Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma
Zaidi ya wananchi 50 walikusanyika katika viunga vya Mahakama
Kuu Kanda ya Kigoma kusikiliza hukumu ya Shauri la Jinai na. 5546 ya mwaka 2024
Jamhuri dhidi ya Athuman Francis Msabila na watumishi wenzake 10 walioshitakiwa
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma kwa makosa nane yaliyotendeka katika
ofisi ya umma.
Matumizi ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (TEHAMA) yametumika vema katika kuhakikisha wananchi wote wanapata
fursa sawa ya kusikiliza usomwaji wa hukumu hiyo huku wakiwa wameketi katika
viti vya kupumzikia wateja wanaposubiria huduma za kimahakama.
Akisoma hukumu hiyo tarehe 21 Agosti, 2025
kwenye ukumbi wa Mahakama ya wazi katika Jengo la Mahakama Kuu Kigoma, Hakimu
Mkazi Mwandamizi, Mhe. Misana Majula alitumia Mahakama Mtandao (Virtual Court)
ili wananchi waliokosa nafasi katika ukumbi wa wazi nao walipata fursa ya
kusikiliza kwa ufasaha hukumu iliyosomwa takribani saa 6 mahakamani hapo.
Aidha, Mhe. Majula, alibainisha kuwa
washitakiwa 11 walishtakiwa mahakamani hapo kwa makosa nane na upande wa
mashtaka uliweza kuthibitisha makosa mawili bila kuacha shaka katika kosa la
utakatishaji fedha za shilingi za Kitanzania milioni 463.5 na kosa la kugushi
nyaraka kati ya makosa nane waliyoshtakiwa nayo.
Aidha, Mahakama hiyo imewatia hatiani Mshtakiwa
nambari moja aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, Bw.
Athumani Francis Msabila na Mshtakiwa namba tano aliyekuwa Mhasibu wa
Halmashauri ya Manispaa Kigoma Ujiji, Bw. Salum Juma Said na kutoa adhabu ya
kifungo cha miaka 20 jela kwa kosa la utakatishaji fedha na la kugushi, ambapo
washtakiwa wote wanne (4), yaani namba moja, nne, tano na 10, ni aliyekuwa
Afisa Uchumi na Mipango, Bw. Frednand Filimbi na Afisa mipango Frank Nguvumali wamehukumiwa
kifungo cha miaka miwili Jela na adhabu zote zitakwenda kwa pamoja kwa washtakiwa
wawili wa kosa la kwanza.
Hakimu huyo aliendelea kubainisha akisoma hukumu
hiyo kuwa, Washtakiwa saba (7) kati ya 11 katika kesi hiyo, upande wa mashtaka
umeshindwa kuthibitisha kosa dhidi yao katika makosa yote nane, hivyo, Mahakama
hiyo imeshindwa kuwatia hatiani na imewaachia huru bila masharti yoyote na
majina ya washtakiwa hao ni Bw. Moses Zahuye,
Bw. Joel Shirima, Jema Mbilinyi, Kombe Kabichi na Bayaga Ntamasambilo
kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma.
Matumizi ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (TEHAMA) sasa ni dhahiri na ni nyenzo muhimu ndani ya Mahakama ya
Tanzania. Hatua hiyo inadhihirishwa na jitihada mbalimbali ambazo zinaendelea
kufanywa na Mahakama zote nchini ikiwemo Mahakama Kuu Kigoma kutumia teknolojia
katika kuwahudumia wananchi katika mashauri yote ya rufaa, maombi pamoja na
mashauri yenye mvuto wa kisiasa kwa wananchi.
Picha ya wananchi wakifuatilia kwa makini hukumu ikisomwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mhe. Misana Majula kwa njia ya Runinga iliyopo katika eneo la kusubiria huduma kwa wateja wanaofika mahakamani kupata huduma mbalimbali.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni