Na HABIBA MBARUKU, Mahakama-Dodoma
Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani
amewataka Mahakimu Wakazi Wapya kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya uadilifu
huku akisisitiza kuwa uadilifu ndio msingi wa kujenga na kuendeleza imani ya
wananchi kwa Mahakama.
Akizungumza jana tarehe 07 Oktoba, 2025 wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mafunzo Elekezi kwa Mahakimu Wakazi Wapya 89 iliyofanyika
katika ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma, Mhe. Dkt. Siyani alisema kuwa, uadilifu
unajenga na kukuza imani ya Umma kwa Mahakama na katika kuhakikisha hilo
amewataka kuwa waadilifu, kuishi kiapo walichoapa ili waendelee kuwa Mahakimu wenye weledi kwa
kufanya kazi kwa kuzingatia haki bila upendeleo.
"Sifa
ya Hakimu pamoja na uwezo wa kufanya kazi ni uadilifu, hakimu mzuri ni yule
ambaye anaweza kufanya kazi yake ya uhakimu lakini ni muadilifu na uadilifu wa Hakimu
una faida nyingi pamoja na kukupa baraka, lakini uadilifu unajenga na kukuza
imani ya Umma kwa Mahakama," alisema Jaji Kiongozi.
Mhe.
Dkt. Siyani aliwahimiza Mahakimu hao kuwa watakapofika kwenye vituo vyao vya
kazi kila mmoja atoe mchango wake katika kutekeleza na kulinda imani ya Umma
kwa Mahakama kwa lengo la kuhakikisha wanakuwa sehemu ya kulinda heshima na
hadhi ya Mahakama nchini.
"Mimi
niwaase sana kila mmoja wetu atakapokwenda kwenye kituo atakachopangiwa siyo tu
kuhakikisha kwamba anajenga na kukuza hiyo Imani bali anaiendeleza hiyo imani
ambayo ipo lakini pia anajiuliza kila wakati haya ninayoyafanya, yanaiweka
Mahakama katika taswira ipi, hilo ni jambo la muhimu sana, jipimeni mchango
wenu katika kujenga, kukuza na kuendeleza imani ya Umma kwa Mahakama,"
alisema Jaji Kiongozi.
Aidha,
Mhe. Dkt. Siyani aliwakumbusha Mahakimu hao kuwa Tanzania ni nchi inayoongozwa
kwa mujibu wa Katiba, Sheria na maelekezo ya viongozi, hivyo ni lazima kila
mmoja afanye kazi kwa kuzingatia misingi hiyo bila kuingiliwa na ushawishi wa
kisiasa au kikundi chochote na kuwaasa wasigeuze Mahakama kuwa chombo cha kisiasa na wasijiunge na vikundi vya uaharakati
na kueleza kuwa ziko namna za kufikisha kero
na changamoto hivyo ni vyema Mahakimu
wakatumia njia hizo.
“Msigeuze
Mahakama kuwa chombo cha kisiasa, msigeuze Mahakama kuwa sehemu ya kufanyia
harakati zozote zile, tunazo sheria na tunao utamaduni, usijiunge kwenye
vikundi vya harakati ziko namna za kufikisha kero na manung'uniko yetu
zitumieni," alisema Jaji Kiongozi.
Mafunzo hayo yanaendeshwa kwa lengo la kuwajengea Mahakimu wapya uwezo wa kiutendaji, kimaadili na kisheria kabla ya kuanza kazi rasmi katika vituo mbalimbali vya kazi nchini.
Sehemu ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania walioshiriki kwenye hafla ya ufunguzi wa Mafunzo Elekezi kwa Mahakimu Wakazi wapya jana tarehe 07 Oktoba, 2025 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma. Wa kwanza kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Kuu ambaye pia ni Amidi wa Mahakama hiyo, Mhe. Imani Aboud, wa pili kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo, anayefuatia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Kuu, Mhe. Abdi Kagomba
Sehemu ya Mahakimu Wakazi wapya wakifuatilia kinachojiri wakati wa hafla ya Mafunzo Elekezi yanayotolewa kwao baada ya kuapishwa rasmi kushika wadhifa huo.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni