· Asisitiza Utawala wa Sheria ni moja ya misingi ya mafanikio
Na
MARY GWERA, Mahakama-Dodoma
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita itashirikiana kwa dhati na Mahakama ya Tanzania katika uboreshaji wa miundombinu ya majengo, vitendea kazi, watumishi na kuimarisha
matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuuwezesha Mhimili huo kutoa haki kwa wananchi mapema ipasavyo.
Rais
Samia ameeleza hayo leo tarehe 14 Novemba, 2025 jijini Dodoma wakati akitoa
hotuba ya Ufunguzi rasmi wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Msingi
mwingine wa mafanikio yote haya ni utawala wa sheria, ahadi yetu ni kuwa
Serikali itashirikiana kwa dhati na Mahakama ya Tanzania kuhakikisha haki
inapatikana kwa watu wote na kwa wakati,” amesema Mhe. Dkt. Samia.
Ameongeza
kwamba, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili Mahakama iweze
kutekeleza wajibu wake kwa ufanisi.
Aidha,
Rais Samia amesema, “tutasimamia utekelezaji kamili wa mapendekezo ya Tume ya
Rais ya kuangalia namna ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai. Tutaendelea kufanya
mageuzi na maboresho katika taasisi zote zinazoshughulikia masuala ya Haki
Jinai ili ziweze kukabiliana na vitendo vyote vya uhalifu.”
Mhe.
Dkt. Samia ameahidi pia, Serikali itakamilisha tafsiri ya sheria zote kwa
lugha ya Kiswahili, ikiwa ni hatua muhimu ya kuhakikisha kuwa wananchi wanaelewa
kwa urahisi sheria za nchi.
Kadhalika,
Mhe. Dkt. Samia ameeleza kuwa, Serikali itaendelea kushirikiana na wadau
mbalimbali katika Sekta ya Sheria, ikiwemo Chama cha Wanasheria Tanganyika
(TLS) pamoja na asasi zingine ili kuwezesha upatikanaji wa huduma na msaada wa
kisheria kwa wananchi, na kusema kwamba manufaa ya huduma hiyo yameonekana
bayana katika kipindi kilichopita katika utatuzi wa changamoto mbalimbali
zinazowakabili wananchi.
Sekta
nyingine ambazo Rais Samia amegusia katika hotuba yake na kuahidi kuboresha zaidi ni pamoja na Afya,
Elimu, Madini, Kilimo, Uvuvi na nyingine.
Viongozi mbalimbali wa Serikali, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wabunge na wengine akiwemo Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju na Jaji Mkuu wa Mahkama Kuu ya Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdallah wameshiriki katika ufunguzi wa Bunge la 13.







Hakuna maoni:
Chapisha Maoni