● Asisitiza kuwa Dira ya Mahakama ni Haki Sawa kwa Wote Mapema Ipasavyo.
● Awataka wadau wa
Haki Madai kuzingatia haki, weledi na kujituma katika kutekeleza majukumu yao.
Na HABIBA MBARUKU, Mahakama-Dodoma
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju amewasisitiza wadau wa Haki Madai kuwajibika na kutekeleza wajibu wao ipasavyo ili kufikia malengo na kufanikisha ustawi wa wananchi ambalo ni jukumu la Serikali kwa mujibu wa Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mhe. Masaju aliyasema hayo jana tarehe 08 Oktoba, 2025 alipokuwa akifunga Mkutano wa wadau kuhusu mikakati na hatua zinazochukuliwa na Mahakama ya Tanzania kushughulikia mashauri ya kodi, biashara, mabenki na ushindani wa kibiashara, uliofanyika katika ukumbi wa mkutano wa Jaji Mkuu Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
"Nilikuwa naangalia hapa michango yote iliyotoka ni ile ya kujenga ambayo imetoka kwa nia njema, na inaonesha utayari wa sisi sote tulioko hapa kila mmoja kutekeleza wajibu wake kwa ufanisi ipasavyo ili malengo haya yafikiwe. Nilipokuwa nazungumza juu ya zile 'softwares' nilikuwa nimezingatia mahusiano ya kijamii, kisiasa na kiuchumi yanayoendelea kuwepo katika Taifa letu. Sisi tukiwa watendaji na watumishi wa umma, tuna wajibu sasa kwenda sambamba na kuwepo kwa uhusiano wa kijamii, kisiasa na kiuchumi ili tunapotekeleza wajibu wetu tuzingatie kwamba tunawajibika kufanikisha ustawi wa wananchi ambalo ndio jukumu la Serikali kwa mujibu wa Ibara ya 8 ya katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania" alisema Jaji Mkuu.
Aidha, Mhe. Masaju alisisitiza kuwa lengo la Mahakama ni kutoa haki sawa kwa wote mapema ipasavyo na kuwahimiza wadau wengine kama vile Benki Kuu na Chama cha Wanasheria Tanganyina kuwajibika ipasavyo, kujituma na kuwa wabunifu katika kutimiza majukumu yao kwa ufanisi.
"Sisi kwenye Mahakama labda lengo letu ni nini, lengo letu sisi ni haki sawa kwa wote mapema ipasavyo na lengo la TRAT ni nini, lengo la TRAB ni nini, lengo la Benki Kuu ni nini, lengo la TLS ni nini, lengo la wadau wote ni nini, kila mmoja akijipima akiangalia hiyo, kwa vyovyote vile atakuwa mwenye kujituma, mwenye ubunifu, mwenye kuwajibika, yaani atataka kutekelea majukumu yake kwa umahiri" alisisitiza Jaji Mkuu.
Mhe. Masaju aliongeza kuwa Taasisi zote zinazohusika na migogoro, utekelezaji wa majukumu yake utapaswa kuzingatia Katiba, Sheria na maadili ya utumishi kwenye sekta mbalimbali katika Taifa na kuwa kila mtu anawajibika kuifuata na kuitekeleza Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na sheria zake kwa mujibu wa Ibara ya 26 ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
"Mkakati wetu mkubwa ni kila Taasisi, Taasisi zote zinazohusika na migogoro na utekelezaji wa majukumu yake, zitapaswa tu kuzingatia Katiba, sheria na maadili yetu ya utumishi katika sehemu tunazotumikia katika Taifa hili, nazungumza juu ya uwajibikaji kwa sababu kila mtu anawajibika kuzifuata na kuzitekeleza Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na sheria zake, Ibara ya 26 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, ndicho kitu kinachoitwa utawala wa sheria, na sisi wote hapa tunafanya kazi kwa kufuata au kwa mujibu wa majukumu tuliyopewa kwa sheria mbalimbali," aliongeza Jaji Mkuu.
Jaji Mkuu pia alizungumzia suala la uwajibikaji na kujituma, na kuwataka wajumbe wote kujituma, kuwa waadilifu, kuwa waaminifu na kutimiza nidhamu ya kazi na kujitahidi kufikia malengo ya pamoja na malengo ya mtu mmoja mmoja ambayo yanaweza kusaidia katika kufikia malengo ya pamoja na malengo yaliyowekwa kwa mujibu wa sheria.
"Ukiangalia ule uwajibikaji, kwenye Ibara ya 25 ambayo napenda kuielezea, pale kuna mambo yamezungumzwa, kuna kujituma, uaminifu, na uaminifu. Tunaweza kuchukulia pia ndio uadilifu, halafu kutimiza nidhamu, nidhamu ya kazi yetu ni ipi, na kujitahidi kufikia malengo, malengo ya pamoja kwa mfano sisi wote hapa kwenye hili tunapaswa tuwe na malengo ya pamoja, lakini na malengo ya kwetu binafsi, ambayo yanaweza kupelekea kufikia malengo ya pamoja, lakini na yale malengo ambayo tumewekewa sasa kwa mujibu wa sheria na pamoja na yaliyowekwa na sheria, kwa mfano Mahakama ya Tanzania ni malengo yapi tuliyowekewa na sheria, Taasisi nyingine ni malengo yapi, kwa hiyo haya ni msingi tukayazingatia sana," alisema.
Jaji Mkuu pia alizungumzia suala la mabadiliko ya kifikra katika mfumo wa utekelezaji wa majukumu, akirejelea Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 ili kuhakikisha inatekelezwa kwa ufanisi.
Alisema kuwa, Serikali imeweka mfumo imara wa usimamizi unaozingatia malengo yake mahususi, malengo yake mahususi ni yapi, mfumo huu umekusudia kuhimiza uwajibikaji, ukihitaji uongozi ulio mahiri na makini katika ufuatiliaji, aidha mfumo unahimiza matumizi ya mbinu zinazotoa matokeo yanayopimika.
"Ndio maana lazima tukutane tuangalie hivi siku ile tulikubaliana kufanya kitu gani, tuone kama tumepiga hatua na wapi tulipokosea, twende tuchukue hatua tujirekebishe," alisema.
Jaji Mkuu pia aliongeza kuwa "msingi wa mkakati huu ni mabadiliko makubwa ya kifikra yakilenga vitendo badala ya maneno, na matokeo badala ya ahadi, uongozi, Taasisi pamoja na watendaji na wadau wote wanapaswa kuwajibika ili kutimiza malengo ya dira kwa ufanisi.
Alisema kwamba Taasisi imara na mifumo madhubuti inayolenga kuondoa uzembe, inayohimiza uwajibikaji na kuchochea ufanisi itakuwa nguzo kuu ya utekelezaji wa Dira ya 2050, ambayo imeweka mfumo madhubuti wa utawala unaohakikisha utekelezaji unafanyika kwa nidhamu, sera zinasomana, Taasisi zinakuwa imara na kila sekta na wadau wote wanashirikiana.
Aidha, Mhe. Masaju alisema kuwa mfumo wa kidigitali wa ufuatiliaji tathmini na kujifunza utawezesha utekelezaji himilivu utakaobadili misukosuko ya kiuchumi, mabadiliko ya tabia ya nchi na maendeleo ya kiteknolojia pamoja na matumizi ya akili unde.
"Matumizi ya teknolojia yanazoendelea kama vile akili unde, mifumo ya taarifa za kijiografia, uchambuzi wa data kwa wakati halisi yataleta ufanisi wa sera, ufuatiliaji na mgawanyo wa rasilimali na mwisho, ili kuimarisha uwajibikaji viashiria vya utendaji katika maeneo hayo vitatumika kufuatilia maendeleo. Ndicho alichokuwa anatukumbusha hapa Naibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, ili kuimarisha uwajibikaji viashiria vya utendaji vitatumika kufuatilia maendeleo, kutambua changamoto na kuboresha utendaji, " aliongeza Jaji Mkuu.
Kadhalika, Mhe. Masaju alisema kuwa, mfumo wa motisha na adhabu utaongeza uwajibikaji kwa watumishi, kuondoa uzembe pamoja na kuhakikisha kuwa utekelezaji wa majukumu unaleta matokeo yenye manufaa kwa Taifa.
"Mfumo wa motisha na adhabu utaimarisha utamaduni wa uwajibikaji ukihamasisha ubora na kuondoa uzembe na kuhakikisha kuwa utekelezaji unaleta matokeo yenye manufaa," alisisitiza.
Mkutano huo umejadili mikakati ya kuboresha utendaji kazi ambayo ni pamoja na wadau wote wa mnyororo wa haki pale inapowezekana watumie njia ya usuluhishi kutatua migogoro kwa mashauri ya kodi, biashara, mabenki na ushindani wa kibiashara kabla hayajafika mahakamani.
Kila Taasisi ambayo ni mdau wa mnyororo wa haki mahakamani iwajibikie ipasavyo kutekeleza jukumu lake kwa kuzingatia Katiba, Sheria na maadili ya utumishi wa Taasisi husika. Wadau wote wa haki madai wenye mashauri mahakamani, wawe tayari kuhudhuria na kuyaendesha kikamilifu ili kuwezesha haki kupatikana mapema ipasavyo.
Mahakama na wadau wa mnyororo wa haki waimarishe
mawasiliano miongoni mwao kwa lengo la kuchukua hatua haraka pale changamoto
zinapojitokeza.
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju akifunga Mkutano wa Wadau Kuhusu Mikakati na Hatua Zinazochukuliwa na Mahakama ya Tanzania Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki na Ushindani wa Kibiashara uliofanyika jana tarehe 08 Oktoba, 2025 kwenye ukumbi wa Mikutano wa Jaji Mkuu Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (wa pili kulia) akijadiliana jambo na baadhi ya Wadau wa Haki Madai walioshiriki katika Mkutano wa Wadau Kuhusu Mikakati na Hatua Zinazochukuliwa na Mahakama ya Tanzania Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki na Ushindani wa Kibiashara uliofanyika jana tarehe 08 Oktoba, 2025 kwenye ukumbi wa Mikutano wa Jaji Mkuu Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni