Ijumaa, 22 Agosti 2025

BALOZI WA IRELAND TANZANIA ATEMBELEA KITUO JUMUISHI TEMEKE

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama

Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Mhe. Nicola Brennan, jana tarehe 21 Agosti, 2025 alitembelea Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujifunza mambo ya kifamilia kuhusu ndoa, mirathi na watoto.

Mhe. Brennan aliwasili kwenye Kituo hicho majira ya saa tano asubuhi na kupokelewa na mwenyeji wake, Jaji Mfawidhi wa Kituo hicho, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa na Viongozi wengine wengine wa Mahakama.

Akiwa ameambatana na wafanyakazi 25 kutoka kwenye ubalozi huo, Mhe. Brennan alipitishwa katika maeneo mbalimbali kabla ya kupokea mada kadhaa kuhusu aina ya mashauri yanayosikilzwa kwenye Kituo, ikiwemo ndoa, talaka, mirathi na Watoto.

Akizungumza baada ya ziara yake, Balozi Brennan alionesha kufurahishwa jinsi Kituo hicho kinavyofanya kazi na kuelezea kama mmoja wa Wadau wa Mahakama ya Tanzania wanavyotoa mafunzo kwa Majaji na Mahakimu kwenye maeneo mbalimbali kupitia Taasisi yao inayoitwa ‘Irish Rule of Law,’ kwa kushirikiana na Chuo cha Uogozi wa Mahakama Lushoto.

‘Tumetembelea maeneo ya Kituo hiki, tumejionea facilities na huduma zinazotolewa hapa. Tumekutana na Mahakimu ambao wamewasilisha mada kwenye maeneo mbalimbali kuhusu mashauri yanayosikilizwa hapa kama mirathi na mashauri ya Watoto. Nimefurahishwa na Kituo hiki ambacho kinatoa haki kwa watu wengi na kiwango cha huduma zinazotolewa ni kubwa sana,’ alisema.

Alisema kuwa kupitia Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania wanafanya kazi na Wadau mbalimbali wa Mahakama kutoa ushauri wa kisheria bila gharama yoyote kwa wahanga ambao mashauri yao yanasikilizwa kwenye Kituo hicho.

Kwa upande wake, Mhe. Mnyukwa alieleza kuwa Mahakama hiyo inapokea mashauri takribani 700 kwa mwezi kwa Mahakama zote nne zilizopo kwenye Kituo hicho, yaani Mahakama ya Mwanzo, Mahakama ya Watoto, Mahakama ya Wilaya na Mahakama Kuu. Alisema ukuaji wa teknolojia katika usajili wa mashauri umechangia kuongezeka kwa idadi ya mashauri yanayofunguliwa katika Kituo hicho.

Naye Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania anayehudumu kwenye Kituo hicho, Mhe. Frank Moshi alisema kuwa tangu kuanzishwa kwake, Kituo kimekuwa kikihudumia idadi kubwa ya wateja wanaofika kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali zinazotolewa na Mahakama pamoja na Wadau wao.

Alisema tangu Kituo hicho kilipoanzishwa hadi Julai 31, 2025, kimehudumia jumla ya wateja 722,496, wakiwemo Wanawake 386,035, sawa na asilimia 53.4, Watoto 4,142, sawa na asilimia 0.57 huku wanaume wakiwa 332,319, sawa na asilimia 46.

Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Mhe. Nicola Brennan [kulia] akipokea zawadi kutoka kwa Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa. Picha chini wakisalimiana baada ya Balozi huyo kuwasili kwenye Kituo hicho. Anayeangalia pembeni kwenye picha ya chini ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania kwenye Kituo hicho, Mhe. Frank Moshi.



Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Mhe. Nicola Brennan [juu na chini] akipokea maelezo na uwasilishaji wa mada mbalimbali alipotembelea kwenye Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke.

Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Mhe. Nicola Brennan[juu na chini] akiwa katika picha za pamoja.

Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Mhe. Nicola Brennan [kushoto] akiagana na Mtendaji wa Mahakama Kuu kwenye Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Bw. Samson Mashala, huku Viongozi wengine wa Mahakama wakishuhudia.
Picha na BAKARI MTAULLAH-Dar es Salaam

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni