Na Dillon Uisso-Mahakama, Dar es Salaam
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA) imeendesha semina ya elimu ya Sheria ya Bima kwa Mahakimu wa Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama za Wilaya Mkoa wa Dar es Salaam ili kuwajengea uelewa mpana kuhusu masuala ya bima na kuongeza ufanisi katika kushughulikia mashauri yanayohusiana na sekta hiyo.
Semina hiyo ambayo ilifanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya King Jada ilihudhuriwa pia na Watendaji wa Mahakama na watumishi wa Mamlaka ya bima na Wadau wa bima. Kupia semina hiyo, TIRA imelenga kuimarisha ushirikiano na Mhimili wa Mahakama ili kuhakikisha utekelezaji wa sheria za bima unafanyika kwa ufanisi, uwazi na kwa manufaa ya wananchi.
Akifungua semina hiyo, Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Awamu Mbagwa aliwashukuru TIRA kwa jitihada hizo kubwa kuhakikisha Mahakimu wanapata elimu ya bima ambayo ni muhimu katika shughuli zao za kushughulikia masuala ya bima kwa kuzingatia kuwa bima inamhusu mtu mmoja na Taasisi.
Mhe. Mbagwa aliwapongeza Wadau mbalimbali wa Mahakama kwa kuweza kushiriki katika semina hiyo muhimu ili waweze kujenga uelewa zaidi katika sheria za bima na hivyo kusaidia katika kutafsiri sheria wakati wa usikilizaji wa mashauri hayo na utoaji haki.
Alibainisha kwa elimu ya bima siyo tu muhimu katika usikilizaji wa mashauri na utoaji wa haki lakini pia imekuwa nyenzo muhimu ya kulinda maisha na mali ya mtu binafsi, familia, Taasisi na nchi kwa ujumla.
Kaimu Jaji Mfawidhi alitoa shukrani kwa TIRA kwa kushirikiana na Mahakama katika kutimiza lengo hilo kwa kuongeza maarifa kwa maofisa kutoka Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama za Wilaya katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Alisema kuwa huo ni mwendelezo wa elimu na ushirikiano kati Mahakama na Taasisi nyingine za umma katika kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unapata elimu na uelewa zaidi wa sekta mbalimbali kwa ajili ya kuwahudumia wananchi kwa weledi, haki na ufanisi.
Naye Kamishna wa Bima nchini, Dkt. Baghayo Saqware, alitoa shukurni za kipekee kwa uongozi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kwa kuhakikisha semina hiyo inafanyika.
Baada ya ufunguzi huo, mada mbalimabali za bima ziliwasilishwa na wawezeshaji waliobobea kwenye sekta hiyo.
Picha ya pamoja ya meza kuu.
Picha za pamoja za washiriki-juu na chini.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Geita.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni