Ijumaa, 14 Novemba 2025

WATUMISHI WAPYA WA MAHAKAMA SIMIYU WAPIGWA MSASA

Na NAUMI SHEKILINDI, Mahakama-Simiyu

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. John Rugalema Kahyoza amefungua mafunzo kwa watumishi wapya wa Mahakama wa kada mbalimbali walioajiriwa hivi karibuni lengo likiwa ni  kuwajenga watumishi hao waweze kuwa bora wakiwa katika utumishi wao kwa kuwa waadilifu, wawajibikaji, wafanisi na wenye bidii ya kazi.

Mafunzo hayo yaliyofunguliwa jana tarehe 13 Novemba, 20254 yameandaliwa na Ofisi ya Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu yakiongozwa na Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, Bw. Gasto Kanyairita.

Aidha, Mhe. Kahyoza alionesha kufurahishwa na maandalizi ya mafunzo hayo na kusema kuwa, yatawafanya watumishi wa ajira mpya wawe bora zaidi wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

Jaji Mfawidhi huyo alitoa mada kuhusu (non-Judicial Staff na Judicial Officers) kwa kueleza namna muundo ulivyoanzishwa na sababu za kuanzishwa kwake na mwisho alisisitiza kwamba watumishi wote wanajenga nyumba moja ambayo ni Mahakama ya Tanzania.

Kadhalika, watumishi hao wamefundishwa namna ya kujipatia kipato cha ziada bila kuathiri utendaji wao wa kazi.

Mafunzo hayo yalitolewa na wakufunzi mbalimbali ambao ni Maafisa Tawala/Utumishi na Wahasibu kutoka Wilaya mbalimbali ndani ya Mkoa wa Simiyu ambao wamewahimiza watumishi hao kuwa waadilifu, wawajibikaji, wafanisi, wenye bidii ya kazi na tabia njema.

Mfanzo hayo yalifungwa na Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, Bw. Gasto Kanyairita ambaye aliwaasa watumishi hao Kwenda kuyaishi yale yote waliofundishwa.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. John  Kahyoza (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi ambao ni ajira mpya walioajiriwa Septemba mwaka huu.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. John Rugalema Kahyoza akiwa katika picha ya pamoja na Wawezeshaji wa mafunzo kwa ajira mpya yaliyofanyika jana tarehe 13 Novemba, 2025.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni