Jumamosi, 20 Septemba 2025

USHIRIKIANO KATI YA MAHAKAMA YA TANZANIA NA JESHI LA MAGEREZA WAZAA MATUNDA

·       Kamishna Mkuu wa Magereza asema umepunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya malalamiko ya Wafungwa, Mahabusu

·       Waipongeza Mahakama kwa kuondoa zaidi ya asilimia 80 ya changamoto zilizokuwa zikiwakabili Wafungwa na Mahabusu

·       Asema idadi ya Mahabusu yapungua na hakuna Mahabusu wa Mahakama za Mwanzo gerezani

·       Wapongeza matumizi ya Mahakama Mtandao ambapo zaidi ya mashauri 10,000 yamesikilizwa kwa njia hiyo

Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma

Kamishna Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini, (CGP) Jeremia Yorum Katungu ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa ushirikiano mkubwa inaoupatia Jeshi hilo ambao umewezesha kupatikana kwa mafanikio lukuki ikiwemo kupungua kwa idadi ya malalamiko ya Wafungwa na Mahabusu.

CGP Katungu alieleza hayo jana tarehe 19 Septemba, 2025 alipomtembelea Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju ofisini kwake Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma lengo likiwa ni kusalimiana na kujadiliana kuhusu masuala mbalimbali kwa ustawi wa utendaji kazi wa vyombo hivyo.

“Matokeo ya ushirikiano huu Mhe. Jaji Mkuu, kwanza magerezani kumekuwa na kupungua kwa malalamiko ya wafungwa na mahabusu kuhusiana na changamoto za mashauri, miaka ya nyuma ilikuwa ukiingia gerezani unaweza kusikiliza malalamiko kuanzia asubuhi mpaka jioni malalamiko yalikuwa mengi sana, lakini sasa hivi nikuhakikishie malalamiko sio kwamba tumeyamaliza yote lakini yamepungua kwa kiasi kikubwa sana na tafsiri yake ni kwamba ni ushirikiano uliopo katika utatuzi wa malalamiko hayo ambayo yamefanya wafungwa na mahabusu kuridhika na hivyo kusababisha utulivu gerezani,” alisema Kamishna Mkuu huyo wa Jeshi la Magereza.

CGP Katungu alishukuru kwa dhati ushirikiano huo ambao umekuwepo kati ya Mahakama pamoja na Jeshi la Magereza na kukiri kuwa, kumekuwa na ziara za mara kwa mara za Majaji na Mahakimu akiwemo Jaji Mkuu ambaye alifanya ziara yake ya kwanza katika Gereza la Isanga tarehe 10 Julai, 2025.  

Kamishna Mkuu huyo alikiri kwamba, ziara hizo zimekuwa na manufaa mengi ikiwemo ushughulikiaji wa mashauri ya wafungwa na mahabusu.

“Usikilizaji wa mashauri ya wafungwa na mahabusu kupitia Mahakama Mtandao ni eneo ambalo pia tumekuwa tukishirikiana vizuri, kama utakumbuka miezi kadhaa iliyopita mlitusaidia kutupa makasha 10 ambayo yanatumika kama vyumba vya Mahakama mtandao lakini pia mmeendelea kutusaidia vifaa vya TEHAMA ambavyo vinatumika kwenye Mahakama mtandao kwakweli tunashukuru katika eneo hilo na tumeendelea kuona ufanisi katika usikilizaji wa mashauri kupitia Mahakama mtandao,” alieleza CGP Katungu.

Kamishna Mkuu huyo wa Magereza alisema kwamba, kuanzia mwaka 2021 ndipo ulianza ushirikiano wa huduma ya wafungwa na mahabusu kusikiliza mashauri yao kwa njia ya Mahakama Mtandao ambapo kufikia Septemba, 2025 huduma ya Mahakama mtandao imeendelea kutolewa katika vituo 97 na mpango uliopo ni kuwa na huduma hiyo katika Magereza yote nchini.

“Katika kipindi cha mwaka 2021 mpaka sasa, zaidi ya mashauri 10,000 yamesikilizwa kwa njia ya huduma ya Mahakama Mtandao katika Vituo hivyo 97 na baadhi maamuzi yamefanyika kwa utaratibu wa Mahakama mtandao na hii kwakweli imekuwa na manufaa sana kuondokana na changamoto za ucheleweshaji wa mashauri,” alisema CGP Katungu.

Aliongeza huku akirejea maelekezo ya Jaji Mkuu alipofanya ziara katika Gereza la Isanga tarehe 10 Julai mwaka huu kuhusu kuondoa mahabusu wa Mahakama za Mwanzo gerezani kwamba maelekezo hayo yamefanikiwa kwa ufanisi mkubwa na sasa.

“Nikupongeze kwa dhati kabisa, maelekezo hayo yamefanikiwa kwa kiasi kikubwa, tumekuwa na mawasiliano ya karibu sana na watendaji  wako kuhusu suala hili na matokeo yanaonekana, sasa ulipokuja Gereza la Isanga kulikuwa na Mahabusu 6, 415 lakini kwa tarehe 18 Septemba, 2025 idadi ya mahabusu waliopo ni 4,658, utaona kuna idadi ya zaidi ya mahabusu 1,757 wamepungua na hayo ni matokeo ya ziara ambayo ulifanya na maelekezo uliyotupa ambayo utekelezaji wa maelekezo yako umeanza kuzaa matunda, na kitu cha kujivunia sana ni kwamba, tunavyozungumza sasa Mahabusu wa Mahakama za Mwanzo hatuna magerezani,” alieleza.

Aliongeza kuwa, Mahakama na Magereza inashirikiana pia ni katika eneo la kubadilishana taarifa ambapo alirejea maelekezo ya Jaji Mkuu alipofanya ziara katika Gereza la Isanga ambapo pamoja na mambo mengine aliomba kupatiwa taarifa za kila siku za idadi za Wafungwa na Mahabusu waliopo katika magereza mbalimbali nchini, amesema kazi hiyo wanaitekeleza kwa dhati kwa kuwa manufaa yake wameanza kuyaona ikiwemo kupungua kwa mashauri pengine hayakuwa na ulazima wa kukaa kwa muda mrefu.

“Lakini kuna kupungua kwa idadi ya waliopo gerezani hususani Mahabusu, Mhe. Jaji Mkuu nitoe tu takwimu kidogo ulifanya ziara tarehe 10 Julai, 2025, maelekezo uliotoa tunaendelea kuyatekeleza, lakini wakati unafanya ziara ile idadi ya wafungwa na mahabusu ilikuwa 25,784 lakini hadi kufikia tarehe 18 Julai mwaka huu idadi ilikuwa 24,761 kwahiyo idadi imepungua hususani ya mahabusu na kwamba Serikali imepunguza gharama kubwa ya kuwahudumia mahabusu na wafungwa,” alisema CGP Katungu.

Aidha, alizungumzia kuhusu changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni pamoja na vikao vya Mahakama Kuu kuchukua muda mrefu kufanyika, changamoto ya kupatikana kwa mtandao kwenye Mahakama mtandao, mahitaji ya vifaa vya TEHAMA,

“Magereza mengi hayana miundombinu inayowezesha urekebishaji wa wafungwa, kuna haja ya kuwa na viwanja vya michezo na burudani ndani ya viwanja vya Magereza, kuna haja pia ya kuwa na vyumba maalum vya kutumika kama madarasa. Kwahiyo sasa hivi magereza nyingi tunazojenga tunajitahidi kuweka miundombinu muhimu itakayowezesha urekebishaji,” alisema.

Kamishna Mkuu huyo alieleza kuwa, kuna changamoto ya baadhi ya Wilaya kukosa Magereza na kwamba lengo ni Wilaya zote ziwe na Magereza ili kurahisisha usafirishaji wa wafungwa na mahabusu. Ameongeza kwamba kwa sasa kuna ujenzi unaendelea wa jumla ya magereza 12.

Aliongeza kwamba vitendea kazi bado ni changamoto hasa magari, Serikali inaendelea kutoa fedha kwa ajili ya kununua magari na hivi karibuni wamepokea jumla ya magari 10 aina Land Cruiser pick up 10.

Naye, Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza kutoka Jeshi Magereza nchini (CP) Nicodemus Tenga alisema kuwa, kwa sasa Jeshi hilo lina Wanasheria zaidi ya 264 na wamesambazwa kwenye vituo mbalimbali vya Magereza ikiwemo Magereza ya mikoani na wilayani.

Aidha, CP Tenga ameishukuru Mahakama kwa kuwafundisha wanasheria hao jinsi ya kutumia Mfumo wa Kieletroniki wa Usimamizi wa Mashauri (e-CMS) na kuwezesha magereza zote nchini kutumia mfumo huo na kuondokana na matumizi ya karatasi na imesaidia kupungua zaidi ya asilimia 80 ya changamoto kufuatia matumizi ya mfumo.

Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Kamishna Mkuu wa Magereza nchini, naye Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju alimpongeza Kamishna huyo kwa kazi nzuri ambayo amekuwa akifanya ambayo matokeo yanaonekana.

“Niwapongeze kwa haya mambo makubwa ambayo mmekuwa mkiyafanya naona unayatekeleza kwa kiwango kikubwa sana licha ya changamoto, nashukuru sana kwa hii taarifa ambayo umetupatia ni taarifa ambayo imejitosheleza ambayo itatusaidia sisi kuboresha huduma         zetu ili kuhakikisha kwamba wajibu wetu katika utekelezaji wa haki jinai unatekelezwa kwa ufanisi ipasavyo,” alisema Mhe. Masaju.

Jaji Mkuu alisema kwamba, kuna umuhimu mkubwa wa kuwa ushirikiano na uhusiano mzuri baina ya Wadau wa Haki Jinai wakiwemo Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Jeshi la Polisi, TAKUKURU, Mamlaka ya Kupambana na Kuzuia Madawa ya Kulevya, Jeshi la Uhamiaji na wananchi ambalo lengo lake ni kupata na kuboresha utekelezaji wa majukumu kwa ufanisi kila sehemu ili lengo lililokusudiwa lifanikiwe.

Aidha, Mhe. Masaju amemtaka Kamishna huyo kuwa kama kuna changamoto zozote zinazohusu Mahakama ambazo zitaendelea kujitokeza asisite kuijulisha Mahakama na kwamba kwa sasa hatatembelea Magereza hadi atakapohakikisha kuwa changamoto zilizopokelewa wakati wa ziara yake katika Gereza la Isanga zifanyiwe kazi/ziishe.

“Nawashukuru kwa ushirikiano mkubwa ambao mmeendelea kutupatia hususani utoaji taarifa, na kwamba kuna taarifa au changamoto zaidi msisubiri tuwaombe nyie andikeni tuyafanyie kazi,” alisisitiza Jaji Mkuu.

Aidha, amewashauri Viongozi hao wa Jeshi la Magereza kushughulikia mapema mapema maombi ya wafungwa wanaosubiri msamaha wa Rais kwa sababu kuna Kamati mahsusi ya kumshauri Rais kuhusu msamaha kwa wafungwa wanaosubiri adhabu ya kifo kwa kufuata utaratibu husika, kwa sababu itasaidia kupungua idadi ya wafungwa.

Aidha, Mhe. Masaju amemuomba Kiongozi huyo wa Jeshi la Magereza kuandaa taarifa kuhusu utekelezaji wa Kifungu cha 134 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai, ili kujua kama kweli mashauri hayo yanamalizika ndani ya miezi sita.

“Tunatengeneza pia Kanuni ambazo zitawezesha katika mashauri yanayosikilizwa na Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama za Wilaya wao nao Mahakama na washtakiwa wawe nao sasa wanapata ushahidi wa upande wa kesi za mashtaka ili iwasaidie na wao kujitetea kwa ufanisi ipasavyo, haitoshi tu kwamba kumpa haki ya kusikilizwa lakini akiwa hana taarifa za tuhuma na ushahidi uliopo dhidi yake hapo hakutakuwa na haki ya kusikilizwa aliyopewa itakuwa imenyofolewa kwa kiasi fulani na itakuwa inakiuka Ibara ya 13 ya Katiba inayotaka usawa mbele ya sheria,” alisisitiza Jaji Mkuu.

Kadhalika, Mhe. Masaju alilipongeza Jeshi la Magereza kwa kazi kubwa ya urekebishaji wanaofanya na kulishauri Jeshi hilo kuangalia uwezekano wa kuwarudisha hadi mipakani wafungwa kutoka nchi za Jirani za Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao wanamaliza kutumikia mifungo vyao badala ya kuendelea kujaza idadi ya wafungwa magerezanina kuwa na wahamiaji haramu nchini.

Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (kulia) akizungumza jambo na Kamishna Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini (CGP), Jeremia Yoram Katungu alipotembelewa na Mkuu huyo wa Jeshi la Magereza ofisini kwake Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (aliyeketi mbele) akizungumza na ujumbe kutoka Jeshi la Magereza nchini ulioongozwa na Mkuu wa Jeshi hilo, CGP Jeremia Yorum Katungu walipomtembelea Jaji Mkuu ofisini kwake Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma. Walioketi kulia ni sehemu ya Viongozi wa Mahakama.

Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju akizungumza jambo na 
Kamishna Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini, (CGP) Jeremia Yorum Katungu (hayupo katika picha) na Viongozi wengine wa Jeshi hilo waliomtembelea Jaji Mkuu ofisini kwake Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Kamishna Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini, (CGP) Jeremia Yorum Katungu akifurahia jambo wakati wa mazungumzo na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania alipokutana na kufanya mazungumzo naye jana tarehe 19 Septemba, 2025 ofisini kwake Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.


Kamishna Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini, (CGP) Jeremia Yorum Katungu akisaini kitabu cha wageni alipowasili ofisini kwa Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju kwa lengo la kusalimiana na kujadiliana kuhusu masuala mbalimbali ya utendaji kazi wa Mahakama na Jeshi la Magereza.

Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza kutoka Jeshi Magereza nchini (CP) Nicodemus Tenga akizungumza jambo wakati wa mazungumzo kati ya Jaji Mkuu na Kamishna Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini yaliyofanyika jana tarehe 19 Septemba, 2025 Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

 Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. George Hubert (kushoto) akizungumza jambo wakati wa mazungumzo hayo. Kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama ambaye pia ni Msaidizi wa Jaji Mkuu, Mhe. Venance Mlingi.
Mazungumzo yakiendelea..

Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Kamishna Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini, (CGP) Jeremia Yorum Katungu (wa pili kushoto). Wa pili kulia ni Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza kutoka Jeshi Magereza nchini (CP) Nicodemus Tenga, wa kwanza kushoto ni Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. George Hubert.

(Picha na MARY GWERA, Mahakama)





 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni