Na. MUKSINI NAKUVAMBA - Mahakama, Mbeya
Mahakama
ya Wilaya Mbeya hivi karibuni Novemba, 2025 ilifanya hafla ya kuwaaga watumishi
wastaafu wa Mahakama ikiwa ni ishara ya kuwaenzi kwa utumishi wao uliotukuka na
kuwapongeza kwa jitihada zao za kulitumikia Taifa kwa kipindi chote cha
utumishi wao.
Akizungumza
katika hafla hiyo Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Mbeya Mhe. Said Kalunde aliipongeza Mahakama ya Wilaya ya Mbeya kwa kuandaa
hafla hiyo.
“Niwapongeze
sana Mahakama ya Wilaya Mbeya kwa kufanikisha kufanya jambo hili kubwa na
muhimu la kuona thamani ya wenzetu tuliokuwa nao katika utumishi kuwaaga kwa
pamoja kwa kuwaandalia hafla hii,” alisema Mhe. Kalunde.
Mhe.
Kalunde aliongezea kuwa, hafla hiyo ina lengo la kutambua mchango wa watumishi hao
wastaafu ambao kwa kipindi chote walikuwa waadilifu na wachapakazi ambao waliitumikia
Mahakama, Serikali na Taifa kwa ujumla.
“Ndugu
zetu mnaondoka katika utumishi wa Umma tunaomba tuendeleze undugu wetu na
upendo wetu, pale mtakapokuwa na shughuli zenu msisite kutualika nasi pia
tutaendelea kuwashirikisha kwenye shughuli zetu na tunawaomba mjumuike nasi” aliongezea
Mhe. Kalunde
Akitoa
neno la shukurani mmoja wa wastaafu hao, Afisa Hesabu Mahakama ya Wilaya Mbeya
Bi. Magreth Kasanga alisema mioyo yao ina furaha isiyo kifani kama wastaafu
walioutumikia Umma na Taifa kwa ujumla kwa uadilifu na mioyo ya kujituma kwa
zaidi ya miaka 30 hadi kufikia hatua hiyo.
“Tunashukuru
sana kwa upendo wenu wa dhati mliotuonesha viongozi wetu na watumishi wenzetu
tuliokuwa pamoja kwenye majukumu mbalimbali ya kiutumishi, kwa hakika sisi siyo
wakamilifu tunaomba radhi kwa yale tuliyowakosea mtusamehe nasi pia kwa umoja
wetu kwa mioyo yetu mikunjufu tumewasameheni nyote,” alisema Bi. Magreth
Kasanga.
Bi.
Kasanga aliongeza kuwa angependa kutoa nasaha fupi kwa watumishi wanaoendelea
na utumishi wa Umma, waendelee kuchapa kazi kwa bidii na kuwa wastahmilivu
wanapokumbana na changamoto mbalimbali za kazini.
“Ninawasihi
watumishi wenzangu ambao mnaendelea na utumishi wa Umma muendelee kuchapa kazi
kwa bidii, uaminifu na uadilifu katika kuutumikia Umma wa Watanzania, muwe na
uvumilivu, hekima, busara wakati wote muwapo kwenye majukumu yenu, nimalizie
kwa kusema ukiona nyani kazeeka kakwepa mishale mingi” aliongezea Bi. Kasanga.
Hafla
hiyo iliyoandaliwa na Mahakama ya Wilaya Mbeya ikishirikiana na Mahakama zake
za mwanzo, hafla ambayo ilihudhuriwa pia na wawakilishi kutoka Mahakama Kuu Kanda
ya Mbeya, Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, Mawakili wa Serikali, Mawakili wa Kujitegemea,
Madalali wa Mahakama pamoja na ndugu na jamaa wa karibu wa waagwa hao.
Watumishi
hao walioagwa katika hafla hiyo walikuwa ni Bi. Magreth Kasanga Afisa hesabu
Mahakama ya Wilaya Mbeya, Bi. Leah Mwakaguta Msaidizi wa ofisi Mahakama ya Wilaya
Mbeya, Bi. Siyoni Kasunga Msaidizi wa kumbukumbu Mahakama ya mwanzo Mwanjelwa, Bi.
Eugenia Mataula msaidizi wa ofisi Mahakama ya mwanzo Mbalizi na Bi. Tabu
Msaidizi wa Hesabu Mahakama ya Mwanzo Uyole.
Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Said Kalunde akitoa hotuba ya kuwapongeza watumishi wastaafu wa Mahakama ya Wilaya ya Mbeya wakati wa kuwaaga kwenye hafla hiyo.
Sehemu ya Watumishi wastaafu ambao walikuwa wanaagwa kwenye hafla hiyo
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni