Jumatatu, 17 Novemba 2025

MSAJILI MKUU ARIDHISHWA NA HATUA ILIYOFIKIWA, MRADI WA UJENZI WA 'IJC' SIMIYU

  •  Amsisitiza Mkandarasi kuongeza bidii kukamilisha mradi huo

Na NAUMI SHEKILINDI, Mahakama-Simiyu

Msajili Mkuu wa  Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya amekiri kuridhishwa na maendeleo ya Mradi wa Ujenzi wa Jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Simiyu ambao ulikuwa umefikia asilimia 92 hadi kukamilika kwake wakati alipotembelea Mradi huo.

Hivi karibuni, Mhe. Nkya alitembelea Mradi wa Ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kinachojengwa Mkoani Simiyu ili kujionea maendeleo ya ujenzi wa Kituo hicho.

Baada ya ukaguzi, Msajili Mkuu alimsisitiza Mkandarasi kuongeza bidii kwa kumalizia asilimia zilizobaki ili kuweza kuanza matumizi ya jengo hilo mapema iwezekanavyo.

Naye Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, Mhe. Martha Mahumbuga alimkaribisha Msajili Mkuu na kumsomea taarifa ya utendaji kazi katika Mkoa huo.

Aidha, Msajili Mkuu alionesha kufurahishwa na ushirikiano uliopo baina ya ‘Judicial na Non-Judicial Officers’ Mkoani humo, “nimependa namna mnavyofanya kazi kwa ushirikiano na hii imejidhihirisha hata kupitia taarifa yenu mlionisomea, hongereni sana Simiyu,” alisema Mhe. Nkya.

Msajili Mkuu aliwashukuru watumishi wa Mahakama Simiyu kwa ukaribisho mzuri alipotembelea Mahakama hiyo.

  Muonekano wa Jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Simiyu lililopo katika hatua za mwisho za ujenzi wake. 


Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya akisaini kitabu cha wageni alipowasili hivi karibuni katika Ofisi ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama kutoka Makao Makuu, Mahakama Shinyanga na Simiyu. Wa pili kulia ni Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga, Mhe. Gadiel Mariki, wa kwanza kulia ni Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, Bw. Gasto Kanyairita, wa pili kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, Mhe. Martha Mahumbuga na wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Bariadi, Mhe. Caroline Kiliwa.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni