- Mahakama ya Tanzania haitavumilia vitendo vya uvivu, uzembe, ubadhirifu, nidhamu mbovu
·
Mjiendeleze dunia
inabadilika kwa kasi sana
Na. HABIBA MBARUKU – Mahakama, Dodoma
Mtendaji
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Prof. Elisante Ole Gabriel amewasisitiza Waajiriwa
Wapya wa Mahakama katika kada mbalimbali kujituma katika kuleta matokeo yenye
tija na kuweka wazi kuwa Mahakama ya Tanzania haitavumilii matukio ya uzembe,
uvivu, ubadhirifu na nidhamu mbovu kwa watumishi wote wa Mahakama.
Prof.
Ole Gabriel ameyasema hayo alipokua akifungua Mafunzo Elekezi kwa Watumishi Wapya
wa Mahakama wa Kada Mbalimbali, yaliyofanyika leo tarehe 17 Novemba, 2025
katika ukumbi wa Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.
Akizungumza
wakati wa hotuba yake Prof. Ole Gabriel amewataka waajiriwa hao kujituma na kujiendeleza
kielimu huku wakizingatia mabadiliko ya kasi ya dunia, huku akiwasisitiza na
kuwashauri kujiendeleza katika kada tofauti na walizo nazo sasa.
“Ningeomba
pia mjikite katika matokeo yenye tija, Mahakama hatuna uvumilivu na watu
wavivu, wazembe, ubadhilifu na nidhamu mbovu , hayo manne hatuna huruma nayo,
naomba sana mnapojitunza muhakikishe kwamba mnajiweka vizuri katika hilo lakini pia mjiendeleze kwa sababu
dunia inabadilika kwa kasi kubwa sana kama umeingia hapa na Diploma au Degree
ya kwanza songa mbele jitahidi kujiendeleza zaidi na mimi nawashauri mfikiri
suala linaloitwa Diagonal Career Development, siyo lazima uende vertical
unaweza ukaongeza vitu vingine itakupa tija zaidi,” ameongeza Mtendaji Mkuu.
Akizungumza
kuhusu matumizi ya TEHAMA Prof. Ole Gabriel amesema kuwa, Mahakama kwa sasa ni miongoni
mwa Taasisi ambazo zimepiga hatua kubwa katika matumizi ya TEHAMA akiweza wazi
mabadiliko makubwa ya matumizi ya TEHAMA katika Mahakama nchini na kuwataka
waajiriwa wapya kujiendeleza kwa nguvu kubwa ili kuwa mahiri katika matumizi ya
TEHAMA.
“Mahakama
kwa sasa ni moja ya Taasisi ambazo zimepiga hatua kubwa sana kwenye matumizi ya
TEHAMA, miaka ile tumezoea makaratasi yanatumika na vitu kama hivyo lakini kwa
sasa Mahakama imejitanabaisha na ndio Taasisi ya kwanza nchini kwa matumizi ya
TEHAMA nawaomba sana mjitahidi sana sana kujiendeleza kadri iwezekanayo, kuwa
mahiri katika matumizi ya TEHAMA,” amesema Prof. Ole Gabriel.
Ameongeza
kuwa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa fursa ya ajira ili
kuongeza kasi ya utendaji wa watumishi kuwatumikia wananchi zaidi ya milioni 60
ambao wanategemea huduma ya Mahakama, na huku akieleza kuwa Mahakama ni chombo
cha juu kabisa katika utoaji wa haki kama inavyoelezwa katika Ibara ya 107 A ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan
inatupa fursa ya ajira ili tuweze kuongeza utendaji wetu kwa kuwatumikia
wananchi zaidi ya milioni 60 ya watanzania wanaotegemea Mahakama iwahudumie…
Mkumbuke
pia kwamba, Mahakama ndiyo chombo cha juu kabisa katika utoaji wa haki Ibara ya
107 A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inafafanua. Usije Mahakama
kwa kudai umekuja kutunza kumbukumbu, unapoingia Mahakama mara zote jifikirie
kwamba na wewe unasaidia uendeshaji wa mashauri kwa ajili ya haki kupatikana
hilo ndilo jukumu letu kubwa,” amesisitiza Prof. Ole Gabriel.
Aidha,
Prof. Ole Gabriel amesisitiza mambo saba muhimu katika utendaji kazi huku
akigusia kuhusu suala la umahiri katika kujifunza kasi ya teknolojia, kujifunza
kuishi na watu wengine akiwataka mara zote kujiuliza kuhusu michango wanayotoa
katika sehemu ambayo wapo, amewakumbusha kuhusu suala la kutunza muda kwa
sababu mafanikio yoyote yale yanatokana na utunzaji wa muda
Vilevile,
Prof. Ole Gabriel amewataka waajiriwa hao wapya kujiuliza kuwa wataifanyia nini
Mahakama ya Tanzania na siyo Mahakama ya Tanzania itawafanyia nini, huku
akiwataka kuwa tayari kufanya kazi mahali popote ndani na nje ya Tanzania
akisema kuwa lipo tatizo la watu kupinga sehemu za kazi walizopangiwa.
Sambamba
na hayo, Prof. Ole Gabriel ametoa tahadhari katika matumizi ya TEHAMA hasa
katika matumizi ya mitandao ya kijamii akiwataka watumishi wapya kuwa makini
wanapotumia mitandao ya kijamii, lakini pia wakizingatia namna ya uzungumzaji,
uchapishaji wa maudhui mtandaoni, na uvaaji wa mavazi yenye maadili.
Ameongeza
kuwa watumishi wapya wanapaswa kujali Itifaki, akieleza kuwa Itifaki ni
kuhakikisha kuwa unafuata na kutekeleza utaratibu wa mila na desturi ya mahali
husika, aidha amewasisitiza waajiriwa wapya kulipa kipaumbele suala la kuandaa
mazingira mazuri baada ya kustaafu.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa Mahakama ya
Tanzania, Bi. Beatrice Patrick amesema kuwa mafunzo hayo yatakayodumu kuanzia
tarehe 17 Novemba hadi tarehe 03 Disemba 2025, yatatoa fursa kwa waajiriwa
wapya 474 kujifunza kuhusu Muundo wa Mahakama, sheria za utumishi wa umma,
kanuni taratibu na miongozo iliyopo katika utumishi wa umma.
Aidha, kujua utamaduni wa Mahakama ya
Tanzania, historia ya Mahakama, Mpango Mkakati wa Mahakama, Dira ya Maendeleo
ya Taifa 20250, majukumu ya Tume ya Utumishi wa Mahakama, kuwaandaa waajiriwa
wapya kiuwekezaji baada ya kustaafu, vilevile, mafunzo kwa ajili ya kutoa
msongo wa Mawazo, jinsia, uzalendo, itifaki, mfumo wa kupima utendaji, utunzaji
wa taarifa mbalimbali na maelekezo maalumu ya mifumo ya TEHAMA inayotumika na
Mahakama kutoa huduma kwa wananchi.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Prof. Elisante Ole Gabriel amewasisitiza Waajiriwa Wapya wa Mahakama katika kada mbalimbali kujituma katika kuleta matokeo yenye tija alipokuwa akifungua Mafunzo Elekezi ya siku tano kwa kada ya wasaidizi wa kumbukumbu wa Mahakama nchini.











Hakuna maoni:
Chapisha Maoni