· Awataka kutambua nafasi ya Mungu katika kazi zao
· Awasisitiza kufanya kazi nyingine halali za kujipatia kipato ikiwa ni pamoja na Kilimo, Ufugaji…
Na MARY GWERA & HABIBA MBARUKU, Mahakama-Dodoma
Jaji Mkuu wa Mahakama
ya Tanzania, Mhe. George Masaju amefungua Mafunzo Elekezi kwa Mahakimu Wakazi
wapya huku akisema kuwa mafunzo hayo ambayo yatasheheni mada mbalimbali
yatahudhuriwa na viongozi wa dini lengo likiwa ni kujenga uwajibikaji, uzoefu,
kuimarisha ufanisi na kuongeza umahiri wa mahakimu wapya katika kutekeleza
majukumu yao ya utoaji haki kwa wananchi.
Mhe. Masaju aliyasema hayo jana tarehe 07 Oktoba, 2025
wakati akifungua Mafunzo Elekezi yanatolewa kwa Mahakimu Wakazi wapya 89 kwenye
ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
“Nimeangalia ratiba yenu na mafunzo ambayo mtayapata
kipindi hiki cha mafunzo elekezi, pamoja na mambo mengine yote yaliyoko pale
nimevutiwa na siku ya pili ya mafunzo haya, pale kutakuwa na muda wa mazungumzo
na Viongozi wetu wa dini wamealikwa kuja kuzungumza na ninyi na tumekuwa na
utaratibu huu kwa sasa mwaka wa tatu kila tunapoapisha tunawaita hawa viongozi
wa dini kuja kuzungumza na ninyi kuwatia moyo, kuwashauri,” alisema Jaji Mkuu.
Aidha, Mhe. Masaju aliwaeleza Mahakimu hao kuwa, Mwenyezi
Mungu ametoa maelekezo ya namna ya kuishi na namna ya kuhusiana na yeye na
namna ya kuhusiana na watu wengine.
“Mimi niwashauri watakapokuja kuzungumza na sisi
tuwasikilize kwa makini na kama kuna maswali waulizeni lakini wamekuja
kutujenga sana, mwelekeo wetu kuanzia sasa tangu tulipokula kiapo imejikita
namna tutazingatia miongozi ya Mwenyezi tunapotekeleza majukumu yetu ya
utumishi wa umma na sheria zile za Mungu hazipingani sana na zile za kwetu, kwa
mfano sheria za Mungu zinatuhimiza tupendane lakini pia zinatuhimiza tusile
rushwa, zinatuhimiza sisi tulio na majukumu ya kutoa haki tusipendelee,”
alisisitiza Jaji Mkuu.
Mhe. Masaju aliongeza kwa kuwakumbusha Mahakimu kuheshimu
siku za ibada za kila dini ambapo alisema, “Na sisi hao watu wa dini tunawapa
kipaumbele sana na utakumbuka hapa kila mmoja ana dini yake na siku ya kufanya
ibada, pengine wapo ambao wanafanya ibada siku ya Ijumaa, wengine siku za
Jumamosi lakini pia wapo wanaofanya ibada siku za Jumapili na pengine wapo
wanaofanya ibada siku nyingine pia lakini siku mahsusi ambazo zimetengwa kwa
ajili ya ibada hatujakatazwa kufanya ibada kila siku, kimsingi ibada ni haki
yako.”
Alisema, madhehebu ya dini yana mchango mkubwa katika katika
Taifa kwa ajili ya usalama wa jamii, amani katika jamii, maadili ya jamii na
umoja wa kitaifa.
Jaji Mkuu alibainisha kuwa, ‘Ibara ya 19 ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema, ‘uhuru wa kuamini dini mtu atakayo’,
Ibara ndogo ya 1 inasema kila mtu anastahili kuwa na uhuru wa mawazo, imani na
uchaguzi katika mambo ya dini pamoja na uhuru wa mtu kubadilisha dini au imani
yake, Ibara ndogo ya 2 inasema kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na kueneza
dini itakuwa ni huru na jambo la hiyari la mtu binafsi na shughuli za
uendeshaji wa jumuiya ya dini zitakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya nchi……’
Kadhalika, Mhe. Masaju alisisitiza juu ya suala la Uwajibikaji
ambalo ni moja ya kipaumbele cha tatu katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya
mwaka 2050. Aliongeza pia kufanya kazi kwa uaminifu.
"Suala la uwajibikaji, baadae mtakuja kusoma Dira ya
Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050, moja ya kipaumbele kikubwa sana ni
uwajibikaji, uwajibikaji ni kipaumbele cha tatu katika ile misingi mikuu ya Dira
ya Taifa ya Maendeleo 2050, uwajibikaji kwa watumishi wa Umma,"
alisisitiza Jaji Mkuu.
Aidha, Mhe. Masaju aliongeza kwamba, suala la Uwajibikaji
ni takwa la kisheria na kuwahimiza Mahakimu Wakazi kufanya kazi kwa kujituma na
kwa uaminifu katika utekelezaji wa shughuli halali na uzalishaji mali pamoja na
majukumu mengine kwa kuzingatia Dira ya Mahakama ya Utoaji haki sawa kwa wote
mapema ipasavyo.
"Na hapo ndipo tunapopata sisi utekelezaji wa Dira
yetu ya Mahakama inayosema, Haki sawa kwa wote mapema ipasavyo, tunaishi hiyo Dira
hatutaki haki icheleweshwe na nyie wenyewe mnasema haki iliyocheleweshwa ni
haki iliyonyimwa, tumeweka utaratibu sasa tungependa zile kesi ziwe
zinamalizika mapema sana isipokuwa kuwe na sababu za msingi," alisema Mhe.
Masaju.
Jaji Mkuu aliwataka pia kutimiza nidhamu ya kazi na
kuzingatia maadili ikiwa ni pamoja na kuvaa vizuri na kujitahidi kufikia
malengo ya uzalishaji mali ya mtu binafsi kama vile kilimo, ufugaji na yale
malengo yaliyowekwa na Sheria.
“Utapimwa kwa maadili yako pia hata unavyovaa, wewe
unategemewa kuwa kioo, na nimeona watu wengine wamevaa vizuri hapa na
wamejistiri na vichwa vyao, hayo ni mavazi ya heshima, endeleeni kuvaa
hivyohivyo msiseme wananipima wananiona mimi sijui mshamba,” alisisitiza.
Mhe. Masaju pia aliwataka kuzingatia vitendea kazi vya
aina mbili ambavyo ni ‘hardware’ na software’, ambavyo ni pamoja na kompyuta,
meza, vitabu vya sheria na vingine, “lakini mimi nataka kuwashirikisha vitendea
kazi ‘software’ ambayo sasa ni fikra ‘mindset’, ninyi ambao mmeitwa sasa na
mmekubali kuwa Mahakimu ili mtoe haki mkiwa mamlaka yenye kauli ya mwisho
kwenye utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, moja ya kitendea
kazi chenu cha muhimu itakuwa ‘sensitivity to justice’, muwiwe kuona haki
inatendeka, ameeleza kuwa haki maana yake ni uamuzi unaofanywa kwa mujibu na
kwa kuzingatia Katiba, Kanuni na Sheria za Nchi na kwa mujibu wa ushahidi
ulioletwa Mahakamani.”
Aliongeza pia, kitendea kazi kingine ni uwajibikaji
ambapo amesisitiza kufanya kwa kujituma na kwa uaminifu, uadilifu kama kitendea
kazi kingine ambapo amewataka kuwa na uwezo endelevu wa kufanya kazi, kuwa
wabunifu na wenye kuchukua hatua za mapema katika kufanya maamuzi na kutatua
vikwazo na changamoto wakati wa kutimiza majukumu yao ili kuimarisha ufanisi
pamoja na Uzalendo wa Taifa.
Makundi mbalimbali ya Mahakimu Wakazi wapya wakisikiliza hotuba ya ufunguzi wa Mafunzo Elekezi iliyokuwa ikitolewa na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (hayupo katika picha).
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani akitoa neno la utangulizi wakati wa ufunguzi wa Mafunzo Elekezi kwa Mahakimu Wakazi wapya jana tarehe 07 Oktoba, 2025 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni