Na ASHA JUMA-Mahakama, Morogoro.
Watumishi wa
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam hivi karibuni walifanya
ziara ya utalii wa ndani kwa kutembelea Mbuga ya Wanyama Mikumi pamoja na
kupanda milima ya Uluguru mkoani hapa.
Ziara hiyo iliyoongozwa na Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi, Mhe. Franck Kiswaga na Mtendaji, Bi. Athanasia Kabuyanja, ilikuwa
sehemu ya kujifunza kuhusu haki na ustawi wa wanyama pamoja na kuimarisha afya
kupitia mazoezi ya kupanda milima.
Kadhalika, ziara
hiyo ilifanyika kwa lengo la kuhamasisha utalii wa ndani, kuongeza uelewa wa
watumishi kuhusu umuhimu wa kulinda mazingira na viumbe hai, sambamba na kukuza
mshikamano miongoni mwao.
Aidha, ziara hiyo
iliwapa fursa ya kujifunza kwa karibu kuhusu haki za wanyama, sheria
zinazowalinda na wajibu wa kila mmoja katika kulinda bioanuai ya Taifa. Akizungumza
mara baada ya ziara hiyo, mmoja wa watumishi alisema:
"Tumepata
kujifunza jinsi wanyama wanavyolindwa kisheria na changamoto wanazokutana nazo.
Hii ni elimu muhimu kwa watumishi wa Mahakama kwa kuwa tuna wajibu wa
kuhakikisha haki inatendeka kwa viumbe vyote."
Wakiwa katika
mbuga hiyo, watumeshi hao wa Mahakama walifanikiwa kuwaona Wanyama mbalimbali,
wakiwemo Swala, Pundamilia, Tembo, Twiga na wengine wengi.
Kupitia kupanda
milima ya Uluguru, watumishi hao walijijengea afya, kuimarisha ushirikiano na
kuondoa msongo wa mawazo, hatua ambayo inasaidia kuongeza ufanisi kazini.
Ziara kama hiyo imeelezwa kuwa chachu ya kuhamasisha watumishi wa umma kuthamini vivutio vya ndani na kuchangia maendeleo ya sekta ya utalii nchini.
Sehemu ya Wanyama [juu na picha mbili chini] walioonekana wakati wa ziara hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni