduma ya utoaji haki.
Watumishi hao waliambatana nabaadhi ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, akiwemo Jaji Mfawidhi, Mhe. Rose Ebrahimu. Baada ya kuwasili katika jengo hilo, watumishi hao walipata fursa ya kuona maeneo mbalimbali ya Makao Makuu ya Mahakama na kuona vitu mbalimbali vilivyomo katika jengo hilo.
Akizungumza mara baada ya kujionea mandhari mbalimbali ya jengo hilo, Mhe. Ebrahimu alisema, “Niliona ni fahari kwamba watumishi wote wa Morogoro waje kushuhudia sehemu hii na kupata moyo na ari ya kuijua na kuielezea historia ya Mahakama pamoja na mapinduzi makubwa ya uboreshaji uliofanyika.’’
Alisema pia kuwa ni vema watumishi pia wakafahamu tulipotoka, tupo wapi na tunakoelekea na kwanini tunatakiwa kufanya kazi kwa bidii na kwa uadilifu ili kuendana na kasi ya Mahakama kwa sasa ya Mahakama mtandao.
Jaji Mfawidhi alitoa rai kwa watumishi wengine kutembelea Makoa Makuu hayo ya Mahakama kwani kuna vitu vingi vya kujifunza na kufahamu kwa undani zaidi.
Naye Jaji wa Mahakama Kuu Morogoro, Mhe Aisha Ally Sinda alionesha kufurahishwa na mabadiriko hayo na ameshauri watumishi wengine kwenda kujionea nini kinaendelea katika Makao Makuu hayo ya Mahakama.
Ziara hiyo ililenga kujifunza kuhusu utekelezaji wa majukumu ya kimahakama, mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano-TEHAMA, uboreshaji mbalimbali wa huduma kwa wananchi pamoja na kubadilishana uzoefu katika utendaji kazi wa kila siku.
Baada ya ziara yao, watumishi hao walionesha kufurahishwa na uboreshaji wa miundombinu ya Mahakama na kuipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa kufanikisha kazi hiyo.
Waliahidi kutumia maarifa waliyoyapata kuboresha huduma kwa wananchi wa Morogoro kupitia Mahakama zao.
Jaji Mfawidhi
wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Rose Ebrahimu akiongea
jambo wakati wa ziara hiyo.
Watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro wakiwa katika picha ya pamoja.
Jaji Mfawidhi
wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Rose Ebrahimu (wa kwanza
kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro
Mhe Aisha Ally Sinda walipotembelea Makao Mkuu ya Mahakama Dodoma.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni