Na ARAPHA RUSHEKE-Mahakama Kuu, Dodoma.
Watumishi wa Mahakama katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma (IJC) wamepata mafunzo maalumu ya huduma ya kwanza (first aid) kutoka Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA), ikiwa ni hatua ya kuimarisha usalama na ustawi wa watumishi pamoja na wananchi wanaohudumiwa mahakamani.
Mafunzo hayo
yaliyofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa IJC yalijikita katika kuwajengea
uwezo washiriki namna ya kutoa huduma ya dharura kwa majeruhi au mgonjwa kabla
ya kupata huduma ya kitabibu.
Aidha, mafunzo hayo yalihusisha
pia masuala ya nadharia na vitendo ikiwa ni pamoja na mbinu za kuziba damu,
kutumia vifaa vya huduma ya kwanza na namna ya kumudu dharura mbalimbali
zinazoweza kujitokeza maeneo ya kazi.
Akizungumza wakati wa
mafunzo hayo, mwezeshaji kutoka OSHA, Bi. Moteswa Meda alisisitiza umuhimu wa
kila Taasisi kuhakikisha ina watumishi wenye ujuzi wa huduma ya kwanza.
Alibainisha kuwa Mahakama
hupokea wananchi wengi kila siku, hivyo uwepo wa watumishi wenye maarifa ya
msingi ya huduma ya kwanza ni nyenzo muhimu ya kuokoa maisha.
“Ni muhimu kuhakikisha
tunafahamu njia salama za kumhudumia mtu pale ambapo anapata matatizo akiwa
sehemu ya kazi, kwani kila mtumishi mwenye ujuzi wa huduma ya kwanza ni ngao ya
usalama kazini,” alisema Mkufunzi huyo.
Vilevile aliendelea
kusisitiza kwa kusema kuwa “Huduma ya kwanza si chaguo, ni hitaji la msingi
mtumishi anayejua kutoa huduma ya kwanza anaweza kuokoa maisha, kupunguza
madhara na kulinda utu wa binadamu kabla ya msaada wa kitabibu kufika,” alisema
Bi. Moteswa.
Kwa upande wao,
washiriki wa mafunzo walieleza kufurahishwa na elimu waliyoipata na kuahidi
kutumia ujuzi huo kuimarisha usalama kazini. Waliongeza kuwa mafunzo hayo
yatasaidia kupunguza madhara ya ajali ndogo ndogo na kuboresha mazingira ya
utoaji wa huduma ndani ya Mahakama.
Mafunzo kama hayo yamekuwa yakitekelezwa katika Taasisi mbalimbali nchini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa OSHA kuhakikisha kuwa wafanyakazi wote wanakuwa na uelewa kuhusu afya na usalama sehemu za kazi.
Watumishi wa Mahakama Dodoma wakifuatilia kwa makini mafunzo hayo.
Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma, Mhe. Zabibu Mpangule [wa kwanza kulia] akifuatilia kwa makini mafunzo hayo. Anayefuatia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Dodoma, Mhe. Thurstone Kombe.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Geita.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni