Jumatano, 10 Septemba 2025

WADAU HAKI JINAI ‘WAPIKWA’ KUTHIBITI UHARIFU WA WANYAMAPORI

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Arusha

Kikao Kazi cha Wadau wa Haki Jinai kwenye uhifadhi wa Wanyamapori kinachofanyika kwenye Hoteli ya Mount Meru jijini hapa kimeinmgia siku ya pili huku washiriki wakipitishwa kwenye mada mbalimbali zinazolenga kuimarisha mapambano dhidi ya uharifu wa Wanyamapori.

Mada zilizowasilishwa zinahusu Matumizi ya Sayansi katika upatikanaji wa Haki: Jukumu la Sayansi Jinai ya Biolojia na Vinasaba vya Wanyamapori katika kesi za Uharifu Dhidi ya Wanyamapori.

Mada hiyo iliwasilishwa kwa pamoja na Mkemia kutoka Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Bi. Leticia Waitara na Wakili Mkuu wa Serikali, Bi Tarsila Gervas.

Katika wasilisho lao, wawezeshaji hao wamesisitiza kuwa ushahidi wa kisayansi katika mapambano ya uharifu wa Wanyamapori hauepukiki kwa sasa, kwani utasaidia kufikia uamuzi usiokuwa na mawaa.

Wameeleza pia kuwa matumizi ya Vina Saba [DNA] kwenye matukio ya Wanyamapori yanaweza kuthibiti changamoto wanazokabiliana nazo kwenye uhifadhi wa Wanyamapori.

Mada nyingine ilihusu Uendeshaji Mashtaka Kiitelijensia katika Uhalifu wa Wanyamapori; Kuimarisha Mkakati wa Uchunguzi na Mwitikio wa Kisheria kwenye Uhalifu wa Wanyamapori, ambayo iliwasilishwa na Bw. Elisifa Ngowi kutoka PAMS Foundation.

Katika wasilisho lake, Mzee Ngowi, pamoja na mambo mengine, ameelezea jinsi ya kutumia intelijensia kwenye upelelezi na umuhimu kwa wapelelezi kuweka kumbukumbu za kiupelelezi kuanzia kukamatwa kwa mtuhumiwa, ukusanyaji wa vielelezo na ushahidi wote kabla ya shauri kupelekwa mahakamani.

Mada nyingine ilihusu Wajibu wa Mahakama katika Ulinzi na Matumizi Endelevu ya Maliasili, ambayo imewasilishwa na Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Stella Mugasha.

Katika wasilisho hilo, Mhe. Mugasha amesisitiza kuwa Mahakama kwa Mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ndiyo yenye mamlaka ya mwisho kwenye utoaji wa haki nchini.

Amesema kuwa mchango wa Mahakama katika masuala ya uhifadhi wa Wanyamapori ni kutafsiri ipasavyo sheria zinazohusika ili kuhakikisha yale yote yanayoahidiwa na Serikali yanatekelezwa katika kulinda maliasili zilizopo.

Mhe. Mugasha ameeleza pia kuwa Mahakama ya Tanzania imeunda Mahakama maalum inayoshughulikia mashauri ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, yakiwemo yale yanayohusu uhalifu wa Wanyamapori na hivi karibuni Jaji Mkuu ametoa mamlaka katika kila Kanda kusikiliza mashauri kama hayo.

Mahakama nchini Tanzania ina jukumu muhimu katika kulinda na kuhakikisha matumizi endelevu ya maliasili kupitia utekelezaji wa sheria husika ambayo ni muhimu kwa kulinda urithi wa asili wa nchi na hatimaye kupata haki kwa asili na kukuza uchumi...

‘Jukumu chanya la Mahakama linaweza kuboreshwa zaidi ikiwa Wadau wengine watachukua hatua chanya katika uchunguzi wa haraka na madhubuti wa makosa ambayo ndiyo nguzo ya ufanisi wa mashtaka ya makosa yanayohusiana,’ amesema.

Mada nyingine zilihusu Mchango wa Utalii kwenye Uchumi wa Nchi; Faida na Changamoto, iliyowasilishwa na Kamishana Msaidizi, Bi. July Lyimo kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa [TANAPA]; Kutangaza Utalii kwa Njia ya Akili Unde nchini Tanzania iliyowaslishwa na Dkt. Hellen Maziku kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Mkazo wa Mahali pa Kazi na Utumiaji wa Akili Unde katika ulinzi wa Wanyamapori iliyowasilishwa na Dkt. Garvin Kweka.



Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Stella Mugasha [juu na chini] akiwasilisha mada kwenye kikao kazi hicho kilichofanyika jijini Arusha.


Bw. Elisifa Ngowi kutoka PAMS Foundation akiwasilisha mada.

Wakili Mkuu wa Serikali, Bi Tarsila Gervas akiwasilisha mada. Picha chini ni Mkemia kutoka Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Bi. Leticia Waitara.

Dkt. Hellen Maziku kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akiwasilisha mada.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi [katikati] akiongoza majadiliano baada ya uwasilishaji wa mada mbalimbali kwenye Kikao Kazi hicho.

Sehemu ya Majaji Wafawidhi [juu na picha mbili chini] wakifuatilia uwasilishaji wa mada mbalimbali wakati wa Kikao Kazi hicho. 




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni