Jumapili, 24 Agosti 2025

MAHAKIMU, WASAIDIZI WA SHERIA WA MAHAKAMA ZA KINONDONI KIGAMBONI, TEMEKE WAPIGWA MSASA

Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Dar es Salaam

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Arnold Kirekiano amewataka Wasaidizi wa Sheria wa Majaji pamoja na Mahakimu kujifunza mara kwa mara na kufanya tafiti mbalimbali za kisheria kabla ya kutoa uamuzi.

Mhe. Kirekiano aliyasema hayo jana tarehe 22 Agosti, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Kinondoni wakati wa mafunzo kwa Wasaidizi wa Sheria wa Majaji na Mahakimu kuhusu utafiti wa kisheria.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mhe. Kirekiano alisema mafunzo hayo yanafanyika kutokana na andiko (Legal Research Manual) la Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) na yanalenga kushirikishana elimu hususani utafiti wa kisheria na katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku iwe uandishi wa hukumu.

Jaji Kirekiano alisema kuwa, katika siku za hivi karibuni alipata fursa ya kushiriki mafunzo ya utafiti wa kisheria kama mshiriki mwezeshaji (ToT) pamoja na baadhi ya Wasaidizi wa Sheria wawili ambao walishiriki pia katika kwa nyakati tofauti mafunzo hayo yaliyowezeshwa na IJA kuanzia tarehe 04 hadi 06 Agosti, 2025. 

Mhe. Kirekiano alimshukuru Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi na alimshukuru pia Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. David Ngunyale ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mafunzo iliyoundwa Jaji Mfawidhi kwa kuona umuhimu wa kuweka utaratibu pale ambapo baadhi ya watumishi wanapata nafasi ya kujifunza jambo fulani na kuweka utaratibu wa kushirikishana na watu wengine ambao hawakupata nafasi hiyo.

"Kwa nia hiyo njema ya  Mhe. Jaji Mfawidhi ninaamini   kwamba wale ambao wamepata nafasi ya kushiriki katika mafunzo haya, pia wawe tayari kwenda kuwashirikisha na wengine,” alisema Jaji Kirekiano.

Aliongeza kwa kusema kwamba, “kesi inaweza kuwa ileile muktadha ukabadilika  hivyo kufanya uchunguzi ni muhimu zaidi.”

Kwa upande wake Msaidizi wa Sheria, Mhe. Claudia Tarimo akizungumza alipokuwa akifundisha Ustadi wa Utafiti wa Sheria alisema matumizi ya Mfumo Unaochapisha Maamuzi, Sheria na Kanuni mtandaoni (TanzLII) ni muhimu sana katika kufanya utafiti kwa kuwa inaonesha kama sheria husika imeanza au lini itaanza kutumika, inaonesha pia marekebisho yote yaliyofanyika katika sheria.

Mhe. Tarimo alisema kwa kutumia karatasi ngumu ni vigumu kutambua kama sheria inatumika au haitumiki.

Wakati huohuo, naye Msaidizi wa Sheria, Mhe. Sheila Biletwa aliwakumbusha washiriki hao kuhusu kuzingatia masuala ya maadili ya kitaaluma pamoja na namna ya kufanya nukuu ambapo alisema kwa kila tafiti zinazofanya lazima kusema umepata wapi kwa nani hiyo ndio nukuu  sahihi inayoepuka udanganyifu katika kazi ya utafiti, lakini pia uandishi mzuri wa hukumu ni ule unaofuata taratibu zilizowekwa na pia kumfanya msomaji avutiwe kusoma kazi hizo.

Mafunzo hayo yalifungwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Hussein Mushi ambapo aliwashukuru wawezeshaji na washiriki wote wa mafunzo hayo na kuwataka kuyafanyia kazi mafunzo hayo katika kazi zao za kila siku na kuchukua taahadhari zilizotolewa katika matumizi ya Akili Unde (AI).

Mhe. Mushi alisema mafunzo hayo yatawasaidia kuongeza ufanisi na usahihi wa kazi na pia matumizi yenye maadili ya taarifa na umuhimu wa kunukuu kwa usahihi jambo lililofundisha kuheshimu uadilifu, uwajibikaji na kutambua haki miliki za kitaalum katika kazi za kisheria ili kuepuka udanganyifu, lakini pia wamekumbushwa kuficha taarifa za wadaawa wanapoandaa hukumu au uamuzi kulingana na waraka wa Jaji Mkuu.

“Utafiti wa kisheria ni uti wa mgongo wa kazi ya Mahakama katika maandalizi ya hoja uchambuzi wa kisheria na utoaji maamuzi yenye mashiko, utafiti na uandishi ni vitu haviepukiki,” alisisitiza Naibu Msajili huyo.

Aliongeza kuwa, ujuzi na maarifa hayo wayatumie kwa bidii na kwa weledi katika kuongeza ubora wa kazi zao na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika utoaji wa haki kwa wananchi. 

Katika mafunzo hayo mada zilizofundishwa ni pamoja na Msingi hasa wa Sheria, kuongeza umahiri katika sheria, nyenzo na njia mbalimbali za kufanya utafiti wa kisheria lakini pia akili mnemba kama nyenzo ya kufanya utafiti wa kisheria, maadili na matumizi ya nukuu.

Mafunzo hayo ya siku moja yalifanyika baada ya baadhi ya watumishi kutoka nje ya vituo vya kazi kupata mafunzo na hivyo Kamati ya Mafunzo kuandaa mafunzo hayo ili kila mtu apate mafunzo hayo. 


 Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Arnold Kirekiano akifundisha mada wakati wa Mafunzo kwa Wasaidizi wa Sheria na Mahakama wa Kanda hiyo yaliyofanyika tarehe 22 Agosti, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Sehemu ya Washiriki wa Mafunzo ya utafiti wa kisheria wakifuatilia mafunzo hayo.

  Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Hussein Mushi akitoa neno la ukaribisho kwa mkufunzi na washiriki wa mafunzo ya utafiti wa kisheria yaliyotolewa tarehe 22 Agosti, 2025 kwa Mahakimu na Wasaidizi wa Sheria.


 Mhe. Sheila Biletwa akitoa mada katika mafunzo hayo.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Arnold Kirekiano (katikati), Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Hussein Mushi (kushoto) na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni- Dar es Salaam, Mhe. Is-haq Kuppa (kulia)  wakiwa katika picha ya pamoja na na Mahakimu wa Wilaya Kinondoni.

Meza kuu ikiongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Arnold Kirekiano (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na Wasaidizi wa Sheria walioshiri katika mafunzo hayo. Kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Hussein Mushi n kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni- Dar es Salaam, Mhe. Is-haq Kuppa.  

 Meza Kuu katika picha ya pamoja na Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo walioshiriki katika mafunzo hayo. Aliyeketi katikati ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Arnold Kirekiano,  Kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Hussein Mushi n kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni- Dar es Salaam, Mhe. Is-haq Kuppa.   

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 



 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni