Jumapili, 14 Septemba 2025

TOENI HUDUMA YA UTETEZI WA HAKI KWA WATU WOTE BILA UBAGUZI; JAJI MKUU

Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma

Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju ametoa rai kwa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) kupigania haki za watu wote kwa usawa bila kubagua baadhi ya makundi kwa kuwa kila raia wa Kitanzania ni sawa na ana haki zinazotambulika kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mhe. Masaju alitoa rai hiyo tarehe 12 Septemba, 2025 alipokuwa akizungumza na Wanachama kutoka TAWLA waliomtembelea ofisini kwake Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Akitoa ufafanuzi kuhusu suala la usawa wa binadamu, Jaji Mkuu alinukuu Ibara ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inasema, ‘watu wote ni sawa mbele ya sheria na wanayo haki bila ubaguzi wowote kulindwa kupata haki sawa mbele ya sheria.” Hata waasisi wa Taifa letu walipokuwa wakiandaa nembo ya taifa, walizangatia usawa ndio maana kuna bibi na bwana na wote wawili ukiwaangalia kwenye nembo ile wanaonekana kushika rasilimali za taifa pasipo ubaguzi.

Mhe. Masaju alisema huku akirejea Ibara ndogo ya 4 ya Ibara ya 13 ya Katiba ambayo inasema, ‘ni marufuku kwa mtu yoyote kubaguliwa na mtu au mamlaka yoyote inayotekeleza madaraka yake chini ya sheria yoyote katika utekelezaji wa kazi au shughuli yoyote ya mamlaka hizo.’

Jaji Mkuu amenukuu, ‘Ibara ya 8 ya Katiba pamoja na mengine inazungumza jinsi Serikali inavyopatikana na lengo kuu la Serikali litakuwa ni ustawi wa wananchi na Serikali itawajibika kwa wananchi.’ Amesema wananchi wanaozungumziwa kwenye Ibara hiyo ni Raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao ni wanawake na wanaume na kwa tofauti za umri wao ambapo kuna wazee, watoto, wavulana na wasichana na kwamba hao wote ni watu ambao haki zao zinapaswa kuzingatiwa.

Mhe. Masaju aliongeza kuwa, ‘Ibara ya 9 pamoja na mengineyo inasema, mamlaka ya nchi na vyombo vyake vyote vinawajibika kuelekeza sera na shughuli zake zote katika lengo la kuhakikisha kuwa; a) Utu na haki nyinginezo zote za binadamu zinaheshimiwa na kuthaminiwa b) Sheria za nchi zinalindwa na kutekelezwa.’

Aidha, Jaji Mkuu aliitaka TAWLA kuainisha sheria na kanuni ambazo wanaona sio rafiki na zinazokiuka haki za binadamu ili ziwezwe kuwasilishwa kwa Watoa Uamuzi ili ziweze kufanyiwa kazi.

“Kama kuna sheria au kanuni ambazo sio rafiki au ni za kibaguzi kwa makundi mbalimbali ikiwemo wanawake, watoto mziainishe kwa sababu Mahakama ndio imepewa jukumu la kulinda haki,” alisema Jaji Mkuu.

Mhe. Masaju alieleza kwamba, Mahakama inatekeleza majukumu yake ipasavyo bila kujali aina ya mtu anayepewa huduma, hivyo  amesisitiza kwa kueleza kwamba, “kama kuna mambo yanafanyika mahakamani ambayo yanaathiri labda kutekelezwa kwa haki za wanawake au za watoto hayo yatakuwa ni madhaifu ya mhusika mmoja mmoja binafsi lakini sio msingi wa Mahakama.”

Alisisitiza kuwa, Mahakama haitafanya upendeleo wa aina yoyote kwa kundi lolote la watu bali itaendelea kutimiza majukumu yake ya utoaji haki kwa mujibu wa Katiba na Sheria za nchi.

“TAWLA mna mchango mkubwa wa kuishauri Mahakama, kwahiyo mnapokuja mahakamani, mnapaswa mjiandae vizuri kuishauri Mahakama ili kufikia maamuzi sahihi,” alisisitiza Jaji Mkuu.

Kadhalika, Mhe. Masaju alikipongeza chama hicho kwa kuendelea kutetea haki na kukitaka kuendelea kutoa elimu ya sheria kwa wananchi na kutetea zaidi haki za binadamu. Aliwashauri kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na vilevile Wizara nyingine katika kutekeleza malengo ya kuanzishwa kwa TAWLA kwa ustawi wa Watanzania.

Akisoma taarifa mbele ya Jaji Mkuu kuhusu Chama hicho, naye Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), Bi. Tike Mwambipile aliipongeza Mahakama ya Tanzania kwa uboreshaji wa huduma za kiutendaji ikiwa ni pamoja na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), maboresho ya Kanuni na Sheria, Uboreshaji wa Miundombinu, Usuluhishi wa migogoro na kuondoa Mahabusu wa Mahakama za Mwanzo Magerezani.

“Tunachukua fursa hii kuipongeza Mahakama kwa hatua kubwa zilizochukuliwa katika maboresho ya kiutendaji, imefanya maboresho makubwa katika matumizi ya teknolojia, usikilizwaji wa mashauri ya njia ya video/mtandao hatua ambayo imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza malalamiko ya wananchi na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kimahakama,” alisema Bi. Tike.

Hata hivyo, Mkurugenzi huyo alitaja baadhi ya changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni pamoja na utekelezaji wa mashauri yaliyoamriwa na Mahakama kutoheshimika ambapo amesema, “kuna baadhi ya kesi ambazo maamuzi ya Mahakama hayaheshimiwi na kutekelezwa kwa wakati jambo ambalo linaweza kuathiri imani ya umma kwa mfumo wa haki na kupunguza ufanisi wa vyombo vya utoaji haki.

Bi. Tike alieleza kuwa, changamoto nyingine wanayokabiliana nayo ni katika Mfumo wa Kielektroniki wa Ufunguaji wa mashauri (e-filling) hususani kwenye mashauri ya mirathi hasa kwa wateja wao wa msaada wa kisheria, ukatili dhidi ya wanawake na Watoto, unyang’anyaji wa mali za wanawake na wazee hususani vijijini.

“Tozo kwenye Mabaraza ya Ardhi kwa wateja wa msaada wa kisheria, hii ni changamoto nyingine, tunaomba ushirikiano wako ili kuangalia namna ya kuondoa tozo hizi kwa wateja wanaopata msaada wa kisheria na kama inawezekana wajumuishwe kwenye orodha ya wanaosamehewa ada za Mahakama,” alisema Mkurugenzi huyo.

Kadhalika, Chama hicho kimeiomba Mahakama kukisaidia kupata vitendea kazi kama kompyuta na vinginevyo katika baadhi ya Ofisi zake na katika Madawati ya Msaada wa Kisheria ambayo yapo katika baadhi ya Mahakama.

Mara baada ya kupokea taarifa hiyo, Jaji Mkuu alikiri kupokea pongezi na changamoto zilizowasilishwa na kuwataka kuandaa taarifa ambayo itajumuisha yote waliyowasilisha na kuzungumza ili Mahakama ione namna ya kuyafanyia kazi.

Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) ni shirika lisilokuwa la kiserikali (NGO) lililoanzishwa mwaka 1989 kwa lengo la kutetea na kuendeleza haki za kisheria na kikatiba za wanawake. Dira ya TAWLA ni kuhamasisha jamii, kulinda na kutetea haki za wanawake.


Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju akizungumza na Wanachama wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) (hawapo katika picha) walipomtembelea Jaji Mkuu ofisini kwake Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (aliyeketi mbele) akizungumza na Wanachama wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania waliomtembelea tarehe 12 Septemba, 2025 ofisini kwake Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Mazungumzo yakiendelea...

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), Bi. Tike Mwambipile akizungumza jambo walipomtembelea Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania tarehe 12 Septemba, 2025 ofisini kwake Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.


Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), Bi. Tike Mwambipile mara baada ya mazungumzo.

Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Viongozi wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) tarehe 12 Septemba, 2025 walipomtembelea ofisini kwake Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

(Picha na MARY GWERA, Mahakama)













 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni