Ijumaa, 10 Oktoba 2025

JAJI KAHYOZA AFANYA ZIARA YA UKAGUZI WA MAHAKAMA KIGOMA

  • Awapongeza watumishi kwa kuchapa kazi, kutunza mazingira

Na AIDAN ROBERT-Mahakama, Kigoma

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Projestus Kahyoza, kwa siku tano kuanzia tarehe 3 Octoba, 2025 alifanya ziara ya ukaguzi wa Mahakama za Wilaya ili kuangalia maeneo mbalimbali, ikiwemo usikilizaji wa mashauri, utekelezaji wa maagizo ya Viongozi wa juu na utunzaji wa mazingira.

Akizungumza katika moja ya Mahakama sita alizokagua, Mhe. Kahyoza alisema “Nawapongeza kwa kuchapa kazi, umalizaji wa mashauri kwa kiwango kizuri ni jibu kuwa mnatimiza wajibu wenu vema. Nawapongeza kwa weledi, ushirikiano, kwa kuendelea kutunza maadili na nidhamu na kwa  utunzaji mzuri wa mazingira.”

Jaji Kahyoza aliendelea kusisitiza kuwa yapo maelekezo ya Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju yanayowataka kuongeza ushirikiano kwa wadau wa Mahakama, kulinda maadili na nidhamu za Maofisa Mahakama na kutoa kipaumbele cha kusikiliza mashauri ya kiuchumi, biashara na kuhakikisha nakala za hukumu zinatolewa kwa wakati.

Alitoa rai kwa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo Kanda ya Kigoma kuweke mkakati imara wa umalizaji wa mashauri kwa kiwango cha juu ili kuondoa na kuzuia mlundikano.

Naye, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa alimshukuru Jaji Kahyoza kwa pongezi na maelekezo yake kwa shughuli za usikilizaji wa mashauri kwa Mahakama za Kanda ya Kigoma.

Aliahidi kuongeza kasi ya usimamizi na ufuatiliaji wa karibu wa maelekezo yote ili utekelezaji wake uwe msaada mkubwa kwa Mahakama na wadau kwenye mnyororo wa utoaji haki kwa wakati.

Kwa upande wake, Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Kigoma, Bw. Filbert Matotay alisema kuwa ataendelea kuongeza kasi ya usimamizi wa shughuli za Mahakama katika Kanda, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mazingira ya watumishi yanaendelea kuboreshwa ili kumrahisishia kutimiza majukumu yake.

Alibainisha Mahakama katika Kanda hiyo itaendelea kutumia rasilimali zilizopo kuhakikisha shughuli za usikilizaji wa mashauri zinafanyika vizuri katika Mahakama zote kanda ya Kigoma.

Mahakama zilizokaguliwa katika ziara hiyo ni Mahakama za Wilaya Kigoma, Kibondo, Kasulu, Uvinza na Kakonko pamoja na Baraza la Aridhi Wilaya Kasulu.


Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Projestus Kahyoza akisisitiza jambo alipokuwa katika ziara ya ukaguzi wa Mahakama kwenye Kanda hiyo.

 

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Projestus Kahyoza akipanda mti wa matunda (Palachichi) katika Mahakama ya Wilaya Uvinza.

 Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Projestus Kahyoza (wa kwanza kulia) akisikiliza maelezo toka kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Buhigwe, Mhe. Venance Mwakitalu (katikati) kuhusu ubunifu wa utunzaji wa mazingira. Kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Mwanzo Manyovu, Mhe. Straton Mosha.

Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Kigoma, Bw. Filbert Matotay akisisitiza jambo kwa watumishi wa Mahakama ya Wilaya Kibondo kuhusu utendaji wa shughuli za Mahakama.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa akisisitiz jambo alipokuwa anaeleza hali ya ujenzi wa uzio wa Mahakama ya Wilaya Kasulu kwa Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Projestus Kahyoza.

 

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Kigoma, Mhe. Projestus Kahyoza (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Fadhili Mbelwa (kushoto), Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Kigoma, Bw. Filbert Matotay (kulia), Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Uvinza, Mhe. Misana Majula (wa kwanza kulia), Ofisa Tawala wa Mahakama ya Wilaya Uvinza, Bw. Tumaini Panga (wa kwanza kushoto) na waliosimama ni sehemu ya watumishi wa Mahakama ya Wilaya Uvinza.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni