Na. REHEMA AWET –Mahakama, Mwanza
Msajili
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya, amefanya ziara ya kikazi mkoani
Mwanza kwa lengo la kukagua maendeleo ya miradi ya ujenzi wa miundombinu ya Mahakama
na kusisitiza matumizi ya mifumo ya kidijitali kuwa sehemu ya miundombinu hiyo
katika utoaji wa huduma za kimahakama.
Katika
ziara hiyo, Mhe Nkya ametembelea na kukagua jengo linalokarabatiwa
litakalotumika kama Mahakama Kuu–Kitengo
cha Familia (Family Court), ambapo ameelezea kuridhishwa kwake na hatua
zilizofikiwa katika utekelezaji wa ukarabati huo.
Mhe.
Nkya amesema uanzishwaji wa kitengo hicho utarahisisha upatikanaji wa huduma za
kimahakama kwa wananchi wanaohusiana na mashauri ya kifamilia, ikiwa ni sehemu
ya jitihada za Mahakama ya Tanzania kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.
Aidha,
Msajili Mkuu ametembelea Mahakama ya
Wilaya ya Nyamagana, ambako amekutana na watumishi wa mahakama hiyo na
kusisitiza umuhimu wa kutumia Mfumo wa
Usimamizi wa Mashauri kwa njia ya Kielektroniki (eCMS) ili kuongeza
uwazi, ufanisi na kasi katika utoaji wa haki.
Mhe.
Nkya pia ametembelea Mahakama ya Mwanzo
Kisesa, iliyopata uharibifu baada ya kuchomwa
moto kufuatia vurugu zilizotokea baada ya uchaguzi Mkuu. Akiwa katika eneo
hilo, ameelezea dhamira ya Mahakama kuhakikisha huduma zinarejea haraka kwa
wananchi huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wadau wote katika
kulinda mali na miundombinu ya Mahakama.
Ziara
hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa Mahakama ya Tanzania wa kuimarisha
miundombinu, kuendeleza matumizi ya teknolojia, na kuhakikisha utoaji wa haki
unafanyika kwa wakati, kwa uwazi na kwa gharama nafuu.
Msimamizi wa Mradi Mha. Daniel (kwanza
kulia) akitoa taarifa ya Maendeleo ya mradi kwa Msajili Mkuu wa Mahakama Mhe.
Eva Nkya(pili kulia). Wengine katika picha ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu
Kanda ya Mwanza Mhe. Crisencia Kisongo(tatu kulia), Hakimu Mkazi Mfawidhi wa
Mahakama ya Wilaya Nyamagana Mhe. Ramla Shehagilo(kwanza kushoto)
Msajili Mkuu wa
Mahakama, Mhe. Eva Nkya (Pili kulia) akitoa ushauri kuhusu maboresho
yanayofanyika katika ukarabati wa Mahakama Kuu kitengo cha familia. Wengine katika
picha ni Mhandisi msimamizi wa mradi Bw. Daniel (kwanza kulia), Katibu wa
Msajili Kuu wa Mahakama Mhe Jovin Bishanga (tatu kulia) na Naibu Msajili wa
Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza Mhe. CrIsencia
Kisongo.
Muonekano wa Jengo la Mahakama kuu
Kanda ya Mwanza kitengo cha familia linalofanyiwa ukarabati.
Muonekano wa Jengo la Mahakama kuu
Kanda ya Mwanza kitengo cha familia linalofanyiwa ukarabati.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni